Prime
Siri kudumu kwa biashara ya familia kizazi hadi kizazi
Katika mazingira ya Tanzania ya leo, biashara nyingi huanzishwa kwa juhudi kubwa lakini hufa au kudhoofika mara tu mmiliki anapoondoka au kustaafu. Tatizo kubwa si kukosa wazo la biashara, bali kukosa mpango wa kuandaa mrithi (succession plan).
Urithishaji wa biashara ni mchakato wa makusudi wa kumwandaa mtu au kundi la watu kuendelea na uongozi na uendeshaji wa biashara kwa mafanikio pindi mmiliki anapostaafu au kuondoka.
Kwanza, ni muhimu kuelewa kuwa urithishaji si tukio la ghafla bali ni mchakato unaohitaji muda na mipango. Wamiliki wengi husubiri hadi wanapochoka au wanapokaribia kustaafu ndipo waanze kufikiria nani atachukua nafasi yao. Hii ni hatari kubwa. Biashara inahitaji kuandaa viongozi wake wa baadaye mapema ili kuhakikisha mwendelezo usiovunjika.
Katika Tanzania, tunashuhudia mifano hai ya mafanikio ya urithishaji katika baadhi ya jamii, hususan wafanyabiashara wenye asili ya India na Uarabuni. Biashara nyingi za makampuni ya familia hizi zimeweza kudumu kwa vizazi vingi. Sababu kubwa ni kwamba watoto huanza kuandaliwa tangu wakiwa wadogo.
Wanaingizwa taratibu katika biashara, wakijifunza misingi ya uendeshaji, nidhamu ya fedha, na maadili ya biashara. Wengine hupelekwa kusomea taaluma zinazohusiana na biashara, na baada ya masomo hurudi kuendeleza biashara ya familia kwa ujuzi wa kisasa.
Kwa mfano, katika biashara nyingi za jumla na rejareja zinazoendeshwa na familia za Kihindi hapa nchini, mtoto anaweza kuanza kwa kufanya kazi ndogo kama kuhudumia wateja au kusimamia hesabu ndogo. Kadri anavyokua, anapewa majukumu makubwa zaidi hadi kufikia hatua ya kushika nafasi ya uongozi.
Mfumo huu wa “kujifunza kwa kufanya” huwajengea uwezo wa kiutendaji na kujiamini. Vivyo hivyo, katika baadhi ya familia za Kiarabu zinazojihusisha na biashara za usafirishaji au ujenzi, kuna utaratibu wa wazi wa kumtambulisha mrithi na kumpa nafasi ya kufanya maamuzi chini ya uangalizi wa wazazi.
Sisi Watanzania tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa mifumo hii. Kwanza, ni lazima tubadili mtazamo kwamba watoto ni “warithi wa mali” tu na si “warithi wa ujuzi na uongozi.” Ni muhimu kuwahusisha katika shughuli za biashara mapema, si kwa kuwanyonya, bali kwa kuwajenga. Pili, elimu ni nguzo muhimu. Mrithi anapaswa kuwa na ujuzi wa kitaaluma na pia uzoefu wa vitendo. Mchanganyiko huu humwezesha kuendeleza biashara katika mazingira ya kisasa yenye ushindani mkubwa.
Hatua nyingine muhimu ni kuweka mfumo rasmi wa urithishaji. Wamiliki wanapaswa kuandika mpango unaoeleza nani atachukua nafasi gani, lini, na kwa masharti gani. Mpango huu unaweza kujumuisha mafunzo ya vitendo, tathmini ya uwezo wa mrithi, na hata kushirikisha washauri wa biashara au wanasheria. Hii husaidia kuepusha migogoro ya kifamilia ambayo mara nyingi huibuka pale ambapo hakuna mwongozo wazi.
Aidha, ni muhimu kuwapa warithi nafasi ya kufanya maamuzi na hata kufanya makosa wakiwa bado chini ya uangalizi. Wazazi wengi hushindwa kuachia madaraka kwa wakati, jambo linalochelewesha ukuaji wa kizazi kijacho. Urithishaji mzuri unahitaji ujasiri wa kuachia na imani kwa wale wanaofuata.
Kwa ujumla, biashara ya familia inaweza kuwa urithi mkubwa kwa vizazi vijavyo ikiwa tu kutakuwa na mpango madhubuti wa urithishaji. Tukijifunza kutoka kwa wenzetu walioweza kudumisha biashara zao kwa vizazi, nasi tunaweza kujenga biashara zinazodumu na kutoa ajira kwa muda mrefu. Wakati wa kuanza kuandaa mrithi si kesho, ni leo.