Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kushikiliwa wakili wa Besigye, mawakili wasimamisha shughuli za mahakama

Wakili maarufu na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Erias Lukwago. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Mawakili nchini Uganda wamegoma kwa siku moja kususia shughuli za mahakama wakipinga kukamatwa na kushikiliwa kwa wakili wa Kizza Besigye, Erias Lukwago, wakidai utawala wa sheria na haki za binadamu vinakanyagwa.

Dar es Salaam. Shughuli katika mahakama mbalimbali nchini Uganda jana zilisimama baada ya mawakili kufanya mgomo wa siku moja kupinga kukamatwa na kuendelea kushikiliwa kwa wakili mashuhuri wa upinzani, Erias Lukwago, hatua iliyozua mjadala mpana kuhusu uhuru wa taaluma ya sheria, utawala wa sheria na mustakabali wa demokrasia nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, ikiwamo Deutsche Welle (DW), mgomo huo ulioratibiwa na Chama cha Wanasheria Uganda (Uganda Law Society - ULS) ulifanyika jana Ijumaa, Juni 26, 2026, sambamba na Siku ya Kimataifa ya Kutoa Mshikamano kwa Waathirika wa Mateso.

Mawakili hao wamesema mgomo huo ulilenga kupinga kile wanachokiita ukiukwaji unaoendelea wa haki za binadamu pamoja na kuingiliwa kwa uhuru wa mawakili katika kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma.

Athari za hatua hiyo zimeonekana katika mahakama mbalimbali baada ya mawakili kutofika kazini jana, hali iliyosababisha kucheleweshwa au kusimama kwa usikilizwaji wa mashauri mengi.

Chanzo kikuu cha mgogoro huo kinatajwa kuwa ni kukamatwa kwa Erias Lukwago, mmoja wa mawakili wanaomtetea kiongozi wa upinzani, Dk Kizza Besigye.

Lukwago alikamatwa wiki iliyopita na baadaye kufunguliwa mashtaka ya kutoripoti taarifa zinazodaiwa kuhusiana na uhaini, shtaka ambalo amelikanusha.

Wanasheria nchini Uganda wamesema kukamatwa kwake na uamuzi wa mahakama kumkatalia dhamana licha ya hali yake ya afya kudaiwa kuwa mbaya, vinaashiria kile wanachokieleza kama kupuuzwa kwa misingi ya sheria na haki za msingi za binadamu.

"Visa vya hivi karibuni vya kukamatwa kwa Erias Lukwago na kukataliwa kwake dhamana vinaonyesha wazi kuwa utawala haujali tena sheria zinazolinda taaluma yetu wala haki za binadamu," imesema ULS katika taarifa yake.

Chama hicho kimesema mgomo wa siku moja ni mwanzo wa hatua za shinikizo na kwamba, endapo madai yao hayatashughulikiwa, watachukua hatua zaidi kwa kushirikiana na vyama vingine vya mawakili Afrika Mashariki na barani Afrika.

"Tukikosa kusikilizwa, tutatangaza hatua nyingine kwa ushirikiano na wenzetu wa Afrika Mashariki na Afrika nzima," wamesema ULS.

Rais wa Uganda Law Society, Isaac Ssemakadde amesema kukamatwa kwa wakili kwa sababu ya kutekeleza wajibu wake, ni tishio kwa mfumo mzima wa utoaji haki.

"Hakuna wakili anayepaswa kuogopa kukamatwa kwa sababu ya kumtetea mteja wake. Hili ni suala la kulinda utawala wa sheria," amesema.

Taasisi na vyama mbalimbali vya wanasheria, vikiwemo Commonwealth Lawyers Association, vimesema uhuru wa mawakili ni nguzo muhimu ya haki na demokrasia na unapaswa kulindwa wakati wote.

Wakati huohuo, Serikali ya Uganda kupitia upande wa mashtaka imesisitiza kuwa Lukwago anapitia mchakato wa kawaida wa kisheria na kwamba hatua zilizochukuliwa dhidi yake zinafuata sheria za nchi.

Hata hivyo, msimamo huo umeendelea kupingwa na jumuiya za wanasheria na watetezi wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Kukamatwa kwa Lukwago kunakuja wakati Dk Besigye naye akiendelea kukabiliwa na kesi ya tuhuma za uhaini, hali inayoongeza mvutano wa kisiasa nchini Uganda, huku upinzani ukidai vyombo vya dola vinatumika kukandamiza wapinzani na mawakili wao.

Mgomo huo umeibua mjadala mpana zaidi kutoka suala la kesi ya Besigye na kuhamia katika hoja ya uhuru wa taaluma ya sheria na uwezo wa mawakili kutekeleza majukumu yao bila hofu. Endapo suluhu haitapatikana, mawakili wa Uganda na wenzao wa kikanda wanatarajiwa kuendelea na hatua za shinikizo zaidi katika siku zijazo.