Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kambi ya Chadema inayompambania Mdude yavamiwa yadaiwa kumwagiwa sumu, Zimamoto waingilia

Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya wakipuliza maji kuondoa presha ya harufu inayodaiwa kuwa sumu ambayo imemagwa katika ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa ambapo wafuasi na viongozi wa Chama hicho wameweka kambi kushinikiza kupatikana kwa kada wao Mdude Nyagali aliyedaiwa kutekwa Mei 2 mwaka huu. Picha na Saddam Sadick.

Muktasari:

  • Maelezo ya Zimamoto ni kwamba ingawa harufu iliyotoka kwenye eneo hilo ilikuwa kali na ya kukera, ni Mkemia Mkuu wa Serikali ndiye pekee anayeweza kuthibitisha kama ilikuwa sumu au la, pia endapo watapata madhara waende Ofisi ya Mkemia Mkuu kwa kuwa tayari amechukua sampuli kwa uchunguzi zaidi.

Mbeya. Taharuki na sintofahamu vimetanda katika ofisi za chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Nyasa, kufuatia madai ya kuvamiwa usiku na watu wasiojulikana waliomwaga unga unaodaiwa kuwa sumu.

Kwa sasa, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imechukua sampuli ya unga huo kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini iwapo kweli ni sumu.

Wakati huohuo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika katika eneo la tukio na kufanya usafishaji kutokana na harufu kali iliyokuwa ikisambaa.

Kwa sasa ofisi hiyo ndio inatumika kwa ajili ya kambi ya wafuasi na viongozi wa chama hicho wanaoshinikiza kupatikana kwa kada na mwanaharakati wa Chadema, Mdude Nyagali.

Nyagali anadaiwa kuvamiwa na kupigwa nyumbani kwake mtaa wa Iwambi jijini Mbeya na watu waliojitambulisha kuwa askari polisi tangu Mei 2 mwaka huu ambapo hadi sasa hajapatikana.

Baadhi ya makada wa chama hicho kutoka maeneo tofauti waliamua kuweka kambi tangu Mei 3 mwaka huu, ikiwa ni mkakati wa kupaza sauti kupatikana kwa kada huyo licha ya Jeshi la Polisi kueleza kuendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwa ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa jijini Mbeya kwa ajili ya kambi wakiwa wanapata chakula. Picha na Saddam Sadick.


Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha), Elizabeth Mwakimomo amedai tukio hilo limewashtua sana na wanalaani waliofanya kitendo hicho, ambacho lengo lake ilikuwa ni kuua.

"Tukio limetokea usiku wa kuamkia leo, hawa walihitaji kuua zaidi kwakuwa wanafahamu tuko hapa tukihitaji kumpata mwenzetu Mdude, tunalaani vikali tukio hili ambalo nia yake haikuwa njema," amesema Elizabeth.

Kwa upande wake Katibu wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Grace Shio amesema pamoja na majaribu hayo, lakini bado msimamo wao ni kuendelea kuweka kambi eneo hilo kushinikiza kupatikana kwa mwenzao Mdude.

Amesema kambi hiyo itakuwa endelevu akieleza kuwa saa tisa usiku walisikia vishindo vya watu na baadaye kukuta unga unaodhaniwa sumu iliyomiminwa maeneo hayo ambayo inadaiwa kuwa na athari kwa afya ya binadamu.

"Kinachosikitisha kingine ni ukimya uliotawala kwa Jeshi la Polisi kutoeleza kinachoendelea kwa Mdude kujua yuko wapi, sisi kambi yetu ni endelevu kuhakikisha tunampata mwenzetu.

"Kuna baadhi ya taarifa tunazopata zinazotupa mwanga kutoka kwa wananchi na wafuasi wetu, lakini Polisi kama ambavyo waliahidi, tunashukuru wananchi wanazidi kujitokeza hapa kambini tunashirikiana nao," amesema Grace.

Katibu huyo ameongeza kuwa kwa sasa nyumbani kwa Mdude hapaendeki, kwani familia imeamua kupaacha palivyo kutokana na damu zilizomwagika wakitaka kujua alipo mwanaharakati huyo.

"Baada ya kutokea tukio hilo kwa kuwa hatuna utaalamu wowote tuliamua kuwaita Zimamoto ambao walifika na kusaidia, hivyo tunasubiri kujua madhara ya sumu hii," amedai kiongozi huyo.

Mmoja wa wanachama wa Chadema, Magreth Mwanguku (80) amesema bado hofu ni kubwa kambini hapo, akieleza kuwa hawaelewi hatima ya maisha ya Mdude akibainisha kuwa hawapo eneo hilo kwa furaha bali kupigania uhai wa mwenzao.

"Tunaanza kuishi kwa hofu, kazi ya Polisi hatujui ni nini, hatma ya Mdude bado hatuelewi, watu tupo hapa si kwa ajili ya sherehe, tunaomba kujua hatima ya mwenzetu," amesema Magreth mkazi wa Kata ya Ruanda jijini Mbeya.

Akizungumzia kwa njia ya simu Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Mbeya, Malumbo Ngata amethibitisha kuwapo tukio hilo akieleza kuwa baada ya kupata taarifa walifika eneo hilo na kutoa huduma.

Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya wakipuliza maji kuondoa presha ya harufu inayodaiwa kuwa sumu ambayo imemagwa katika ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa ambapo wafuasi na viongozi wa Chama hicho wameweka kambi kushinikiza kupatikana kwa kada wao Mdude Nyagali aliyedaiwa kutekwa Mei 2 mwaka huu. Picha na Saddam Sadick.

Kuhusu kinachodaiwa kuwa sumu, Kamanda Ngata amesema hana uhakika kwa kuwa majibu hayo ni kwa Mkemia Mkuu wa Serikali akifafanua kuwa wao walifika na kupuliza maji kuondoa presha ya harufu hiyo.

"Kujua kama ilikuwa au haikuwa sumu Mkemia Mkuu ndiye anaweza kuzungumza, lakini ilionekana kuwa na harufu kali na ya kukereketa wakaomba tupulize maji kuondoa presha ya harufu.

"Sisi tumefanya sehemu ya wajibu wetu kusafisha lakini tumeacha ushauri iwapo watapata madhara yoyote wawasiliane na Mamlaka ofisi ya Mkemia Mkuu ambao walifika kuchukua sampuli kujua kama ni sumu au ni kitu gani," amesema Ngata.