Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Teknolojia za kisasa uchenjuaji dhahabu Chunya mkombozi wachimbaji wadogo

Meneja wa Kampuni ya Kindai, Khadija Ramadhan, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchango wa kampuni hiyo kwa wachimbaji wadogo wa madini, hususan katika utoaji wa elimu na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, yameelezwa kuwa mkombozi kwa wachimbaji wadogo kutokana na kuondoa matumizi ya kemikali hatarishi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ajira pamoja na kipato.

Mbeya. Matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu wilayani Chunya,  yametajwa kuleta mageuzi makubwa kwa wachimbaji  kuondokana na dhana ya matumizi ya kemikali hatarishi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ubora wa madini yanayouzwa sokoni.

Imelezwa teknolojia hizo zimepunguza adha ya kusafirisha madini kwenda mkoani Geita kwa ajili ya hatua mbalimbali za uchenjuaji na uongezaji thamani.

Mabadiliko hayo yamechangiwa na hatua ya Serikali kufungua fursa za uwekezaji wa viwanda vya kisasa vya uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini ya dhahabu, hatua inayolenga kuongeza tija katika sekta ya madini na kuinua uchumi wa wananchi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 24, 2026, baadhi ya wachimbaji wadogo wamesema uwekezaji huo umeleta mapinduzi katika shughuli za uchimbaji, huku ukichangia kuongezeka kwa ajira kwa vijana.

Mchimbaji mdogo wa madini kutoka Kijiji cha Itumbi, Kata ya Matundasi, Lestar Ndomba amesema teknolojia hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji ambao kwa miaka mingi walitegemea mbinu za kienyeji na matumizi ya kemikali hatarishi.

"Sisi wachimbaji wadogo tumekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya madini, lakini kwa muda mrefu tulilazimika kutumia kemikali hatarishi katika uchenjuaji wa dhahabu. Hali hiyo ilikuwa ikiweka maisha yetu na afya zetu katika hatari kubwa," amesema.

Ndomba amesema uwekezaji wa kiwanda kinachotumia teknolojia za kisasa katika eneo la Makongoro umekuwa na tija kubwa kwao katika kuchangia fursa ya ajira, kiuchumi na maendeleo katika jamii inayo wazunguka.

"Miaka ya nyuma tulilazimika kusafirisha madini au mabaki ya mchanga wenye dhahabu hadi Geita kwa ajili ya marudio, jambo lililo tugharimu muda na fedha nyingi. Sasa huduma hizo zinapatikana karibu nasi kwa gharama nafuu," amesema.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hizo zimeongeza uhakika wa kupata dhahabu yenye ubora na kuwapa nafasi ya kuuza  kwa bei na thamani stahiki sokoni.

Naye mchimbaji eneo la Chokaa, Sekela Mwakyusa, amesema kwa sasa wachimbaji wengi wameachana na matumizi ya kemikali za hatarishi kukamatisha dhahabu na badala yake wanatumia huduma za viwanda vya kisasa vilivyopo wilayani humo.

Amesema uwepo wa viwanda vinavyotumia teknolojia za kisasa za uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini umeondoa utegemezi wa mbinu za zamani zilizo kuwa na athari kwa afya na mazingira.

"Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuvutia fursa za  uwekezaji viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani wa madini. Zamani tulilazimika kwenda Geita kupata huduma hizi, lakini sasa zinapatikana karibu nasi," amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha Kindai kilichopo Kata ya Makongorosi, Khadija Ramadhan, amesema uwekezaji huo umekuwa mkombozi kwa wachimbaji wadogo na umechangia kuimarisha ufanisi katika sekta ya madini.

Amesema matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchenjuaji wa dhahabu yamechangia kuondoa matumizi ya kemikali hatarishi, kuongeza ubora wa madini na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wachimbaji.

"Tunaendelea kutoa elimu kwa  wachimbaji kwa kuwajengewa uwezo wa mbinu mbalimbali za uzalishaji madini yenye tija katika soko la ndani na nje ya nchi ili kutangaza dhahabu inayozalishwa wilayani Chunya," amesema.

Amesema  mazingira rafiki yaliyowekwa na Serikali yameleta tija kubwa kunufaisha wachimbaji wadogo na kuchangia kuongezeka kwa mapato  kupitia sekta ya madini.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona amesema matumizi ya teknolojia za kisasa yameleta mageuzi makubwa katika sekta ya madini kwa kuongeza ubora wa dhahabu inayo zalishwa na kuuzwa sokoni.

"Tutaendelea kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao, ikiwemo upatikanaji wa huduma karibu na maeneo yao pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri," amesema.

Kambona amesema halmashauri itaendelea kushirikiana na  wadau wa sekta ya madini ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika zaidi na rasilimali za madini na kuchangia maendeleo ya uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.