Theresia , mjane aliyetengwa kwa imani za kishirikina

Mjane Theresia Hamisi(45) wa Kijiji cha Lwamgasa mkoani Geita akikiandaa chakula ndani ya boma analoishi. Aliyelala ni mtoto wake Majaliwa Stephano, wanayeishi pamoja. Picha na Jackline Masinde
Muktasari:
Anaishi kwa kuokota chakula, mvua, jua vyaishia mwilini mwake
Mkoa wa Geita umekuwa ukikumbwa na matukio mengi ya mauaji ya wazee na wanawake kutokana na imani za ushirikina. Mwaka 2014-2015 wanawake wazee 42 wameuawa mkoani humo kwa tuhuma hizo
Geita. “Igogoo, Igogoo, Igogoo, Igogoo.” Ni kelele za sauti nzito, zilizonishitua baada ya kufika Ofisi ya Serikali, Kata Lwamgasa, Kijiji cha Lwamgasa mkoani Geita nilipofika kikazi na baada ya kuuliza wenyeji kulikoni nikajibiwa kuna mama anayedaiwa mshirikina aliyetengwa na familia yake sasa anaishi jirani na ofisi hiyo na ndipo zinatoka kelele hizo.
Nilishindwa kuvumilia nikaomba niende kushuhudia kinachoendelea na baada ya kufika nilishikwa na mshangao na kujawa huzuni kwa nilichoshuhudia.
Ni boma ambalo halijaezekwa, lilijengwa miaka mitano iliyopita kwa matofali ya kuchoma. Boma hili ni kama limetelekezwa kwani limejaa uchafu wa kila aina. Kwa hali ya kawaida hapafai kuishi binadamu; ni eneo hatari kiafya na kiusalama.
Hata hivyo, humo ndimo anamoishi Theresia Hamisi (45), ambaye ni mjane mwenye mtoto wa kiume, Majaliwa Stephano (20), wote wakazi wa kijiji hicho.
Niliposogea katika boma hilo nilimkuta Majaliwa akiwa utupu, amejaa upele mwili mzima, amelala juu ya kipande cha godoro kilichojaa kunguni huku akiendelea kupiga kelele kwa kutamka neno; “Igogoo.”
Niliposogea zaidi nilibaini Majaliwa hawezi kuongea zaidi ya kupiga kelele.
Wakati nashangaa hali hiyo, mara nikamwona Theresia akija katika boma hilo akiwa amebeba mfuko mweusi ambao ulikuwa na pumba za mchele.
“Dada karibu,” alinikaribisha mama huyo huku akiweka mfuko wake chini. Nilimuuliza mama huyo kwa nini kijana Majaliwa anapiga kelele? Alinijibu kuwa ana njaa, anahitaji kula.
Mazingira ya mama na mwana hao yalinitia huzuni, kwani ndani ya boma hilo kulikuwa na mafiga ya kupikia, vyombo vichache pamoja na vipande viwili vya magodoro vilivyochafuka na kuchafuka kupita kiasi. Bila shaka ndiyo wanayolalia.
Nilitamani kuzungumza na mama huyo kumuuliza kwa nini anaishi katika mazingira hayo, lakini hatukuweza kuelewana. Bahati mbaya kila nilichomuuliza zaidi ya swali kuhusu sababu ya kilio cha Majaliwa, alinijibu tofauti na alionekana kama mwenye upungufu wa akili.
Niliamua kwenda kwa majirani wa eneo hilo ambao walinisimulia historia ya mama huyo na mtoto wake kuishi kwenye nyumba hiyo ambayo haijakamilika.
Baadhi ya watu walitoa maelezo yaliyodai kuwa Theresia alifukuzwa na kutengwa na ukoo pamoja na jamaa zake, hata baadhi ya watoto wake kwa tuhuma za kuwafanyia ushirikina pia kuhusika na kifo cha mume wake aliyetajwa kwa jina la Stephano Charles.
Majirani hao walisema kuwa mama huyo ana muda mrefu tangu alipoanza kuishi kwa kutangatanga yeye na kijana wake Majaliwa ambaye pia anaonekana kuwa na ugonjwa wa akili ambaye ni mtu wa kulala tu kwani hawezi kuongea wala kutembea.
“Kama mnavyomwona huyu mama na mtoto wake, anatia huruma, analala nje. Mvua yake, jua lake, lakini watoto wake wapo na tunaishi nao hapa kijijini. Ana watoto watano tena wakubwa tu na wana uwezo, lakini inaelezwa kuwa walimtenga kisa ni ushirikina,” anasema Wastara Amina, jirani wa mama huyo.
Anastazia Bwagege anasema: “Alikuwa anaishi eneo la uwanjani, kisha akaja kuishi katika ofIsi ya kata; wakamfukuza, ndipo akaanza kuishi kwenye boma hili. Unavyomwona, anaishi kwa kuokoteleza vyakula majalalani, siku nyingine anaenda sokoni kufagia mahindi yanayoanguka na mchele, anakuja kupika.”
Marunde Kija ambaye pia ni jirani wa mama huyo anaeleza: “Maisha ya Theresia ni mabaya, anaishi na mtoto wake ambaye pia ni mgonjwa na hana nguo. Muda wote anapigwa jua, baridi pia ni lake. Watoto wake licha ya kuwa walishakamatwa na polisi, lakini walikataa kabisa kumchukua, wakidai kwa kitendo alichowafanyia hawawezi kuishi naye.”
Kija anasema kuwa haijulikani mama huyo aliwatendea kosa gani watoto wake mpaka wanamwacha akiteseka kiasi hicho na kwamba taarifa walizonazo zinaeleza mama huyu alikuwa akiishi na mume wake na watoto, kisha mumewe alifariki na kudaiwa yeye ndiye aliyehusika kwa kifo hicho.
“Watoto wa mama huyu wapo hapa kijijini, lakini hawamsaidii. Anaishi hapa kwa zaidi ya miaka miwili sasa, kila siku ni adhabu kwake, chakula anaokota, wakati mwingine majirani humsaidia,” anasema.
Anasema kuwa kijana anayeishi naye ni mkubwa, lakini hana nguo muda wote hukaa uchi.
Wananchi wa eneo hilo wanalaani Theresia kutengwa na jamii yake wakiwataka watoto wake kumsaidia badala ya kuwaacha kwenye mazingira magumu.
“Ni vyema ukoo na watoto wakae wajadiliane, kama hawataki kuishi naye basi wamjengee hata nyumba huko,” Neema Majura anashauri.
Hata hivyo, Theresia alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alikanusha kuhusika na ushirikina hata kutengwa na watoto wake, akieleza kuwa mumewe ndiye aliyemtenga.
“Mimi siyo mchawi na watoto wangu hawajanitenga. Walishanifuata wakaniambia wanijengee nyumba, lakini nikakataa kwa sababu nina mume wangu na ninampenda. Nikienda kuishi kwa watoto, mume wangu ataniacha,” anasema mama huyo ambaye alionekana kama amechanganyikiwa.
Anasema mumewe ndiye aliyempeleka kuishi kwenye jengo hilo na kwamba anamsubiri hadi atakaporudi na kumjengea nyumba na haoni shida kuishi maisha hayo, kwani ameridhika nayo.
Mtoto wa Theresia
Hata hivyo, mmoja wa watoto wa Theresia anayeishi kijijini hapo, Majiko Stephano, maarufu kwa jina la ‘White’, alipoulizwa sababu za kumwacha mama yao aishi katika mazingira hatari na kumtenga kwa imani za kishirikina, alikanusha.
“Mama yetu tulishambembeleza sana lakini alikataa. Siyo kweli kwamba tumemtenga kwa imani za kishirikina. Mama mwenyewe amechagua kuishi maisha hayo. Kwa sasa hatuna namna nyingine ya kumsaidia, tumeamua kumwacha aishi hivyo na kijana wake,” anasema Stephano.
Anafafanua kuwa hata mdogo wao Majaliwa anayeishi na mama yao hawezi kuishi na mtu mwingine tofauti na mama yao.
“Kwa hali aliyonayo, mdogo wangu hawezi kuishi na mtu tofauti na mzazi wake ambaye ni mama. Hata ukienda kumchukua yule mama hawezi kukubali,” alisema Stephano.
Stephano alieleza kuwa mama yake ana tatizo la kuchanganyikiwa lililomuanza wakati yeye alipokuwa mdogo na kwamba alikuwa na tabia ya kukimbia watu na hata mdogo wake alizaliwa akiwa hana akili timamu.
“Tulishampeleka kwa waganga lakini hali yake ni ile ile. Hadi hali aliyonayo sasa ndiyo maana tunapata shida hata kumtoa hapo,”anaeleza kijana huyo.
Ofisa Mtendaji
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Lwamgasa, Erasto Majura anakiri kumtambua mama huyo akisisitiza kwamba alitelekezwa na watoto wake kwa imani za kishirikina. “Siku moja nilikwenda ofisini asubuhi, nikamkuta mama huyo akiwa amelala kwenye mlago wa ofisi na mtoto wake ambaye alikuwa akipiga kelele. Nilipofuatilia, nikagundua mama huyo ametengwa na jamii yake na sababu kubwa ni imani za kishirikina,” anasema Majura.
Anaeleza kuwa kwa sasa serikali ya kijiji na kata inafanya taratibu za kuwashawishi ndugu na watoto wa mama huyo ili waondoe dhana ya imani ya kishirikina juu ya Theresia .
Anabainisha kuwa aliwahi kuonana na mtoto wa mama huyo anayemtaja kwa jina moja la ‘White’ lakini baada ya kuelezwa kuhusu mama yao alionekana kuwa mgumu kuelewa huku akidai huo ndiyo msimamo wa ukoo. “Huyu mama hana matatizo ya akili isipokuwa anaonekana ameathirika kisaikolojia kutokana na kifo cha mumewe na kitendo cha kutelekezwa. Kuna kipindi anaongea vizuri na mnaelewana,” anafafanua Majura.
Hata hivyo ni muhimu sasa jamii ikaacha kukumbatia imani za kishirikina na kutoa uamuzi unaweza kuathiri familia na kuziacha hoi kwa umasikini kama Theresia.