Serikali yaahidi kuwathamini wachimba chumvi

Naibu waziri wa madini, Steven Kirusi (wa kwanza kushoto) akikagua madini aina ya chumvi katika machimbo ya chakulu yaliyopo wilayani uvinza, mkoani Kigoma.

Muktasari:

  • Serikali imesema itaendelea kuwathamini wazalishaji katika sekta ya madini hasa wachimbaji wa chumvi nchini kwa kuhakikisha wanaondokana na changamoto zote zinazowakwamisha maendeleo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chumvi kwa wingi.

Uvinza. Serikali imesema itaendelea kuwathamini wazalishaji katika sekta ya madini hasa wachimbaji wa chumvi nchini kwa kuhakikisha wanaondokana na  changamoto zote zinazokwamisha maendeleo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chumvi kwa wingi.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa wakati alipotembelea eneo la uchimbaji wa chumvi Chakulu wilayani Uvinza mkoani Kigoma ili kuzungumza na kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wachimbaji wa kikundi cha Twikome na kukundi cha wakulima cha Kinyo Fam, uliodumu zaidi ya miaka mitano, amesema  lengo wachimbaji wa madini wafanye shughuli zao kwa tija.

Naibu Waziri Kiruswa amesema kutatua changamoto za sekta hiyo inaenda sambamba na kutatua migogoro mbalimbali inayowakabili wachimbaji hao ambao hali ikiwa salama kutachochea ongezeko la uzalishaji wa chumvi nchini na wachimbaji watanufaika na rasilimali hiyo.

"Ninasisitiza kuondoa migogoro katika eneo hili ili kuchochea ongezeko la uzalishaji wa chumvi hapa nchini ili wachimbaji wanufaike na rasilimali hii muhimu," amesema Naibu Waziri Kiruswa.

Aidha Kiruswa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Uvinza kwa kushirikiana na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma kufanya kikao na wamiliki wa leseni na ardhi Februari 20, 2023, kwa ajili ya kuandika makubaliano yaliyofanyika katika mkataba.

Meneja wa Leseni wa Tume ya Madini, Samwel Mayuki amewataka wamiliki wa leseni na wamiliki wa ardhi kukubaliana na pendekezo la kuingia makubaliano ili kuepuka kusitishwa kwa shughuli za uzalishaji wa chumvi endapo mgogoro huo utaendelea au kutakiwa kufanyika kwa fidia ya ardhi.

Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Pius Lobe amevitaka vikundi hivyo wakubaliane ili kuondoa migogoro waliyonayo.

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini,  Nashoni Bidyanguze ameishukuru Serikali kwa kufika kutatua mgogoro huo wa chumvi ambao umechukua muda mrefu, huku akimuomba naibu waziri huyo kuboresha machimbo hayo ili kuongeza uzalishaji wa chumvi, kuongeza mapato ya serikali na wananchi kupata ajira.