Wadau 500 wa uwekezaji kukutana Zanzibar kujadili uchumi wa buluu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff (Katikati) akizungumza na wanahabari kuhusu tamasha la uwekezaji.
Muktasari:
- Wadau hao wanajumuisha wafanyabiashara wakubwa, watunga sera, washirika wa maendeleo, Watanzania waishio diaspora pamoja na wawekezaji wa kitaifa na kimataifa, wakilenga kujadili na kuibua fursa mpya za uwekezaji
Dar es Salaam. Zaidi ya wadau 500 wa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika msimu wa pili wa Tamasha la Uwekezaji Zanzibar, litakalofanyika kuanzia Juni 3 hadi Juni 5, 2026 visiwani Zanzibar.
Wadau hao wanajumuisha wafanyabiashara wakubwa, watunga sera, washirika wa maendeleo, Watanzania waishio nje (Diaspora) pamoja na wawekezaji wa kitaifa na kimataifa, wakilenga kujadili na kuibua fursa mpya za uwekezaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Aprili 27, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema tamasha hilo linalenga kupanua wigo wa uwekezaji Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Amefafanua kuwa tamasha hilo limejikita katika kukuza sekta mbalimbali muhimu za uchumi, zikiwamo uchumi wa buluu, afya, usafiri wa anga, uzalishaji wa viwandani, usafirishaji wa baharini, utalii wa hadhi ya juu pamoja na maendeleo ya nyumba za biashara.
Aidha, Shariff amesema tamasha hilo litafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi jambo linaloashiria dhamira thabiti ya Serikali ya kuendeleza uchumi unaoongozwa na sekta binafsi pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika uwekezaji.
Shariff amesema kupitia tamasha hilo, Serikali imetayarisha miradi ambayo itatoa fursa kwa wawekezaji binafsi kushirikiana na Serikali katika maendeleo ya nchi ili kuhakikisha uwekezaji huo unakuwa na tija za ajira na vipato kwa Watanzania.
“Tamasha hili la uwekezaji la mwaka 2026, litajumuisha shughuli mbalimbali zikiwamo, ziara za kutembelea maeneo ya uwekezaji, maonesho ya uwekezaji, majadiliano ya kiwango cha juu,”
“Pia, madarasa maalumu ya uwekezaji na biashara, mkutano maalumu wa Diaspora, mikutano ya ana kwa ana ya biashara na hafla ya chakula ya kuwatambua wawekezaji bora,” amesema Shariff.
Katika mkutano huo, Shariff amegusia uamuzi wa Zanzibar wa kuingia katika mradi wa ‘Zanzibar Airlines’ kwa ushirikiano na sekta binafsi, ili kuhakikisha watalii wanasafiri moja kwa moja hadi visiwani humo au Tanzania Bara.
“Sasa hivi watalii wanaokuja lazima waunganishe ndege aidha wapitie Dubai, Qatar, Addis Ababa au nyingine, kwa watalii hii ni kero. Watalii wanapenda safari za moja kwa moja na si kutua sehemu,” amesema na kuongeza kuwa:
“Ametokea mwekezaji ambaye tuna mazungumzo naye ili kushirikiana kutengeneza huo mradi utakaoitwa ‘Zanzibar Airlines’. Tupo katika mazungumzo na si lazima mwekezaji mmoja wanaweza kujitokeza wengine,” ameeleza Shariff.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema baada ya tamasha la mwaka jana, katika miradi 135 yenye thamani ya zaidi ya Dola 750 milioni za Marekani, miradi ya dola milioni 430 ilisajiliwa Pemba.
“Hii inafanya zaidi ya asilimia 55 ya thamani ya miradi iliyosajiliwa katika kipindi cha mwaka 2025 inakwenda kutekelezwa Pemba. Hii faida kubwa iliyopatikana katika tamasha la mwanzo,” amesema Mohamed.