Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sabasaba ya ghasia nchini Kenya, Gen-Z waingia tena barabarani

Muktasari:

  • Julai 7, 1990, yalifanyika maandamano ya kitaifa katika Uwanja wa Kamukunji Nairobi nchini Kenya, wananchi walikuwa wakidai uchaguzi huru wakati wa utawala wa Rais Daniel Arap Moi. Sasa ni miaka 35 imepita huku Gen Z wakiadhimisha siku hiyo kwa kufanya maandamano hayo

Nairobi. Hali ni tete nchini Kenya kufuatia maandamano ya vijana wa Gen-Z walioingia mitaani leo na kufunga barabara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Sabasaba yaliyofanyika Julai 7, 2024.

Hata hivyo, Julai 7, 1990, yalifanyika maandamano ya kitaifa katika Uwanja wa Kamukunji Nairobi nchini Kenya, wananchi walikuwa wakidai uchaguzi huru wakati wa utawala wa Rais Daniel Arap Moi. Sasa ni miaka 35 imepita huku Gen Z wakiadhimisha siku hiyo kwa kufanya maandamano hayo.

Gen-Z hao wa Kenya wamekuwa wakiandamana mara kadhaa wakipinga utawala wa Rais William Ruto, wakidai amewasaliti kwa kuwa, hajatimiza ahadi yake ya kuwaletea maisha bora hasa watu wa hali ya chini maarufu kama ‘ma-hustler.’

Katika Jiji la Nairobi, maduka yamefungwa, vijana wameingia mitaani na kufunga barabara katika mitaa mbalimbali kama vile Barabara ya Kamiti, Barabara ya Thika na Roysambu ambako vijana wanatafuta upenyo wa kufika Katikati ya Jiji (CBD).

Walinzi binafsi waliokodiwa kuimarisha ulinzi wameonekana katika mitaa ya Nairobi, wakiwa wamebeba virungu kwa ajili ya kukabiliana na waandamanaji watakaojitokeza mitaani kuandamana au kuharibu mali.

Huko Kisii, polisi walilazimika kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakikabiliana na wahalifu waliokuwa wamebeba mikuki.

Mtu mmoja alichomwa mkuki mkono wa kushoto, na aliwahishwa hospitali.

Eldoret na Kaunti ya Uasin Gishu, nako waandamanaji wamesuka mipango ya kuingia mitaani kuadhimisha Sabasaba. Vijana hao wanataka kuandhimisha miaka 35 ya Sabasaba kwa namna ya tofauti.

Huko Nyeri, Jeshi la Polisi lilipiga mabomu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika katika Mtaa wa Kimathi. Maandamano hayo yamewafanya wafanyabiashara katika Soko la Mudavadi waliokuwa wamefungua maduka yao, kuyafunga.

Maandamano hayo yanayoongozwa Gen-Z yameitikisa nchi katika wiki za hivi karibuni. Tofauti na maadhimisho ya Sabasaba ya miaka iliyopita, maandamano ya mwaka huu yamechochewa kwa kiasi kikubwa na uhamasishaji wa mtandaoni kupitia majukwaa kama X, TikTok na Facebook.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Gilbert Masengeli ameonekana akifanya doria katika eneo la katikati ya Jiji la Nairobi  na kusimama katika moja ya vizuizi vya barabarani vilivyokuwa vikizuia watu kuingia jijini humo.

Katika mahojiano mafupi na NTV, Masengeli amedai kuwa Wakenya hawakuwa wanazuiwa kuingia katikati ya jiji , kauli ambayo inapingana na hali halisi iliyokuwa ikishuhudiwa mitaani.

“Kila mtu anaingia CBD, kila mtu anaenda kazini kama kawaida. Hakuna wasiwasi,” amesema Masengeli.


Hali ilivyo Nairobi

Polisi wameweka kizuizi barabarani eneo la Junction Mall kwenye Barabara ya Ngong, Nairobi, asubuhi ya Julai 7, 2025.

Hakuna gari, pikipiki au mtembea kwa miguu kutoka Barabara ya Ngong aliyeruhusiwa kuelekea jijini, ni magari tu kutoka jijini yaliyokuwa yakiruhusiwa kupita.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Gilbert Masengeli amedai kuwa, kuwepo kwa idadi kubwa ya polisi kulilenga tu kuhakikisha usalama unakuwepo huku Wakenya wakiendelea na shughuli zao za kila siku.

“Hamtafukuzwa. Wajibu wetu ni kuwasihi wote kudumisha amani na kufuata sheria,” amesema.

Moja ya barabara kuu zilizofungwa ni Barabara ya Ngong, hali iliyowazuia Wakenya waliokuwa wakielekea katikati ya jiji. Magari na pikipiki zote kutoka Ngong, Karen, Kawangware na Kabiria zilikuwa zikielekezwa kupita katika eneo la Junction Mall.

Mabasi kutoka maeneo ya mashinani yaliegeshwa nje ya Kituo cha Polisi cha Kabete baada ya polisi kuzuia Barabara ya Waiyaki, Julai 7, 2025.

Idadi kubwa ya polisi, pia imeonekana karibu na makao makuu ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), waandishi wa habari, magari ya wagonjwa na watumishi wa umma pekee ndio waliokuwa wakiruhusiwa kupita kwenye kizuizi hicho.

Barabara ya Waiyaki ilikuwa miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi, huku magari ya huduma ya umma ya masafa marefu yakizuiwa katika eneo la Kangemi. Baadhi ya mabasi na daladala zilizokuwa zikielekea CBD zilielekezwa hadi Kituo cha Polisi cha Kabete.

Asubuhi ya leo Jumatatu, maduka katika mitaa ya Kimathi, Tom Mboya, Kenyatta Avenue, Moi Avenue na Ronald Ngala yalikuwa yamefungwa.

Polisi walifunga mzunguko wa Barabara ya Haile Selassie/Uhuru Highway ili kuwazuia waandamanaji kuingia katikati mwa jiji kabla ya maandamano yaliyopangwa ya Sabasaba leo Julai 7, 2025.

Biashara kadhaa ndani ya CBD ziliimarisha milango yao kwa kuweka vyuma vya ziada ili kulinda bidhaa zao iwapo kutatokea uporaji. Siku moja kabla, baadhi ya wafanyabiashara walionekana wakisafisha maduka yao na kuhamisha bidhaa nyumbani ili kuepuka hasara.

“Ingawa tunatambua na mara nyingi tumekuwa mstari wa mbele katika kampeni na maandamano, ni wazi kwa Wakenya wote kuwa maandamano haya yamepoteza mwelekeo. Kile kilichoanza kama njia ya kuonesha changamoto za utawala sasa kimeporwa na wahalifu na watu wenye nia ovu za kisiasa,” inaeleza taarifa ya wabunge.

Kwa mujibu wa wabunge, kama viongozi waliochaguliwa, wamepewa jukumu la kuleta maendeleo karibu na jamii zote, maendeleo yako hatarini iwapo mwenendo wa sasa wa uharibifu wa mali ya umma na binafsi utaendelea.

“Sisi ni viongozi wa maendeleo, si maandamano. Hatuwezi kama taifa kusimama tu bila kufanya lolote huku tukitazama ushujaa huu wa kipuuzi ukijitokeza. Wiki hii tutaanza kuwataja na kuwaaibisha wote wanaochochea vurugu, uharibifu na machafuko,”inaeleza taarifa hiyo.


Maandamano ya Juni

Juni 17, 2025, maelfu ya Wakenya waliingia mtaani kuandamana ikiwa ni mwendelezo wa maandamano yaliyoanza wiki moja kabla, lakini hayo yalionekana kuwa na sura na picha kubwa kufuatia kifo cha mwanablogu wa Kenya, Albert Ojwang aliyepoteza maisha akiwa mikononi mwa polisi.

Kifo chake kilichotokea akiwa anashikiliwa na maofisa wa polisi kimeendelea kuzua ghadhabu miongoni mwa Wakenya, wengi wakishinikiza waliohusika na mauaji hayo wawajibishwe kisheria.

Japo, kulikuwa na kesi iliyokuwa ikiendelea mahakamani, kuna waliokamatwa na kujiweka kando, kupisha uchunguzi, lakini hiyo haikuwatosha Wakenya, walioingia tena mtaani.

Maandamanao hayo yalijiri siku moja baada ya aliyekuwa Naibu Inspekta wa Polisi, Eliud Lagat kuachia madaraka kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa kifo cha kutatanisha cha Ojwang.

Kupitia taarifa iliyotolewa Juni 16, 2025, Lagat alisema uamuzi wake umechukuliwa kwa fikra pana na dhamira ya dhati kutokana na uzito wa ofisi yake na masilahi ya umma kuhusiana na suala hilo.

Taarifa hiyo ilieleza, “nimeamua kujiweka kando kutoka ofisi ya Naibu Inspekta Jenerali, Huduma ya Polisi Kenya hadi pale uchunguzi utakapokamilika. Majukumu ya ofisi sasa yataendeshwa na naibu wangu hadi uchunguzi utakapoisha.” 

Taarifa hiyo iliongeza: “Niko tayari kutoa usaidizi wowote utakaohitajika wakati wa uchunguzi wa tukio hili la kusikitisha.”

 Wakati uchunguzi ukiendelea, Ofisa Mkuu wa Polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi, Samson Talaam na Konstebo wa Polisi, James Mukhwana tayari wamekamatwa.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA), pia, iliwakamata wafungwa raia watatu, Gin Ammitou Abwao, Collins Karani Ireri na Brian Mwaniki Njue, waliokuwa wakizuiwa katika kituo hicho hicho wakati wakimshikilia Ojwang.