Singida wataka bei nono alizeti

Mkalama. Wakati bei ya mafuta ya kula ikilalamikiwa, viongozi wa Mkoa wa Singida wameiomba Serikali kuweka kodi kwenye mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ili kupandisha bei ya alizeti mkoani humo na kuvutia zaidi oko.

 Viongozi hao walibainisha hayo jana, wakati wa mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo uliofanyika katika Shina namba tano la CCM lililopo katika kijiji cha Iguguno, wilaya ya Mkalama mkoani Singida.

Walimwomba Chongolo kusaidia ili Serikali iweke kodi kwenye mafuta yanayotoka nje ya nchi au kama yataingizwa, basi wanunue na mafuta yanayozalishwa Singida ili wakulima wapate hamasa ya kuzalisha kwa wingi kama ambavyo Serikali imekuwa ikiwahimiza.

Katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23, Serikali iliondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mafuta ya kula ili kusaidia kupunguza bei ya bidhaa hiyo sokoni ambayo ilikuwa ikilalamikiwa na wananchi nchini kote.

Hata hivyo, hatua hiyo ya Serikali imesababisha kushuka kwa bei ya alizeti inayolimwa Singida na kuwakatisha tamaa wakulima. Chongolo ameahidi kushughulikia jambo hilo kwa kwenda kuzungumza na wenzake.

Akizungumzia jambo hilo, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Francis Isaack alisema bei ya alizeti imeshuka na kwamba haiendani na gharama za uzalishaji, jambo linalowakatisha tamaa wakulima.

Alisema kitu kilichosababisha hali hiyo ni mafuta ya kula kuingizwa nchini bila kodi, jambo ambalo limesababisha mafuta ya kula yanayozalishwa ndani ya nchi, hasa Singida kushindwa kushindana sokoni na mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

“Ndugu katibu mkuu, nikuombe utete na Mama (Rais Samia Suluhu Hassan), angalau hata kama yameingizwa bila kodi kutoka nje basi na haya ya alizeti yanunuliwe pia.

“Wakulima wengi wamevunjika moyo wa kulima alizeti kwa sababu msimu uliopita hawajauza alizeti zao, bado zimejaa kwenye maghala kwa sababu bei iko chini sana,” alisema Isaack akimweleza Chongolo.

Akisisitiza jambo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kurudisha kodi ya mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.

“Tukiweka kodi, maana yake tutaweza kushindana, alizeti zetu zitapanda bei, wakulima watapata motisha ya kuzalisha zaidi,” alisema Serukamba wakati akizungumza kwenye mkutano huo.

Serukamba alisema Singida wamelima ekari 600,000 za alizeti, maana yake zikivunwa, asilimia 44 ya mafuta ya kula nchini yatatoka mkoani humo.

Akizungumzia hoja hiyo, Chongolo alisema amelichukua, atakwenda kujadiliana na wenzake kuona namna bora ya kulitatua ili wakulima waendelee kuzalisha kwa faida.

“Tumehamasishana kulima, tumelima. Hatuwezi kuhamasisha wakulima wa nje wakati wa ndani hawanufaiki. Hili nimelibeba, ngoja tukajadiliane na wenzangu huko, tutaleta majibu. Mniamini,” alisema Chongolo.


Wapunguziwa bei ya maji

Ziara ya Katibu Mkuu Chongolo imeshusha neema kwa wananchi wa kijiji cha Iguguno baada ya kushushiwa bei ya maji ambayo wamekuwa wakilalamikia kwa muda mrefu tangu wakipofikishiwa huduma hiyo.

Wakazi wa kijiji hicho wamekuwa wakilipia Sh2,000 kwa unit moja, lakini wakati wa mkutano huo wa Chongolo, Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa), umewahakikishia kwamba bei itapungua hadi Sh1,500 kwa unit moja.

“Moja ya kero zetu ni bei kubwa ya maji, tunauziwa unit moja kwa Sh2,000,” alisema katibu wa shina hilo, John Mseli.