Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trump kuongeza ushuru asilimia 25 magari kutoka Ulaya

Rais wa Marekani, Donald Trump akisalimiana na Rais wa EU, Ursula Gertrud von der Leyen. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Hatua ya Trump itajwa kuongeza hofu ambavyo inaweza kuathiri masoko ya kimataifa na mnyororo wa usambazaji wa bidhaa duniani.

Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuongeza ushuru wa magari na malori yanayoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya (EU) hadi asilimia 25, hatua inayotajwa kuongeza mvutano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump aliishutumu EU kwa kile alichodai kushindwa kutekeleza kikamilifu makubaliano ya biashara yaliyokuwa yamefikiwa hapo awali, bila kutoa maelezo ya kina kuhusu madai hayo.

“Nimefurahi kutangaza kwamba… Wiki ijayo nitaongeza ushuru unaotozwa Umoja wa Ulaya kwa magari na malori,” aliandika Trump jana Ijumaa Mei 1, 2026.

Hatua hiyo imekuja huku sekta ya magari ikiwa mhimili muhimu wa uchumi wa Ulaya, jambo linaloifanya EU kuona uamuzi huo kama pigo kubwa kwa viwanda vyake.

Kwa upande wake, Tume ya Ulaya imesema itaendelea kuweka chaguo zote mezani ili kulinda maslahi ya bloc hiyo, ikisisitiza kuwa EU inaendelea kutekeleza wajibu wake chini ya makubaliano ya biashara, huku ikitaka ufafanuzi zaidi kutoka Marekani kuhusu hatua zake.

Uamuzi huo unakuja chini ya mwaka mmoja tangu Marekani na EU kufikia makubaliano katika uwanja wa gofu wa Turnberry, Scotland, yaliyosaidia kupunguza ushuru wa bidhaa nyingi za Ulaya hadi asilimia 15.

Makubaliano hayo yaliipa EU ahueni baada ya Trump awali kutishia kuweka ushuru wa hadi asilimia 30 katika kile alichokiita ‘Siku ya Ukombozi,’ mpango uliolenga kulinda viwanda vya Marekani dhidi ya ushindani wa kimataifa.

Katika miaka ya nyuma, Trump amekuwa akitoa vitisho kadhaa vya ushuru mkali dhidi ya washirika wa Marekani, ikiwemo kutishia kutoza ushuru mkubwa magari kutoka Ulaya, bidhaa za teknolojia kutoka Asia pamoja na bidhaa za chuma na alumini.

Hatua hizo zilikuwa sehemu ya sera yake ya ‘America First’ iliyolenga kupunguza nakisi ya biashara ya Marekani.

Hata hivyo, alipoulizwa ni kwa namna gani EU imekiuka makubaliano ya sasa, Trump hakutoa maelezo ya kina zaidi, akisema; “Tuna makubaliano ya biashara na Umoja wa Ulaya. Hawakuyazingatia ipasavyo, ndiyo maana nimeongeza ushuru kwa magari na malori.”