Mjukuu wa Bob Marley afariki dunia

Joseph 'Jo Mersa' Marley
Muktasari:
Mjukuu wa nguli wa muziki wa Regge, Bob Marley, Joseph ‘Jo’ Mersa afariki dunia akiwa na miaka 31.
Dar es Salaam. Tasinia ya muziki duniani na familia ya Marley imepatwa na pigo kubwa hii ni baada ya kuondokewa na mwanafamilia Joseph Marley, ambaye ni mjukuu wa nguli wa muziki wa Reggae, Bob Marley, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 31.
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari za Burudani ‘thirty-mile zone’ TMZ wameeleza kwamba Joseph, anayejulikana katika ulimwengu wa muziki kama Jo Mersa, alifariki siku ya Jumanne Desemba 27, kutokana na matatizo yanayohusiana na pumu ingawa maelezo kuhusu kifo chake hayako wazi.
Inaelezwa Jo Mersa, ambaye ni mtoto wa Stephen Marley aliripotiwa kutoitikia ndani ya gari alipokuwa Marekani, ndipo ilipofahamika amefariki dunia.
Joseph ambaye ni mtoto wa Stephen Marley, alienda Chuo cha Miami Dade na kusomea uhandisi wa sauti baada ya kukaa miaka yake ya mapema huko Jamaica.
Wakati fulani kipindi cha uhai wake, Jo aliambia kituo kimoja cha habari kwamba changamoto pekee aliyokumbana nayo ilikuwa kudumisha viwango vya juu vya jina la Marley.
"Baba yangu ameunda urithi kwa kuweka nyimbo zenye maana, ni jambo ninalopaswa kuliishi,” alisema
Wakati wa Uhai wake Jo, alitoa EP mwaka 2014 iliyoitwa "Comfortable", ambayo ilikuwa na nyimbo kama vile "Rock and Swing" na "Bogus." Pia alitoa wimbo uliovuma, "Burn It Down," mwaka wa 2016 na kisha kuongeza EP ya 2, "Eternal," mwaka jana.
Kifo cha Jo kimeshtua watu wengi nchini Jamaica, baada ya Waziri Mkuu wa Jamaica ku-Tweet katika mtandao wake wa Twitter kuonesha ni jinsi gani amesikitishwa na kifo hicho.
Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness, alishiriki ujumbe wa Twitter akimheshimu Joseph Marley.
"Kifo chake kisichotarajiwa akiwa na umri mdogo wa miaka 31 ni hasara kubwa kwa muziki tunapoangalia kizazi kijacho," Holness aliandika.
Aliongeza: "Kifo chake kisichotarajiwa katika umri mdogo wa 31 ni hasara kubwa kwa muziki tunapoangalia kizazi kijacho.
Familia ya Marley ni miongoni mwa familia maarufu duniani katika tasnia ya muziki kama ilivyo kwa familia ya Jackson’s ile ya kina Michael Jackson.
Bob Marley akiwa kama mwanzilishi wa familia hiyo aliacha alama katika muziki wa Regge ambao ni muziki pendwa huko nchini Jamaica, ambapo enzi za uhai wake alifanya mambo mengi makubwa hadi kuwarithisha watoto na wajukuu, kuingia katika tasnia hiyo ya Regge.