Mwanafunzi auawa katika maandamano Kenya

Waandamanaji nchini Kenya wakikimbia baada ya kurushiwa mabomu ya machozi na polisi.

Muktasari:

  • Mtu mmoja nchini Kenya ameuawa baada ya kupigwa risasi katika maandamano ya upinzani dhidi ya serikali kupinga gharama za maisha jana Jumatatu.

Nairobi. Mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Kenya amefariki, huku maofisa sita wa polisi wakijeruhiwa katika maandamano ya kuipinga Serikali na kupanda kwa gharama za maisha yaliyoongozwa na kiongozi wa vuguvugu la Azimio, Raila Odinga jana Machi 20.

 Waandamanaji waliiteka mitaa ya mji mkuu wa Nairobi na katika baadhi ya miji mingine wakitekeleza agizo la kiongozi huyo wa upinzani.

Baadhi walionekana wakiwasha moto katika mitaa huku wengine wakiwarushia maafisa polisi mawe. Polisi walirusha vitoa machozi na maji ya kuwasha, ikiwa ni pamoja na msafara wa Odinga alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake kutoka kwenye paa la jua la gari lake.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maseno, Magharibi mwa Kenya, alipigwa risasi shingoni na polisi wakati maafisa walipofyatua risasi za moto baada ya kuishiwa na vitoa machozi.

Ripoti ya polisi ilisema maafisa hao walikuwa wakikabiliana na wanafunzi waliochoma moto barabarani na kuharibu biashara za eneo hilo.

Akizungumza mbele ya waandamanaji, Odinga ametaja gharama ya juu ya unga wa mahindi, uliopandisha mfumuko wa bei, kuwa ndiyo sababu ya kuitisha maandamano.

Pia ameendeleza madai yake ya kuporwa ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022, ambao Rais William Ruto alitangazwa kuwa mshindi.

Odinga alipinga matokeo hayo mwaka jana mbele ya Mahakama ya Juu, ambayo iliidhinisha ushindi wa Ruto.

Takriban wabunge wanne walikamatwa wakati wa maandamano hayo na kuachiliwa kwa dhamana na watafikishwa mahakamani siku ya Alhamisi kujibu mashtaka ya mkusanyiko usio halali.