Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tumbaku yaipeleka Chunya kwenye lengo la Sh16.4 bilioni

Muktasari:

  • Mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka kutoka zaidi ya Sh10 bilioni mwaka wa fedha 2025/26 hadi Sh16.4 bilioni mwaka 2026/27, yakichochewa na ukuaji wa sekta za kilimo na madini pamoja na kuimarika kwa usimamizi wa mapato.

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imeweka lengo la kukusanya Sh16.4 bilioni za mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh6 bilioni ikilinganishwa na zaidi ya Sh10 bilioni zilizokusanywa mwaka 2025/26.

Ongezeko hilo linatarajiwa kuchangiwa na kuimarika kwa sekta za kilimo na madini, pamoja na hatua za kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Julai 15, 2026, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Athuman Bamba amesema kilimo cha tumbaku kinaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya ndani, kikifuatiwa na sekta ya madini.

Amesema kwa wastani zao hilo huchangia zaidi ya Sh5 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Licha ya Chunya kuwa na sekta ya madini, kilimo cha tumbaku ndicho kinachochangia kwa kiwango kikubwa mapato ya ndani ya halmashauri," amesema Bamba.

Amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato tangu mwaka wa fedha 2020/21, ambapo halmashauri ilikusanya Sh3.1 bilioni pekee.

Kwa mujibu wa Bamba, maboresho ya mifumo ya ukusanyaji mapato na usimamizi wa vyanzo mbalimbali yameiwezesha halmashauri hiyo kuongeza makusanyo na kuvuka malengo yaliyowekwa na Serikali.

"Miaka ya 2020 hadi 2021 ukusanyaji wa mapato haukuwa wa kuridhisha, lakini sasa tumeshuhudia ongezeko kubwa la mapato na tumekuwa tukivuka malengo ya Serikali," amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Athuman Bamba, akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake leo, Jumatano Julai 15, 2026. Picha na Hawa Mathias.

Amesema sehemu kubwa ya mapato hayo imekuwa ikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan sekta za elimu na afya, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kuchonga barabara.

Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kupitia mapato ya ndani ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa kituo kikuu cha kisasa cha mabasi chenye uwezo wa kuhudumia mabasi 1,000 kwa siku.

Miradi mingine ni uboreshaji wa miundombinu ya afya na ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kukidhi ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari.

Katika sekta ya kilimo, Bamba amesema halmashauri imejipanga kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa, mbegu bora na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati.

Amesema mazao yanayopewa kipaumbele ni pamoja na tumbaku, ufuta na alizeti, sambamba na kuimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala ili kuongeza tija na mapato kwa wakulima.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa halmashauri hiyo, Gideon Mapunda amesema tumbaku inaendelea kuwa zao muhimu katika uchumi wa Chunya.

Amesema zaidi ya wakulima 156,427 wanajihusisha na kilimo cha tumbaku, huku takribani asilimia 90 ya wakazi wa Tarafa ya Kipembawe wakitegemea zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato.

Mapunda amesema tumbaku hulimwa katika eneo la takribani hekta 22,000, huku uzalishaji ukitarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya kilo milioni 30.9 katika msimu huu kutoka kilo milioni 28 za msimu uliopita.

Ameeleza kuwa uzalishaji wa tumbaku umechangia zaidi ya Sh68 bilioni katika uchumi wa wakulima wa Chunya, huku halmashauri ikiendelea kukusanya zaidi ya Sh5 bilioni za ushuru kutokana na zao hilo kila mwaka.

Kuhusu mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), Mapunda amesema halmashauri imetenga zaidi ya ekari 10,000 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kati ya eneo hilo, ekari 600 tayari zimetengwa katika vijiji viwili, ikiwemo Lualaje, ambako mkandarasi ameshaanza kazi za maandalizi ya kusafisha eneo la mradi.

Kwa upande wa wakulima, Josia Joan kutoka Kata ya Lupa amesema msimu huu wameongeza uzalishaji kutokana na upatikanaji wa pembejeo na mikopo kwa wakati.

"Serikali imeboresha mazingira ya uzalishaji kupitia pembejeo na mikopo. Hilo limetupa ari ya kuongeza uzalishaji na kupata mavuno bora zaidi," amesema.

Hata hivyo, ameiomba Serikali kuendelea kupanua wigo wa ushindani kwa kampuni zinazonunua tumbaku ili kuwawezesha wakulima kupata manufaa zaidi kutokana na uzalishaji wao kupitia bei elekezi.