Ifahamu Hospitali ya Gemelli anayotibiwa Papa Francis

Muonekano wa Hospitali ya Gemelli kwa nje.
Muktasari:
- Hospitali ya Gemelli inatambulika kimataifa kutokana na miundombinu yake ya kisasa na kuwa na idara nyingi za matibabu.
Dar es Salaam. Hospitali ya Gemelli ni moja ya hospitali kubwa na maarufu nchini Italia, iliyo mjini Roma, anayotibiwa Baba Mtakatifu, Papa Francis.
Hospitali hiyo, Policlinico Universitario Agostino Gemelli, ni hospitali ya Kikatoliki, iliyofunguliwa miaka ya 1960.
Ikiwa na vitanda zaidi ya 1,500 vya kulaza wagonjwa, Gemelli ni moja ya hospitali kubwa zaidi za kibinafsi barani Ulaya.

Sehemu ya Hospitali ya Gemelli.
Hospitali hiyo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Cattolica del Sacro Cuore na inajulikana kwa utoaji wa huduma bora za matibabu na utafiti wa kisayansi.
Vilevile, inatambulika kimataifa kutokana na miundombinu yake ya kisasa na wataalamu wa afya wa kiwango cha juu.
Si hayo tu, Gemelli ni maarufu kwa kuwa na idara nyingi za matibabu, ikiwa ni pamoja na upasuaji, tiba ya kansa, na uangalizi wa magonjwa ya moyo, kati ya mengine.
Pia, kuna sehemu ya uangalizi maalumu kwa wagonjwa muhimu na huduma za afya ya akili.
Nje ya hospitali hiyo kuna sanamu kubwa ya Papa Yohane Paulo II, mmoja wa wagonjwa waliotibiwa hosipitalini hapo mara kadhaa kabla ya kifo chake.

Sanamu la Papa John Paul II lililopo nje ya Hospitali ya Gemelli.
Sanamu hiyo inaonyesha Papahuyo akiwa ameinama na kushikilia msalaba, ilikuwa ni katika miaka yake ya mwisho katika utume wake.
Papa Yohane Paulo II alitibiwa hospitalini hapo baada ya kupigwa risasi katika jaribio la mauaji lililoshindwa katika Uwanja wa Mt Peterm Vatican Mei 1981.
Madaktari katika Hospitali ya Gemelli walisaidia kuokoa maisha yake ambapo alifanyiwa upasuaji kwa saa sita kuondoa risasi kutoka kwenye fumbatio lake.
Papa Yohane Paulo II aliipa jina la utani "Vatican Three," na pia St Peter's Square Vatican kuwa Vatican One, na makazi ya papa huko Castel Gandolfo, Vatican Two.
Kitengo cha mapapa
Katika miaka ya 1980, Gemelli alianzisha kitengo maalumu cha Papa, ambacho bado kinatumika hadi leo.

Ni nyumba ndogo iliyopo kwenye gorofa ya 10, ina chumba cha kulala na bafu, kuna sebule na kitanda pamoja na kiti kwa ajili ya wasaidizi wa Papa na kanisa dogo kwa ajili ya ibada, lenye msalaba mkubwa, ambapo Papa anaweza kuhudhuria au kuadhimisha misa na kufanya maombi.
Chumba cha Papa katika hospitali hiyo kimehifadhiwa maalumu kwa ajili ya mapapa, lakini wagonjwa wengine wanatibiwa kwenye gorofa moja nayofuata.
Papa Benedikto XVI, mrithi wa Papa Yohane Paulo II, hakuwahi kulazwa hospitalini wakati wa miaka minane ya utume wake, ingawa alitembelea hospitali hiyo wakati kaka yake alipokuwa akipokea matibabu mwaka 2014.
Papa Francis kutibiwa Gemelli
Miongoni mwa wagonjwa wa sasa wa hospitali hiyo ni Papa Francis (88), ambaye alilazwa Februari 14, 2024 akiwa na maambukizi ya mfumo wa kupumua.
Amegunduliwa kuwa na homa ya mapafu katika mapafu yote mawili na mwishoni mwa wiki amegundulika pia ana tatizo la figo, lililo katika hatua za awali.

Muonekano wa Hospitali ya Gemelli.
Papa Francis amekuwa akitibiwa katika hospitali ya Gemelli mara kadhaa na mwaka 2013, alifanyiwa upasuaji wa utumbo. Mnamo Machi 2023 alitibiwa ugonjwa wa mafua, pia alifanyiwa upasuaji wa utumbo baadaye mwaka huo.
Ugonjwa unaomtesa Papa
Jarida la ‘Everyday Health’ limechapisha taarifa kuhusu maambukizi yanayomtesa kiongozi huyo, kuwa huweza kusababishwa na aina tofauti za bakteria, virusi au vimelea vingine ndani ya mapafu.
Nimonia hutokea pale maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi yanaposababisha kuvimba na kujazana kwa majimaji kwenye mapafu.

Maambukizi hayo yanaweza kuathiri pafu moja au yote mawili kwa wakati mmoja, hali hiyo kitaalamu ndiyo inaitwa ‘bilateral pneumonia’.
Kwa mujibu wa jarida hilo, visababishi vya kawaida vya nimonia ni pamoja na mafua ya msimu, Uviko-19 na ugonjwa wa pneumococcal unaosababishwa na maambukizi ya bakteria aina ya “streptococcus pneumoniae.”
“Dalili za nimonia ni pamoja na upumuaji wa shida, homa, kikohozi kinachotoa makohozi ya manjano, kijani au yenye damu. Kwa watu wazee dalili zinaweza pia kujumuisha mabadiliko ya ghafla ya hali ya akili, kukosa hamu ya kula na uchovu,” limeandika jarida hilo.
Nimonia inavyotibiwa
Profesa mshiriki na Mkurugenzi wa Tiba ya Upumuaji katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Dk Meredith McCormack, anasema: “Antibiotiki au dawa za kuua bacteria ndio matibabu makuu.

Wakati mwingine tunatumia dawa ya kuvuta inhalers au steroids hasa kwa wagonjwa wenye historia ya pumu au magonjwa sugu ya mapafu.”
Kulingana na Chama cha Mapafu cha Marekani, watu wengi wenye nimonia wanaweza kudhibiti dalili kwa kunywa maji mengi, kupumzika vya kutosha na kutumia dawa za kushusha homa na kikohozi.
“Matibabu saidizi ni muhimu,” anasema Dk McCormack huku akiongeza; “Hii inaweza kujumuisha kuwapa wagonjwa oksijeni au hata msaada wa mashine za kupumulia kwa wale walioko kwenye hali mbaya.”
Maendeleo yake
Kiongozi huyo anaendelea kuimarika, lakini madaktari wanasema bado wanahitaji muda zaidi kufuatilia hali yake kabla ya kutoa tathmini kamili ya afya yake.
Taarifa iliyotolewa jana Februari 27, 2025 na Vatican ilieleza kuwa hali ya kiongozi huyo imeendelea kuwa tulivu, huku akiendelea na matibabu ya tiba ya oksijeni kwa kiwango cha juu na mazoezi ya kupumua.
“Kwa kuwa hali yake ni ngumu kitabibu, inahitajika siku zaidi za uangalizi wa karibu ili kubaini maendeleo ya afya yake,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, chanzo cha ndani cha Vatican kimebainisha kuwa dalili za nimonia ya Papa Francis hazijabadilika, lakini hali yake kwa sasa haichukuliwi kuwa ‘mbaya.’
Kwa mujibu wa ratiba, Vatican imefuta mikutano ya hadhara iliyopangwa, ikiwemo Jubilei ya Hadhi iliyotarajiwa kufanyika Machi 1, huku Kardinali Angelo De Donatis akitarajiwa kusimamia ibada ya Jumatano ya Majivu Machi 5, mwaka huu badala ya Papa Francis.
Waumini wa Kanisa Katoliki duniani kote wameendelea kumuombea afya njema kiongozi huyo, huku Kardinali Baldassarre Reina, aliyeteuliwa na Papa kama mlezi wa Dayosisi ya Roma, akiongoza Misa maalum katika Kanisa la San Marcello al Corso kwa ajili ya kuomba afya njema ya Baba Mtakatifu.
Vatican haijatoa tarehe rasmi ya kuruhusiwa kwa Papa Francis kutoka hospitalini, huku wataalamu wa afya wakisisitiza umuhimu wa uangalizi wa karibu ili kuhakikisha hali yake inaimarika ipasavyo.