Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahimizwa kutumia fursa za mikopo

Wafanyabiashara ya matikiti maji wakisubiri wateja katika Barabara ya Nane, Ngamiani mjini Tanga. Walikuwa wakiuza matunda hayo kati ya Sh3,000 na 5,000. Picha na Salim Mohammed     

Muktasari:

Ni wajasiriamali wa Tanga, watakiwa kukuza biashara zao na kutafuta masoko ya EAC.

Tanga. Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Chumbageni Halmashauri ya Jiji la Tanga, Saida Gaddafi (CCM), amewataka wajasiriamali wanawake kuzitumia fursa za mikopo katika taasisi za fedha zikiwamo benki ili kukuza biashara zao na kuingia katika masoko ya ushindani likiwamo la Afrika Mashariki.

Akizungumza katika kongamano la wanawake wa kata hiyo jana, Gaddafi alisema wajasiriamali wengi wanashindwa kuziendeleza biashara zao na kuishia njiani baada ya kutojua masoko yalipo.

Alisema tangu kuanzishwa kwa soko la pamoja la Afrika Mashariki, wajasiriamali wengi wameshindwa kulitumia vyema kutokana na bidhaa zao kuwa chini ya viwango sambamba na kutojua masoko ya bidhaa hizo yalipo.

“Sisi ambao tuko mpakani na nchi jirani tuna nafasi kubwa ya kutangaza kazi zetu... tatizo ni kwamba hatujawa na utayari na ndiyo maana kazi zetu haziendelei na kuwa na ubora,” alisema Gaddafi.

Aliongeza: “Hebu kwa pamoja tujifunge vibwebwe na kuwa na utayari wa kuzitumia fursa za mikopo katika taasisi za fedha ili kazi zetu tuzifanye katika ubora na kuyafikia masoko ya nje.”

Aliwataka kuunda vikundi ili kuweza kutambulika na kuweza kupata fursa za mikopo katika taasisi za fedha, lengo likiwa ni kujikwamua katika maisha na kuendeleza kazi za mikono yao.

Mjasiriamali anayetengeneza mikoba ya ukili na majamvi, Debora Daffa alisema katika kazi zao, wamekuwa wakikabiliana vikwazo mbalimbali vikiwamo vya kutokuwa na katiba ya kikundi na hivyo kuyataka mashirika na taasisi kuwasaidia.

Alisema tatizo hilo limekuwa kikwazo katika kazi zao na hivyo kuyataka mashirika na taasisi kusaidia ili kuweza kuleta umoja na kupiga hatua katika maendeleo.

“Ili kufanya kazi kwa weledi ni muhimu kuwa na katiba yetu ambayo itatuongoza,” alisema Daffa.

Aliwataka wajasiriamali hao kuwa wabunifu kati utengenezaji wa kazi za mikono na kuyafikia masoko ili kuweza kuleta ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi ikiwa ni hatua ya kujitangaza.