Hiki hapa alichozungumza Trump baada ya kuapishwa

Rais wa Marekani, Donald Trump
Muktasari:
- Ahadi ya kuwarudisha makwao wahamiaji haramu wote, kuimarisha mipaka ya nchi hiyo hasa ule wa kusini ni miongoni mwa mambo yaliyotawala hotuba ya Rais Trump leo baada ya kuapa.
Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump ameapa rasmi kutumikia Taifa hilo huku akisisitiza masuala ya usalama wa mipaka, kukomesha uhamiaji haramu na kuwarudisha makwao wahamiaji haramu wote.
Trump ameapa leo Jumatatu Januari 20, 2025 katika sherehe rasmi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Capitol, Washington D.C nchini humo.
Rais huyo wa 47 wa Taifa hilo lenye nguvu duniani, amesisitiza kulinda mipaka ya nchi hiyo na kuwarudisha nchini kwao wahamiaji haramu wote, ili kurudisha heshima ya Marekani.
"Kwanza, nitatangaza hali ya dharura ya kitaifa katika mpaka wetu wa kusini…Uingiaji haramu utasitishwa mara moja na tutaanza mchakato wa kuwarudisha mamilioni ya wageni haramu katika maeneo walikotoka,"amesema Trump.
Katika hotuba hiyo iliyoibua mjadala na kukosolewa na baadhi ya wanadiplomasia Trump ameongeza kuwa: “Mipaka yetu imekuwa shimo la kupita kwa wale wasioheshimu sheria zetu. Kuanzia sasa, Marekani inasimama imara dhidi ya wavamizi wa mipaka na wahalifu wa kimataifa."
Katika kukabiliana na usalama kwenye mipaka na wahamiaji haramu nchini humo, Trump amesema atachukua hatua za haraka kama ailivyo katika sera yake ya uchaguzi.
Ameahidi kurudisha sera zilizokuwa zikizuia uhamiaji holela, ameahidi kujenga na kuimarisha ukuta katika mpaka wa kusini, akisema kwamba utaimarisha usalama wa taifa hilo na kuweka vikwazo vipya vya kisheria kwa wale wanaojaribu kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
Katika hotuba hiyo iliyoibua hisia tofauti, Trump amesisitiza kwamba; “Anguko la Marekani limekwisha”
Aidha, amesema moja ya malengo yake makuu ni kuhakikisha Marekani inarejea kuwa taifa lenye nguvu na usalama wa hali ya juu huku akieleza kuwa uhamiaji haramu ni tishio kubwa kwa usalama wa Marekani, uchumi wake na utangamano wa kijamii.
Trump, alishinda urais kwa tiketi ya Chama cha Republican, Novemba 2024 dhidi ya mpinzani wake wa Chama cha Democratic, Kamala Haris na kurejea madarakani baada ya muhula wake wa kwanza wa 2017 hadi 2021.