Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu

Muktasari:
- Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu hasa vijana hapa nchini ikiwemo kusaidia bunifu zao.
Arusha. Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu hasa vijana hapa nchini ikiwemo kusaidia bunifu zao.
Aidha imewataka vijana kuonyesha bunifu zenye tija ili na zinazoweza kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba 11,2022, jijini Arusha na Afisa Uratibu wa Utafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Bestina Daniel wakati akizungumza kwenye program na shindano la ubunifu kwa vijana wa mikoa ya Kanda ya kaskazini lililoandaliwa na kampuni ya Clouds Media Group.
Amesema serikali inatambua juhudi zinazofanywa na vijana katika kubuni mashine,vifaa na vitu mbalimbali ambavyo vinasaidia kurahisisha matumizi ya teknolojia.
Afisa huyo amewataka wabunifu hao kuwa na mawazo ya kiuhalisia na bunifu zao ziwe zinaangalia jamii na wadau wanataka nini.
Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Maria Mng’ong’o,aliwahamasisha vijana hao kujiunga kwenye vikundi na kuchangamkia fursa ya asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa Serikali iliyotengwa kwaa jili yao kama kundi maalum.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410, taasisi zote nunuzi zinapaswa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi ya mwaka kwa ajili ya makundi maalimu ikiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Akizungumza na vijana hao,Mkurugenzi wa Ndoto Hub, Faraja Nyalandu amesema kuwa kila mbunifu anapaswa kutambua yeye ni kiongozi na kuwa moja ya makosa wanayofanya wabunifu ni kushindwa kufahamu kwamba ubunifu wanaoufanya siyo kwa ajili yao bali ni kwa ajili ya wengine.
Aidha katika mashindano hayo bunifu 14 kutoka kwa vijana wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara ziliwasilishwa huku kundi la SVEPLA(Safe vegetables and plants),linaloundwa na wasichana saba waliohitimu kidato cha sita mwaka huu likiibuka mshindi.
Kiongozi wa SVEPLA Hospia Madikenya (20),amesema wamebuni kifaa cha kupambana na wadudu wanaoshambulia mazao shambani ambayo haitumii kemikali na itasaidia wakulima wengi hapa nchini.
“Tukiwa shule tulienda kwenye mafunzo ya masuala ya sayansi na baada ya mafunzo hayo tulipata wazo hili ambapo kifaa hicho kinasaidia kulinda mazingira na kuhakikisha afya za walaji ziko salama,”amesema
“Tunaomba serikali itusaidie ili tuweze kuboresha kifaa hiki na kiwasaidie wakulima kwani hakitumii kemikali,”alisema
Naye Mkuu wa vipindi wa Clouds Tv, Dotto Bahemu amesema kuwa moja ya vigezo walivyoangalia kwenye bunifu hizo ni pamoja na thamani ya ubunifu,namna itatatua tatizo kwenye jamii,utofauti wake na kuwa wanaamini kifaa hicho kitaweza kuwakomboa wakulima.
Katika programu hiyo vijana hao walionyesha bunifu mbalimbali ikiwemo mashine ya kumenya ndizi,mashine ya kupukuchua mahindi,mashine ya kumenya viazi,kifaa cha kufua umeme na mfumo wa kusaidia wajasiriamali kuuza bidhaa zao mtandaoni.