Sekta binafsi nchini yaangazia mikopo nafuu ya kimataifa

Muktasari:
- Hivi karibuni, Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula alifanya mazungumzo na uongozi wa juu wa benki kubwa ya Japan, Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC), katika makao makuu ya benki hiyo jijini Tokyo, Japan.
Dar es Salaam. Sekta binafsi nchini inatarajia kunufaika kuvutia mitaji na mikopo ya gharama nafuu kutoka taasisi za fedha za kimataifa, kufuatia hatua ya rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi kuanzisha mazungumzo ya kimkakati na benki kubwa za kimataifa.
Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Agricom Africa, hivi karibuni alifanya mazungumzo na uongozi wa juu wa benki kubwa ya Japan, Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC), katika makao makuu ya benki hiyo jijini Tokyo, Japan.
Mazungumzo hayo yaliongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha Fedha za Biashara (Trade Finance) wa benki hiyo, Mitsuhiro Kawamura. SMBC ni benki ya pili kwa ukubwa nchini Japan, ikiwa na mali zenye thamani ya Dola 1.9 trilioni
Kabla ya mazungumzo na benki ya SMBC, Ngalula pia alikutana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kubota Corporation, Yuichi Kitao, jijini Osaka, Japan.

Kadhalika Ngalula alipata fursa ya kumtembelea Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda na kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Japan.
Ameeleza kuwa fedha za riba nafuu katika taasisi za kimataifa zipo nyingi, na kinachotakiwa ni kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kuwa na mtazamo mpana na kuziandaa kampuni zao kufikia viwango vinavyokidhi vigezo vya taasisi hizo.
Ngalula amesema pamoja na uwepo wa pesa hizo elimu inapaswa kutolewa kwa nguvu ili Watanzania wengi waelewe vigezo na hatua za kufuata ili kufikia mikopo hiyo.
Pia, ametoa wito kwa wafanyabiashara wachache waliopata fursa hizo kusaidia kuwaelimisha wenzao, ili kwa pamoja wajenge sekta binafsi imara itakayoweza kushindana na kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) ya mwenendo wa uchumi wa kila mwezi. Kwa Februari, 2025 mikopo ya benki za biashara kwenda sekta binafsi ni
Sh36 trilioni zilitolewa huku wastani wa riba za mikopo ukipungua kutoka wastani wa asilimia 15.73 kwa mwaka hadi asilimia 15.14. Sekta zilizoongoza kwa kuchukua kiwango kikubwa cha mikopo ni kilimo kwa asilimia 37.2, ujenzi asilimia 23.1 na ya uzalishaji viwandani kwa asilimia 16.9.