Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sera jumuishi za kifedha kutatua changamoto za SMEs Afrika

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo akizungumza jijini Arusha leo Jumatatu Mei 11,2026 katika mkutano kidunia wa Taasisi ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Kifedha (Alliance for Financial Inclusion-AFI).

Muktasari:

  • Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anayesimamia uthabiti na usimamizi wa sekta ya fedha, Sauda Msemo, amesema kuwa changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali (SMEs) bado ni kubwa, licha ya mchango wao mkubwa katika ajira na uzalishaji.

Arusha. Wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) barani Afrika na katika nchi zinazoendelea bado wanakabiliwa na vikwazo vya msingi vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia mifumo rasmi ya kifedha.

Kuimarishwa kwa sera za uwiano, matumizi ya teknolojia ya kifedha, kunatajwa kuwa suluhisho kwa wanawake hao wanaokumbana na changamoto kubwa za upatikanaji wa huduma za kifedha, zikiwemo ukosefu wa dhamana na upungufu wa umiliki wa mali.

Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha leo Jumatatu, Mei 11, 2026, na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anayesimamia uthabiti na usimamizi wa sekta ya fedha, Sauda Msemo, wakati akifungua mkutano wa kidunia wa Taasisi ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Kifedha (Alliance for Financial Inclusion - AFI).

Mkutano huo unajadili namna ya kuboresha sera na mikakati ya ujumuishwaji wa wananchi katika masuala ya kifedha, ambao utajadili masuala ya wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), na masuala ya viwango vya kimataifa ikiwemo kisheria na namna vinavyoathiri ujumuishwaji katika masuala ya kifedha.

Amesema miongoni mwa changamoto zinazokabili kundi hilo ni ukosefu wa dhamana za mikopo, ukosefu wa umiliki rasmi wa mali, upungufu wa utambulisho wa kidijitali na mifumo ya udhibiti wa kifedha ambayo haijazingatia mazingira halisi ya wanawake wajasiriamali, hususan wale wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi.

Amebainisha kuwa wanawake wengi katika sekta hiyo ya biashara wanashindwa kupata mikopo kutokana na ukosefu wa rekodi rasmi za kifedha, ukosefu wa mali zinazoidhinishwa kama dhamana, pamoja na changamoto za mifumo ya kitambulisho isiyo jumuishi.

Amesema suluhisho la changamoto hizo linahitaji mageuzi ya kina katika sera za kifedha, kuimarisha mifumo ya kidijitali na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha.

Nyingine ni matumizi ya mifumo ya fedha kwa simu na mifumo ya malipo ya kidijitali kama njia ya kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake na wajasiriamali kwa ujumla.

“Ni muhimu kuhakikisha kwamba sheria na kanuni hazigeuki kuwa kikwazo kwa watu tunaolenga kuwasaidia, hususan wanawake wajasiriamali. Tunafahamu SMEs zinatoa ajira nyingi sana hata katika nchi yetu, hivyo kuleta kipato kwa wananchi wengi,” amesema.

“Tutaangalia ni kwa kiasi gani sheria mbalimbali na kanuni za kimataifa zinaweza kuleta athari kwenye ujumuishwaji wa masuala ya kifedha na namna gani inaweza kufanywa na kuweka miongozo mbalimbali ambayo itasaidia nchi wanachama wa AFI katika kuhakikisha athari hasi katika ujumuishwaji wa kifedha inasimamiwa na kuwekwa uwiano sawa,” amesema.

Naibu Gavana huyo amesema itasaidia kutoathiri masuala ya ustahimilivu wa fedha na ujumuishwaji wa kifedha.

“Kuna sheria na mifumo mbalimbali ya usimamizi wa masuala ya utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi. Sasa wakati unaweka miongozo ya kuhakikisha kwamba nchi zinakuwa na mifumo thabiti ya usimamizi wa masuala haya,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa programu za sera na utekelezaji kutoka AFI, Dk Eliki Boletawa, amesema mkutano huo umeshirikisha washiriki zaidi ya 70 kutoka nchi 44 duniani.

Amesema SMEs ndiyo nguzo kuu ya uchumi wa nchi nyingi kutokana na mchango wao katika ajira na ukuaji wa uchumi katika mataifa mengi duniani kupitia uzalishaji na kukuza uchumi wa wananchi.

“Mfumo wa udhibiti wa uwiano (proportional regulation) ni muhimu kuhakikisha kuwa tunalinda uthabiti wa kifedha bila kuwatenga wale tunaotaka kuwasaidia,” amesema.

Mkurugenzi wa Uendelezaji na Ujumuishaji wa Kifedha kutoka BoT, Kennedy Komba, akielezea safari ya ujumuishaji wa kifedha nchini, amesema sera madhubuti, ubunifu wa teknolojia na ushirikiano wa wadau vinaweza kubadilisha maisha ya wananchi.

Amesema katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma rasmi za kifedha, ambapo mageuzi hayo yalianza mwaka 1991 na kuweka msingi wa ukuaji wa sekta ya benki.