Mtoto auawa kwenye mchezo wa kupigana makofi

Muktasari:

  • Mtoto mmoja kutoka nchini Zambia ameuawa baada ya kupigwa mateke, makofi na marafiki zake. Tovuti ya Zambian Observer imeripoti.

Zambia. Francis Ngosa, mtoto mwenye umri wa miaka 12 kutoka Kijiji cha Katanga wilaya ya Mansa Mkoa wa Luapula nchini Zambia amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa na marafiki zake watatu wakati wakicheza mchezo wa ‘mateke na makofi’.

Ofisa Mkuu wa Polisi wa Mkoa, Fwambo Siame amesema kulingana na shangazi wa marehemu, Mary Kabaso, mtoto huyo aliagizwa kuchota maji saa kumi jioni Alhamisi ya Mei 18, 2023 lakini alirejea nyumbani saa mbili usiku, huku akishindwa kutembea.

Shangazi Kabaso alipomuuliza kwa nini anashindwa kutembea na kwa nini alichukua muda mrefu kufanya kazi ambayo kwa kawaida ilikuwa ndogo, alimjibu kwamba alikuwa akicheza na marafiki zake watatu wanaodaiwa kumpiga.

Inadaiwa usiku huo huo hali ya Ngosa ilibadilika na familia yake iliamua kumkimbiza katika Zahanati ya Luamfumu ambako alifikwa na umauti.

Matokeo ya awali kwenye mwili wa mtoto huyo yalionyesha kuwa marehemu alikuwa akivuja damu mdomoni.

Watoto aliocheza nao mchezo huo wenye umri wa miaka 13, 15 na 16 mtawalia wamekamatwa na kushtakiwa kwa mauaji na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni.