Kumbe Ruto alipunguza uzito baada ya kupata urais!

Muktasari:

  • Miezi michache baada ya kuingia madarakani, Rais William Ruto amekuwa akionekana kama mtu anayedhoofu kiafya kadiri siku zinavyokwenda, jambo linaloibua hisia kwamba huenda “majukumu yanamwelemea.”

Nairobi. Rais wa Kenya, Dk William Ruto amesema hakuna sababu ya wananchi wake kuwa na hofu na kupungua kwake uzito ambako kumedhihirika hivi karibuni kwa baadhi ya Wakenya na kusababisha maneno kwenye mitandao ya kijamii.

 Akizungumza na vyombo vya habari katika Ikulu ya Nairobi Jumapili usiku, Dk Ruto alisema alipunguza uzito baada ya kurejesha programu yake ya ukakamavu wa mwili, lishe na afya njema ambayo ilikumbwa na changamoto wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2022.

Utafutaji wa kura dhidi ya muungano wa Azimio la Umoja ukiongozwa na Raila Odinga na Uhuru Kenyatta, alisema uliathiri mpangilio wake wa ulaji na lishe, wakati mwingine akijikuta anakula kupita kiasi.

“Tuliingia kwenye uchaguzi na unajua unapokuwa kwenye uchaguzi kunakuwa na shinikizo kubwa, wakati mwingine unaondolea shinikizo kwenye chakula,” aliuambia mkutano huo wa pamoja wa vyombo vya habari.

“Lazima ufanye hivi na vile na huna muda wa kwenda kufanya mazoezi, akati mwingine unakula na hujui ni muda gani utapata mlo unaofuata, na wakati mwingine unajikuta umekula kupita kiasi.”

Katika kuwashawishi wapigakura, Ruto na mgombea mwenza wake, Rigathi Gachagua walionekana mara kwa mara wakifurahia chakula na ‘mahustlers’ kwenye migahawa na masoko ya wazi sehemu mbalimbali nchini humo.

Picha mbalimbali zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimwonyesha Ruto wa sasa na yule wa zamani kabla hajawa Rais, akiwa ni mwenye mwonekano tofauti, sasa akiwa amepungua zaidi.

Bila kutoa maelezo ya kina, kiongozi huyo wa Kenya Kwanza alisema kuwa amepoteza kilo kadhaa alipokuwa akijiandaa kukabiliana na changamoto za kuendesha nchi ambayo alisema iliachwa katika hali mbaya na mtangulizi wake, Kenyatta.

“Niliamua kupunguza uzito kwa sababu ‘ile kibarua niko nayo si kidogo’. Unahitaji kuwa macho sana, ili kufanya kazi vizuri zaidi.”