Kanisa Katoliki lakataa mchango wa Ruto, kutumika kisiasa

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi, Philip Anyolo.
Muktasari:
- Askofu Anyolo amesema lazima libaki kuwa chombo huru kisichohusishwa na ushawishi wa kisiasa, ili liweze kuhudumu ipasavyo.
Nairobi. Kanisa Katoliki nchini Kenya limekataa sadaka ya KSh6 milioni (Sh123 milioni) iliyotolewa kwenye ibada ya Jumapili na Rais William Ruto, huku likiwataka viongozi wa kisiasa waende kanisani kupewa chakula cha kiroho na si kutafuta umaarufu.
Pia, limekataa sadaka ya KSh2 milioni (Sh41.2 milioni) iliyotolewa na Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki na Ksh200,000 (Sh4.1 milioni) iliyotolewa na Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja.
Amri ya kurejesha fedha hizo za sadaka ilitolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Nairobi, Philip Anyolo.
Kwa mujibu wa Askofu Anyolo ni kinyume cha kanuni za kanisa hilo kupokea fedha kutoka kwa wanasiasa kwa kuwa wanailinda nyumba ya Mungu kutumiwa na wanasiasa vibaya kwa masilahi ya kisiasa.
Amesema kukataliwa kwa sadaka ya Rais Ruto ni kuzingatia agizo la Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) linalokataza matukio ya kanisa kugeuzwa majukwaa ya kisiasa, huku wanasiasa wakiyatumia kuchangisha sadaka kwa masilahi yao. Wamewataka viongozi hao kufuata maadili ya uongozi.
"Kanisa Katoliki linapinga matumizi ya matukio ya kanisa kama vile kuchangisha fedha na mikusanyiko kuwa majukwaa ya kujitangaza kisiasa. Wanasiasa wanaombwa kujiepusha kugeuza mimbari kuwa jukwaa la porojo za kisiasa, kwani vitendo hivyo vinadhoofisha utakatifu ibada," amesema.
Askofu Anyolo amesema kanisa linatakiwa kukataa michango kutoka kwa wanasiasa, wakihofu michango hiyo inaweza kuhatarisha uhuru wa kanisa.
Amesema viongozi wa kisiasa wanapaswa kujitahidi kufanyia kazi masuala ya msingi yaliyoibuliwa na KCCB, ikiwa ni pamoja na kukomesha ufisadi na kushughulikia ahadi ambazo hazijatekelezwa.
"Kanisa limetakiwa kudumisha uadilifu kwa kukataa michango ambayo inaweza kuhatarisha uhuru wake bila kukusudia au kuwezesha kujitajirisha isivyo haki.
“Viongozi wa kisiasa wanahimizwa kuonyesha uongozi wa kimaadili kwa kushughulikia masuala muhimu yaliyoibuliwa na KCCB, ikiwa ni pamoja na mizozo ya kisiasa, ufisadi, siasa za kujitegemea, masilahi, utamaduni wa uongo, ahadi zisizotekelezwa na vipaumbele visivyofaa," amesema.
Askofu Anyolo amesema kwa kuzingatia Sheria ya Rufaa ya Kuchangisha Fedha za Umma 2024 chini ya kifungu cha 10(2), watu wanaokusudia kukusanya fedha kwa njia ya uchangishaji lazima waombe kibali.
“Kwa hiyo, michango iliyotolewa kwa Kanisa Katoliki la Soweto Jumapili, Novemba 17, inayokiuka maagizo haya na sheria hizi ni pamoja na Gavana wa Nairobi kutoa mchango wa Ksh200,000 (Sh4.1 milioni) kwa kwaya ya Parokia na Baraza la Wamisionari la Parokia (PMC), mchango wa Rais wa Ksh600,000 (Sh12.3 milioni) kwa kwaya na PMC na Ksh2 milioni (Sh41.2 milioni) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya padri.
“Fedha hizi zitarejeshwa kwa wafadhili husika zaidi ya hayo, ahadi ya ziada ya KSh3 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya padri, pamoja na mchango wa basi la parokia kutoka kwa Rais zimekataliwa," amesema Askofu Anyolo kwenye taarifa yake na kuongeza:
“Wanasiasa wanakaribishwa kanisani ili kulishwa chakula cha kiroho, lakini wanashauriwa wafanye hivyo kama waumini wengine. Hii itahakikisha kuwa hawatumii nyadhifa zao kwa manufaa ya kisiasa.”
Askofu Anyolo alikuwa akirejea taarifa iliyotolewa Ijumaa na KCCB, ambayo ilishutumu utawala wa Rais Ruto ikieleza umejaa uongo na unaohusika na maovu mengi kama ufisadi na utekaji.
Pia, walisema utawala huo haujali shida za Wakenya kutokana na kuanzishwa kwa Bima ya Afya ya Jamii, ufisadi na mfumo mpya wa ufadhili wa elimu kwenye vyuo vikuu ambao umewasababishia wanafunzi mateso mengi.
Amesema Dayosisi ya Nairobi inaunga mkono taarifa hiyo, akisisitiza kanisa siku zote linastahili kutoegemea mrengo wowote wa kisiasa, na viongozi hawafai kutumia vibaya majukwaa kanisani kujipigia debe.
Sadaka ya Rais Ruto
Jumapili ya Novemba 17, 2024, Rais Ruto alitoa sadaka ya Ksh2 milioni kwa kanisa hilo kujenga nyumba ya padri na akamuomba kiongozi huyo Jumatatu au Jumanne ya Novemba 18, afuate ofisini kwake fedha nyingine Ksh3 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.
Rais Ruto pia alitoa sadaka ya Ksh600,000 ambazo Ksh300,000 zilikuwa zitumike kununua sare ya kwaya ya watoto na Ksh300,000 nyingine kwa ajili ya kwaya kuu. Rais pia aliahidi kununua basi jipya kwa ajili ya kanisa. Alisema angewarejea Januari, mwakani.
Rais Ruto alihudhuria misa ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la Soweto eneo Bunge la Embakasi Mashariki viungani mwa Jiji la Nairobi.
Alifuatana na Gavana wa Nairobi, Sakaja na Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah.
Naibu Rais, Profesa Kindiki
Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki akiwa Kirinyaga alisema Serikali iko tayari kupokea maoni ya kuikosoa ili kuisadia kujenga Kenya bora, thabiti na salama.
Profesa Kindiki baada ya hotuba alitoa sadaka ya Ksh5 milioni ambazo alisema ni kutoka kwa Rais kisha akatoa Ksh2 milioni kusaidia ujenzi wa kanisa la AIPCA.
“Mnajua mambo ya harambee tulisimamisha kwa sababu wanasiasa walikuwa wakiitumia harambee kufanya mambo yao. Hata hivyo, mambo ya kutoa sadaka hayajafungwa na hakuna sheria inayozuia kwa sababu hiyo ni amri ya Mungu.
“Nimetumwa na sadaka ya Rais ya Ksh5 milioni na wanahabari mwelewe sadaka ndiyo tunatoa hatushiriki harambee. Nami nina sadaka pia hata kama nilikuwa nimebeba ya mkubwa wangu na ninatoa Ksh2 milioni yangu,” alisema.
Naibu Rais alisema yuko tayari kusaidia ujenzi wa makao makuu ya AIPCA akimwambia Askofu Fredrick Wang’ombe kuwa yuko tayari kutuma pesa zaidi iwapo kutakuwa na upungufu wowote.
“Makao haya makuu tunajenga na ninyi. cement (saruji) ikipungua, niambieni. Si M-Pesa, Paybill na nambari ya akaunti iko? Nilizaliwa katika familia ya uchungaji na naelewa mambo ya makanisa,” alisema.
Mchango huo mkubwa kwa siku moja unakuja wakati ambao kuna marufuku ya harambee ambayo ilitolewa na Rais Ruto Julai 5, 2024.