‘Yesu’ wa Tongaren kupimwa akili

Muktasari:

  • Baada ya kukamatwa na maafisa wa upelelezi jana Yesu wa Tongareni kupelekwa kupimwa akili.

Kenya. Eliud Wekesa ataendelea kusalia mahabusu kwa siku nne zaidi baada ya mahakama ya Bungoma kuruhusu maafisa wampeleke akapimwe akili. Tovuti ya Taifa Leo ya nchini humo imeeleza.

Wekesa ambaye anatambulika kama ‘Yesu’ wa Tongaren alikamatwa jana na maafisa wa ofisi ya upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI), ikiwa ni operesheni ya kuwasaka wachungaji ‘feki’ nchini humo.

Inaelezwa maafisa wanataka muda wa kwenda kufanya msako nyumbani kwake na katika kanisa lake la New Jerusalem Church.

Jana Alhamisi Wekesa alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Tom Olando aliyemnyima dhamana hivyo akalala rumande na kurudishwa tena mahakamani leo Ijumaa.

“Mahakama inatarajia kwamba mshukiwa atapelekwa hospitalini akapimwe akili, na maafisa wa idara ya upelelezi watafanya msako kwenye kanisa lake na makazi yake katika siku nne hizo,” amesema hakimu Olando.

Maafisa wanataka kujua namna alivyoanza kujiita Yesu. Pia anatuhumiwa kutoa mafundisho ya kupotosha wafuasi wake wakiwemo watoto na utakatishaji wa fedha.

Haya yanajiri baada ya kisa cha Shakahola, ambako makaburi yanafukuliwa kuondoa miili ya watu ambao inadaiwa walifariki baada ya kupotoshwa na mhubiri tata wa kanisa la Good News International, Paul Mackenzie.