Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Thamani Soko la Hisa yapaa, lavutia wawekezaji

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20, katika ofisi mpya za DSE zilizopo Morocco Square jijini Dar es Salaam. Picha na Sute Kamwelwe.

Muktasari:

  • Thamani ya Soko la ndani iliongezeka kwa asilimia 7.4, na kufikia Sh12.24 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh11.4 trilioni mwaka 2023. 

Dar es Salaam. Thamani na shughuli za biashara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka kwa mwaka 2024 licha ya changamoto zinazogusa soko hilo zilizojitokeza.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, thamani ya mtaji wa soko la ndani uliongezeka kwa asilimia 7.3 na kufikia Sh12.2 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh11.4 trilioni mwaka 2023.

"Kwa ujumla wake ukichukua soko la ndani na nje kampuni za ndani na nje jumla ya thamani ya mtaji ilitoka Sh14.6 mwaka 2023 hadi kufikia Sh17.8 trilioni ikiwa ni ukuaji wa asilimia 22.2," amesema.

"Maana make kama thamani ya mtaji inaongezeka na utajrii wa wawekezaji pia unaongezeka. Kama ulinunua hisa kwa Sh100 na ikaongezeka hadi Sh120 basi thamani ya uwekezaji wako inakuwa imeongezeka," amesema. 

Amesema jumla ya hisa milioni 228 ziliuzwa mwaka 2024 ambapo zilipanda kwa asilimia 21.28 kutoka hisa milioni 188 mwaka 2023.

Aidha, amesema ukwasi wa soko ambao ni uwezo wa kupata hisa pale mwekezaji anapohitaji pamoja na miamala kufanyika kwa haraka umeongezeka na ulifikia kiasi cha Sh228 bilioni mwaka 2024 kutoka Sh225 bilioni mwaka 2023. 

Kuhusu kilichochangia mafanikio ya soko la hisa, Nalitolela amesema ni juhudi za kutoa elimu pamoja na uhamasishaji wa uwekezaji kupitia simu ya mkononi DSE Hisa Kiganjani. 

"Kutokana na kutangaza soko wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wameongezeka jambo ambalo limechangia kuendelea kwa soko letu," amesema Nalitolela. 

Aidha pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwa upande wa hisa mauzo ya hatifungani amesema ulishuka kwani mwaka 2024 ziliuzwa Sh3.15 trilioni kutoka Sh3.64 trilioni mwaka 2023. 

Amesema kilicho sababisha kushuka kilichangiwa na mpango wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kubadilisha uendeshaji wa Hatifungani katika soko ambapo ilichangia kupungua kwa ukwasi.

"Kuanzia mwaka huu Benki kuu ya Tanzania (BoT), imebadilisha mfumo wa uuzaji ambao utachangia kupelekea mafanikio katika soko la awali na upili ambalo ndilo DSE," amesema.

Amesema pia fahirisi ya Hisa Tanzania (TSI) ilipanda kwa asilimia 7.3, na kufikia pointi 4,618.78 kutoka pointi 4,304.4 mwaka 2023.

Nalitolela amesema hiyo imechangiwa na kupanda kwa thamani za baadhi ya kampuni kubwa za ndani kama vile Benki ya CRDB, Benki ya NMB, Swissport, Tanga Cement, DCB na DSE yenyewe.  

Soko la ujumla la Fahirisi ya Hisa Zote (DSEI) kampuni za ndani na nje ilishuhudia ukuaji mkubwa zaidi, ukipanda kwa asilimia 22.22 hadi pointi 2,139.73 kutoka pointi 1,750.63.

Nalitolela amesifu ukuaji huo kwa njia bora za biashara ikiwemo za simu za mkononi, kuongezeka kwa ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, na utendaji mzuri wa kampuni zilizoorodheshwa.