Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tetemeko la ardhi laua 1,000 Myanmar, maelfu wajeruhiwa

Naypyidaw, Myanmar. Zaidi ya watu 1,000 wameripotiwa kufa kutokana na tetemeko la ardhi nchini Myanmar, huku kukiwa na hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuzidi mara 10 kutokana na nguvu za tetemeko hilo.

Kwa mujibu wa taarifa, tetemeko hilo lenye kiwango cha 7.7, pia limeathiri nchi za Bangladeshi, India, Laosi, Tailandi na China.

Taarifa za Huduma ya Jiolojia ya Marekani zimesema tetemeko la Myanmar la Ijumaa Machi 28, 2025 ni lenye nguvu zaidi kuliko lililoshuhudiwa nchini mwaka 1912.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, tetemeko mbali na kusababisha vifo, pia limesababisha majeruhi ya watu 2,300, kuporomoka kwa majengo na inaaminika watu wengi bado wamefukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoanguka.

Taarifa kutoka Serikali ya kijeshi ya Myanmar zimeeleza kuwa uharibifu mkubwa umejitokeza katika maeneo ya Mandalay na miji mingine ya kaskazini, huku mamia ya watu wakiwa hawajulikani walipo.

Tetemeko hilo, lililokuwa na ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter, lilitokea karibu na mji wa Sagaing, kilomita 12 kutoka mji wa Mandalay.

Mandalay, mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar, umeathiriwa sana na tetemeko hilo.

Picha na video kutoka eneo la tukio zimeonyesha majengo mengi yakiwa yameporomoka na kuwa vifusi, huku wafanyakazi wa uokoaji wakifanya juhudi kuwaokoa watu waliofukiwa na vifusi hivyo.

Imeelezwa idadi ya vifo imeendelea kuongezeka kutokana na ugumu wa kufikia maeneo yaliyoathirika, hasa kutokana na uharibifu wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na barabara, madaraja,na huduma za mawasiliano.

Hali ya hatari imetangazwa katika mikoa sita ya Myanmar na maelfu ya familia zinahitaji msaada wa dharura kutokana na kushindwa kwa miundombinu muhimu ya usafiri na huduma za afya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Serikali ya kijeshi, vifo zaidi ya 694 vimethibitishwa katika mji wa Mandalay, na majeruhi zaidi ya 1,600 kutoka katika miji mbalimbali.

Tetemeko hilo limesababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, hospitali, shule na majengo ya umma. Maji ya kunywa na huduma za afya pia zimeathiriwa.

Serikali mbalimbali na mashirika ya misaada ya kimataifa yameonyesha nia ya kutoa msaada kwa Myanmar.

India, Ufaransa, Umoja wa Ulaya, na Marekani zote zimetangaza kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa tetemeko.

Rais wa Marekani, Donald Trump pia ametangaza kwamba Marekani itatoa msaada katika kukabiliana na athari za tetemeko hili kubwa la ardhi.

Nchi nyingine nyingi, ikiwemo Japan na Australia, zimetangaza kutoa msaada wa kibinadamu na vifaa vya dharura.

Shirika la Afya Duniani (WHO) pia limetangaza kwamba litaongeza juhudi zake za kutoa msaada wa afya kwa waathirika na lipo tayari kupeleka vifaa vya matibabu kutoka kituo chake cha Dubai.

Hata hivyo, Serikali ya Myanmar, ambayo inakumbwa na vikwazo vya kimataifa kutokana na utawala wake wa kijeshi, inaendelea kukutana na changamoto za kiutawala na kidiplomasia.


Tetemeko la Thailand

Kwa upande wa Thailand, tetemeko hilo pia limeiathiri mji mkuu Bangkok, ambapo vifo 10 vimethibitishwa na watu wengine 16 kujeruhiwa.

Aidha, watu 101 wanaripotiwa kuwa hawajulikani walipo na uharibifu mkubwa umeonekana katika maeneo matatu ya ujenzi, ikiwemo ghorofa za juu.

Baada ya tetemeko kubwa, kulikuwa na matetemeko madogo ya baadaye, mojawapo likiwa na ukubwa wa 6.4 katika kipimo cha Richter.

Tetemeko hili limeonyesha changamoto kubwa zinazokumba mataifa ya kusini mashariki mwa Asia katika kushughulikia matukio makubwa ya kiasili.

Wahudumu wa dharura nchini Thailand wamethibitisha watu kadhaa wamefukiwa kwenye vifusi kufuatia tetemeko la ardh.

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa tetemeko lenye ukubwa wa kipimo cha Ritcher 7.7 limeukumba mji mkuu wa Bangkok, Thailand saa 7:30 mchana (saa za Thailand). Idara ya dharura nchini Thailand pia imesema watu wengine wanahofiwa kufukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka na shughuli ya uokoaji inaendelea.

Polisi nchini Thailand imesema idadi kamili ya watu waliokumbwa na maafa kutokana na kuporomoka kwa jengo hilo karibu na soko maarufu la Chatuchak bado haijajulikana na hakukuwa na taarifa za mara moja kuhusu ni wafanyakazi wangapi waliokuwapo kwenye eneo la ujenzi wakati huo.

Video inayosambaa mitandaoni inaonyesha jengo la ghorofa lililokuwa na kreni juu yake likiporomoka na kusababisha wingu kubwa la vumbi, huku watu waliokuwa wakitazama wakipiga kelele na kukimbia kwa hofu.

Wakazi wa Bangkok waliotoka nje ya majengo yao walipewa onyo la kubaki nje kwa tahadhari dhidi ya matetemeko mengine yanayoweza kufuata.

Mfanyakazi wa Idara ya Dharura, Songwut Wangpon, akizungumza pembeni ya kifusi cha jengo moja la ghorofa lililoporomoka amesema kuwa watu wengine saba wamepatikana wakiwa hai.

Mtalii kutoka Scotland, Fraser Morton, aliyekuwa akinunua bidhaa kwenye moja ya maduka makubwa jijini Bangkok amesema: “Kwa ghafla, jengo lote lilianza kutikisika. Ghafla, vilisikika mayowe na hali ya hofu ikatawala.”

Ameongeza: “Nilianza kutembea kwa utulivu mwanzoni, lakini baadaye jengo lilianza kutikisika vibaya sana. Kulikuwa na mayowe mengi, watu walikuwa wakikimbia ovyo, wengine wakishuka ngazi za umeme kwa njia isiyo sahihi, huku kelele za vitu vikidondoka zikiwa kila mahali.”

Maelfu ya watu walimiminika kwenye bustani ya Benjasiri kutoka kwenye maduka makubwa, majengo marefu na majengo ya makazi yaliyoko kando ya barabara ya Sukhumvit, moja ya maeneo yenye shughuli nyingi jijini Bangkok.

Watu wengi walikuwa wakizungumza kwa simu wakijaribu kuwasiliana na wapendwa wao, huku wengine wakijikinga na jua kali la alasiri. Baadhi yao walikuwa wakitazama kwa hofu majengo marefu yaliyojaa katika sehemu hiyo yenye msongamano mkubwa wa watu.

“Nilitoka nje na kisha nikatazama juu, nikaona jengo likitikisika, vumbi na vipande vikianguka – ilikuwa hali ya kutisha sana,” amesema Morton.

Sauti za ving’ora zimeenea katika jiji la Bangkok huku barabara zikifurika magari, na kusababisha msongamano mkubwa.

Mfumo wa usafiri wa treni za umeme na njia ya chini ya ardhi vilifungwa. Halmashauri ya jiji hilo ilitangaza Bangkok kuwa eneo la maafa ili kuwezesha msaada wa dharura na uratibu wa huduma za uokoaji.

Kwa upande wake, mtalii kutoka Uingereza aliyekuwa kwenye baa ya barabarani, Paul Vincent, amesema baada ya kutokea tetemeko hilo watu walifurika mtaani kwa hofu ya kutokea mtikisiko mwingine.

Alisema alipojitokeza mtaani, aliona jengo refu likiyumba, huku maji yakimwagika kutoka kwenye bwawa la juu ya jengo hilo.

“Nilipoona jengo hilo, oh Mungu wangu, ndipo nilipotambua ukubwa wa hali hii. Watu walikuwa wakilia mitaani, hali ya hofu ilikuwa mbaya sana,” amesema Vincent.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari.