Serikali yaipa kongole NMB kazi ya upandaji miti nchini

Muktasari:
- Katika kuhakikisha kampeni ya upandaji miti inaendelea nchini Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imezishauri taasisi mbalimbali kuhamasisha hatua hiyo muhimu kwa mazingira kama inavyofanya Benki ya NMB.
Kibaha. Katika kuhakikisha kampeni ya upandaji miti inaendelea nchini, Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imezishauri taasisi mbalimbali kuhamasisha kazi hiyo muhimu kwa mazingira kama inavyofanya Benki ya NMB.
Hatua hiyo inakuja wakati NMB ikitenga Sh225 milioni kwa ajili ya kuzizawadia shule bora katika kampeni ya upandaji miti milioni moja ya ‘Kuza Mti Tukutuze’ ambapo shule ya Sekondari ya Mwambisi Forest ya Mamlaka ya Mji wa Kibaja Pwani ikiibuka kinara kwa kupata Sh50 milioni.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Tamsiemi, Mohammed Mchengerwa, wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa shule vinara wa kampeni hiyo iliyozinduliwa Machi, 2023 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na ofisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, Mwambisi Forest ilipanda miche 2,800 na kuikuza kwa asilimia 99, ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Ibondo ya Sengerema iliyopanda na kutunza asilimia 88.5 ya miti yao na kuzawadiwa Sh30 milioni.

“Pongezi za Serikali ziwaendee NMB, sio tu kwa dhamira ya dhati ya utunzaji mazingira kwa kuanzisha kampeni ya upandaji miti milioni moja kote nchini, bali kushirikisha shule 189 kutoka halmashauri zetu zote nchini kote, hii ni njia bora kabisa ya kuibua kizazi chenye mtazamo chanya juu ya mazingira.”
Amesema NMB imethibitisha kuwa sio tu vinara wa masuala ya kifedha, bali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo endelevu ya Taifa na kuutaja uamuzi wa benki hiyo kutenga kiasi hiko cha fedha kwa ajili ya zawadi za motisha kwa shule zitakazostawisha miti, kuwa kielelzo cha dhamira njema ya taasisi hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, amepongeza NMB kwa kutenga kiasi cha Sh100 bilioni za mikopo nafuu kwa wauzaji, wasamabazaji na mawakala wa Nisati Safi ya Kupikia, na kubainisha kuwa fungu hilo la mikopo nafuu linathibitisha dhamira ya dhati ya benki, inayoenda nchi nzima kusaidia jamii kuachana na matumizi ya nishati chafu.
“Wito wangu kwa taasisi nyingine zote nchini, ziige mfano wa NMB kwa kushirikiana na Serikali katika juhudi za kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira, kuboresha elimu, juhudi ambazo zinalenga kukuza uchumi na kustawisha jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Katika zawadi hizo shule ya msingi Itimbo, iliyopo Mafinga mkoani Iringa, ilifanikiwa kupanda miti, kuitunza na kukuza kwa asilimia 83.2 na kujizolea Sh20 milioni, huku shule shiriki 19 zilizopanda miti 1,000 au zaidi na kuwa na ustawishaji wa asilimia 60 ya miti hiyo, kila shule ikizawadiwa Sh2 milioni kila moja.
Aidha, shule nyingine 121 zilizoshiriki ‘Kuza Mti Tukutuze’ ya NMB, zimepewa kifuta jasho cha Sh500,000 pamoja na vyeti vya shukurani kwa kila shule kwa ushiriki bora wa kampeni hiyo iliyoshirikisha shule za msingi na sekondari 189 kutoka katika halmashauri 184 Tanzania bara na visiwani.
Kimori amesema kampeni ina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba walivuka lengo la kupanda miti milioni moja, ikapandwa miti 1,400,000 kote nchini.