Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Israel kufanya mashambulizi ya ardhini Wapalestina 7,000 wakiuawa

Muktasari:

  • Kusini mwa Gaza, Mpalestina aliyefiwa na familia yake, Umm Omar al-Khaldi ameiambia  AFP jinsi alivyoshuhudia majirani zake wakiuawa katika shambulizi la Israel lililosababisha nyumba kuwa kifusi, huku wengi wakihofiwa kufukiwa chini.

Jerusalem. Israel imetuma vifaru, wanajeshi na magari ya kivita katika Ukanda wa Gaza katika “uvamizi uliopangwa” usiku ambao uliharibu maeneo mengi kabla ya kuondoka katika eneo linaloongozwa na Hamas, jeshi lilisema jana.

Moshi mweusi ulitanda angani baada ya mlipuko katika picha za usiku ambazo wanajeshi walitoa saa chache baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kutangaza maandalizi ya vita vya ardhini.

Katika siku ya 20 ya vita kali zaidi vya Israel huko Gaza, ambavyo tayari vimeua maelfu ya watu, jeshi lilisema kuwa vikosi vyake vimeshambulia maeneo mengi ya Wapalestina, miundombinu na vituo vya kurushia makombora ya vifaru.

“Operesheni hiyo kaskazini mwa Gaza iko katika maandalizi ya hatua zinazofuata za mapambano,”, lilisema jeshi katika taarifa yake.

Video hiyo isiyo na rangi ilionyesha msafara wa magari ya kivita yakisogea karibu na uzio wa mpaka wa Gaza. Kanda zingine za video zilionyesha shambulizi la anga na majengo yakipigwa kwa risasi na kusababisha moshi kujaa angani.

Saa chache kabla, Netanyahu alikuwa amewahutubia Waisrael kwenye televisheni ya taifa wakiwa bado wana huzuni na hasira baada ya mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, akiwaambia “tuko katikati ya kampeni ya kuwepo kwetu”.

Shambulizi hilo la kushtukiza, lilishuhudia watu wenye silaha wa Hamas wakimiminika kutoka Gaza hadi Israeli na kuua zaidi ya watu 1,400, wengi wao wakiwa raia, na kuwateka nyara wengine 224, kwa mujibu wa ripoti rasmi.

Israel imelipiza kisasi kwa mashambulizi makali ambayo Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema imeua zaidi ya watu 7,000, wengi wao wakiwa raia, idadi hiyo inayotarajiwa kuongezeka ikiwa wanajeshi wa Israeli watashambulia karibu na Gaza.

Hali hiyo imeongeza hofu kimataifa huku mshtuko ukiongezeka kuhusu ukubwa wa athari za binadamu ndani ya eneo lililozingirwa ambapo Israel imekata huduma ya maji, chakula, mafuta na huduma nyingine muhimu.

Kusini mwa Gaza, Mpalestina aliyefiwa na familia yake, Umm Omar al-Khaldi alisimulia AFP jinsi alivyoshuhudia majirani zake wakiuawa katika shambulizi la Israel lililosababisha nyumba kuwa kifusi, huku wengi wakihofiwa kufukiwa chini.

“Tuliona wakipigwa mabomu, watoto walipigwa bomu wakati mama yao akiwakumbatia,” mwanamke huyo alisema huku akiomba msaada kutoka nje.

“Waarabu wako wapi, ubinadamu uko wapi?” alisema. “Utuhurumie, utuhurumie.”

Idadi ya vifo inayoongezeka katika vita hivyo ni ya juu zaidi tangu Israel ilipojiondoa kwa upande mmoja katika eneo dogo la pwani mwaka 2005, kipindi ambacho kimeshuhudia vita nne hapo awali huko Gaza.

Katika matukio ya ghasia, wafanyakazi wa dharura wa kujitolea na majirani wamepiga kucha, wakati mwingine kwa mikono mitupu, kupitia kuta zilizovunjika na mchanga ili kuwavuta raia walioathirika.

Mara nyingi wao huona maiti ambazo zimerundikana, zikiwa zimefunikwa kwa sanda nyeupe zilizotapakaa damu.

“Hakuna mahali palipo salama huko Gaza,” Lynne Hastings, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu katika maeneo ya Palestina.

Rais wa Marekani, Joe Biden, mshirika mkubwa wa Israel, ameunga mkono wito wa “kuwalinda raia wasio na hatia” na kufuata “sheria za vita” wakati ikiwalenga Hamas.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wenye wanachama 27, walikuwa wakijadiliana jana kuhusu kutoa wito wa kusitishwa kwa vita ili watoe misaada ya kibinadamu inayohitajika sana.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron akizungumza mjini Cairo juzi, alionya kwamba “uingiliaji kati ambao utaweka maisha ya raia hatarini, litakuwa kosa”.

Na mfalme wa Jordan, Abdullah II alisema hasira juu ya mateso inaweza kusababisha mlipuko katika Mashariki ya Kati.

Netanyahu, wakati kukiwa wito wa kuzuia kampeni mbaya ya ulipuaji mabomu, alisema Israel imekuwa ikiwashambulia Hamas na kuua maelfu ya Wapalestina.

Alisema baraza la mawaziri la vita na wanajeshi wataamua wakati wa mashambulizi ya ardhini kwa lengo la kuwaondoa Hamas na kuwarudisha mateka wao nyumbani.

Netanyahu pia alikiri kwa mara ya kwanza kwamba atalazimika kuelezea upungufu wa usalama uliyofichuliwa Oktoba 7.

“Kosa litachunguzwa na kila mmoja atalazimika kutoa majibu nikiwemo mimi,” alisema. “Lakini haya yatafanyika baadaye.”

Biden, pia akitafakari siku zijazo akisisitiza kwamba mgogoro huo utakapomalizika, lazima kuwe na maono ya kile kinachofuata.

Alisema kuwa Marekani inaunga mkono suluhu la mataifa mawili na huru ya Israel na Palestina.

“Inamaanisha juhudi kubwa kwa pande zote, Waisraeli, Wapalestina, washirika wa kikanda, viongozi wa kimataifa, kutuweka kwenye njia kuelekea amani ya kudumu,” alisema Rais wa Marekani.