Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Amnesty: Maandamano ya Gen-Z Kenya yasababisha vifo vya watu 16

Muktasari:

  • Maandamano ya Gen-Z yalikuwa yakiwakumbuka waandamanaji 60 waliouawa Juni 25, 2024, wakati wa maandamano ya kupinga muswada wa fedha

Nairobi. Takriban watu 16 wameuawa na zaidi ya 400 kujeruhiwa kufuatia vurugu zilizozuka katika maandamano yaliyofanyika jana nchini Kenya.

Maandamano hayo yalikuwa yakiwakumbuka waandamanaji 60 waliouawa Juni 25, 2024, wakati wa maandamano ya kupinga muswada wa fedha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Juni 26, 2025, na Shirika la Amnesty International nchini Kenya, baadhi ya waliouawa wanadaiwa kushambuliwa na maofisa wa polisi, huku wengine wakikutwa na majeraha ya risasi.

Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Kenya, Irungu Haughton, amedai Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) imethibitisha vifo vya watu 16 hadi kufikia leo asubuhi.

"Baadhi yao waliuawa kwa kipigo cha polisi," amedai Haughton, akiongeza kuwa miili ya watu watano imekutwa na majeraha ya risasi.

KNCHR imedai kuwa zaidi ya watu 400 wamejeruhiwa katika maandamano hayo, wakiwamo waandamanaji, maofisa wa polisi na waandishi wa habari.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), tume hiyo imedai kuwa inaendelea kukusanya taarifa zaidi kuhusu kiwango cha ukiukwaji wa haki za binadamu kilichotokea wakati wa maandamano hayo.

Juzi, wakati wa maandamano ya kizazi cha Gen-Z nchini Kenya ambayo pia yalihusisha watu wazima, akiwamo Jaji Mkuu mstaafu David Maraga, Mamlaka ya Mawasiliano (CA) iliagiza vituo vyote vya televisheni na redio kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano hayo, hatua iliyozua mjadala mpana kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na haki ya umma kupata taarifa.

Maraga alionekana akishiriki maandamano hayo jijini Nairobi, akiungana na vijana wa Gen-Z kulaani matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayodaiwa kufanywa na polisi dhidi ya waandamanaji.

Uwepo wake uliibua hisia kali na kupeleka ujumbe mzito kuhusu umuhimu wa kulinda haki za raia na misingi ya demokrasia.

Hatua ya mamlaka ya kuzuia matangazo mubashara  ilizua mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata taarifa kwa wakati.

Pia, uamuzi huo ulilalamikiwa na vituo vikubwa binafsi vya televisheni, ikiwamo NTV na KTN, vilieleza kuwa, polisi walivamia vituo vyao na kuzima matangazo, huku Kituo cha Citizen TV kikiripoti kuwa polisi walifika, lakini hawakuzima matangazo.

Katika maandamano ya mwaka jana, waandamanaji walivamia Bunge wakati muswada wa kuongeza kodi ulipopitishwa na kuchoma sehemu ya jengo hilo huku wabunge wakikimbia kuokoa maisha yao.

Miili ya watu ilitapakaa mitaani, huku wahudumu wa afya na mashirika ya uangalizi wa haki wakisema polisi walifyatua risasi moja kwa moja. Jeshi la ulinzi lilipelekwa kudhibiti hali.

Rais William Ruto siku ya Jumatano aliwaomba waandamanaji “wasiiangamize” nchi.

“Hatutakuwa na nchi nyingine ya kukimbilia mambo yakiharibika. Ni jukumu letu kuilinda nchi yetu,” alisema wakati wa shughuli ya mazishi ukanda wa pwani, huku waandamanaji wakielekea Ikulu jijini Nairobi.

Vijana wa Kenya walitumia mitandao ya kijamii kupanga maandamano hayo kwa ajili ya kuwakumbuka waliopoteza maisha mwaka jana. Msemaji wa serikali, Isaac Mwaura, Jumatatu alisisitiza kuwa, hakutakuwa na maandamano yoyote.