Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajasiriamali wapatiwa mafunzo ya kurasimisha biashara

Wajasiriamali na wafanyabishara wa Manispaa ya Geita wakiwa kwenye mafunzo ya umuhimu wa kurasimisha biashara zao.

Muktasari:

  • Mafunzo hayo yanalenga kutoa mwanga kwa wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kuingia kwenye mfumo rasmi wa biashara, ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza mitaji, kupata masoko na kufungua milango ya ushirikiano na taasisi mbalimbali ili kuchangia pato binafsi na la Taifa.

Geita. Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Geita imewataka wafanyabiashara na wajasiriamali kuacha kulalamika kuhusu changamoto za kiuchumi badala yake wachangamkie fursa zilizopo, ikiwemo kurasimisha biashara zao, ili ziweze kuwanufaisha kwa mikopo, masoko na uwekezaji.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Geita, Robert Gabriel wakati wa mafunzo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali yaliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya FinacTax,  ikilenga kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara zao.

Gabriel amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kupitia sera na mifumo rafiki kwa wafanyabiashara, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutumia fursa hizo kwa vitendo.

 “Wafanyabiashara waache kulalamika. Badala yake, wachangamkie fursa kama uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati na kurasimisha biashara zao ili waweze kufaidika na huduma rasmi za kifedha na mitaji,” amesema Gabriel.

Ameongeza kuwa TCCIA itatoa msaada wa kuwaunganisha wafanyabiashara hao na taasisi za umma na binafsi zinazohusika na uwekezaji, biashara na masoko, ili kuhakikisha wanapata huduma wanazohitaji.

Kwa upande wake, Hamis Kashililia, msimamizi wa huduma za kodi, fedha na biashara wa FinacTax, amesema taasisi hiyo imeteuliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kusaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Geita, Robert Gabriel akizungunzia fursa za kiuchumi na umuhimu wa wajasiriamali kurasimisha biashara zao.

Amebainisha kuwa moja ya malengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha wajasiriamali kurasimisha biashara zao kwa mujibu wa sheria.

“Licha ya kuwa na Watanzania zaidi ya milioni 60, waliorasimisha biashara zao hawazidi milioni tatu, hii ina maana kuwa idadi kubwa wanaendesha biashara kwa njia isiyo rasmi, jambo linalowanyima fursa ya mikopo, bima ya biashara, mafunzo ya kitaalamu na hata masoko ya uhakika,” amesema Kashililia.

Amesema wajasiriamali wakirasimisha biashara wanakuwa na uwezo wa kupata mikopo kutoka halmashauri kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani, ambayo hugawanywa kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, lakini wengi wanakosa mikopo hiyo kutokana na kutotimiza masharti.

Akitolea mfano, “amesema kikundi kisichosajiliwa hakiwezi kupewa mkopo, lakini baadhi ya watu wanahofia kuwa usajili unahitaji gharama kubwa, jambo ambalo si kweli. Tunahitaji kuwaelimisha kuwa gharama za kurasimisha ni ndogo ukilinganisha na faida ambazo mfanyabiashara anazipata baadaye,” amesema.

Baada ya kupata mafunzi hayo, Ikorongo Emanuel, mjasiriamali kutoka Manispaa ya Geita amesema wengi wao wanashindwa kurasimisha biashara kwa sababu ya uelewa mdogo na hofu ya kulipa kodi kubwa.

 “Tunadhani kurasimisha biashara ni mzigo mkubwa, kumbe ni njia ya kutufungulia fursa nyingi,” amesema.

Mjasiriamali mwingine wa wa biashara ndogondogo, Mariam Sharif amesema  mafunzo waliyoyapata yametoa mwanga mpya kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuingia kwenye mfumo rasmi na kuwa maisha yao yatabadilika pale watakapokubali kuiheshimu pesa na kurasimisha biashara zao.

Amesema hiyo ni hatua muhimu ya kukuza mitaji na kufungua milango ya ushirikiano na taasisi mbalimbali zilizopo mkoani humo.