Wafanyabiashara wapya kupata msamaha wa kodi mwaka mzima
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akizungumza wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27bungeni jijini Dodoma.
Muktasari:
- Serikali inapendekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani badala ya asilimia 10 ili asilimia tano itumike kwa ajili ya uwekezaji wa miradi, ujenzi na maboresho ya masoko na maeneo ya ujenzi, biashara na masoko.
Dar es Salaam. Serikali inapendekeza kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wapya kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe ya kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN).
Pendekezo kama hilo lilishatolewa na Tume ya Rais ya Kutathmini Mifumo ya Kodi, iliyotaka mfanyabiashara mpya asitozwe kodi ya mapato kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Utaratibu wa sasa unamtoza kodi mfanyabiashara pale tu atakapofungua biashara na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi.
Hata hivyo, utekelezwaji wa pendekezo hilo utategemea ridhaa ya wabunge baada ya kulijadili na kulipitisha.
Pendekezo la Serikali limewasilishwa bungeni jijini Dodoma leo, Alhamisi Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipowasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambayo ni Sh62.3 trilioni.
Katika hotuba, waziri amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia urasimishaji wa sekta isiyo rasmi inayoajiri zaidi vijana na wanawake.
“Hatua nyingine ni kufanya maboresho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 ili kuwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani badala ya asilimia 10 ya mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu,” amesema.
Balozi Omar amesema kati ya asilimia 15 zitakazotengwa asilimia 10 zitaendelea kuelekezwa kwenye makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, huku asilimia tano ikitumika kwa ajili ya uwekezaji wa miradi, ujenzi na maboresho ya masoko na maeneo ya ujenzi, biashara na masoko.
“Hii itavutia na kuongeza fursa za ajira kwa vijana, wanawake na makundi maalumu,” amesema.