Tanzania, Sweden zatia saini mkataba wa tafiti za mabadiliko ya tabianchi

Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu (kushoto) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania , Charlotta Macias wakisaini mkataba.
Dar es Salaam. Serikali ya Sweden na Tanzania zimeingia mkataba wa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2029, lengo likiwa ni kuimarisha tafiti za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha mifumo ya ubunifu na mawasiliano ya sayansi katika vyuo vikuu na kuimarisha mawasiliano ya kisayansi.
Kwenye mkataba huo, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) itapokea Sh10 bilioni, ambapo Sh8.2 bilioni zitaingia nchini Tanzania, huku fedha zilizobaki zikielekezwa kwa washirika wa Sweden, watakaoshirikiana katika kutoa mafunzo kuhusu utafiti, ubunifu na mawasiliano.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo leo, Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu amesema mazingira wezeshi waliyowekwa na Serikali yamechangia wadau wa maendeleo kuendelea kuamini taasisi hiyo na kuwapatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi.
Dk Nungu amesema hii ni mara ya nne kwa Costech na Sweden kusaini mkataba wa aina hiyo, ambapo katika kipindi chote cha ushirikiano, zaidi ya miradi 53 ya utafiti na ubunifu imefadhiliwa katika maeneo mbalimbali kama viwanda, bioteknolojia, uvuvi, kilimo, teknolojia ya habari na mawasiliano, maji, ufugaji na afya.
Amesema kuwa, kupitia ushirikiano na Sweden, Costech ilifanikiwa kupata fedha kutoka Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) na kufadhili tafiti 40 za mabadiliko ya tabianchi.
Dk Nungu amesema kuwa katika Kongamano la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STiCE) la mwaka 2024, Costech ilitoa Sh6.3 bilioni kwa watafiti 19 wa mabadiliko ya tabianchi, na watafiti 21 waliobaki watapatiwa fedha ili kukamilisha tafiti zao.
Pia, Dk Nungu amesisitiza kuwa Tanzania inajivunia mifumo bora ya utafiti ambayo imejifunza kutoka Sweden na kwamba taasisi za Afrika kama za nchi za Ghana, Sierra Leone na Côte d'Ivoire zinajifunza kupitia mifumo hii.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Macias, ameeleza kuwa msaada huu wa kifedha unalenga kuimarisha uwezo endelevu wa watafiti vyuoni, maendeleo ya miundombinu ya utafiti, na kuanzisha mifumo ya usimamizi wa utafiti.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto za Uviko-19, Costech imetengeneza mfumo wa kitaifa wa utafiti na kufanikisha miradi iliyozalisha matokeo chanya katika maeneo ya mazingira, teknolojia bora ya uvuvi, na chanjo za mifugo.
Macias amesisitiza kuwa mkataba huu utaimarisha mifumo ya ubunifu na mawasiliano ya sayansi katika vyuo vikuu vya Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Costech, na kwamba wataimarisha mawasiliano ya kisayansi ili kuendeleza tafiti za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha mazingira ya utafiti nchini.