Prime
Sababu Dangote kuifikiria Mombasa badala ya Tanga kujenga kiwanda
Muktasari:
- Kiwanda hicho cha kusafisha mafuta katika ukanda wa Afrika ya Mashariki kina uwezo wa kuchakata mapipa 650,000 kwa siku, huku kinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 15 hadi 17 bilioni za Marekani.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu, Aliko Dangote, amesema anaiangalia zaidi Kenya kama sehemu inayofaa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, badala ya Tanga iliyokuwa imependekezwa awali.
Dangote ametoa kauli hiyo alipofanya mahojiano na Financial Times, ikiwa ni siku chache tangu atangaze utayari wake wa kuzisaidia nchi za Afrika Mashariki kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho ikiwa ziko tayari.
Wakati hayo yakielezwa, wataalamu wa uchumi wametaka kauli hiyo kuchukuliwa kama kitu kitakachoiamsha Tanzania kuangalia mazingira yake ya uwekezaji na kushughulikia mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa zaidi au kuwakwaza wawekezaji.
Katika mahojiano hayo, Dangote amesema anapendekeza Mombasa kwa sababu ina bandari kubwa na yenye kina kirefu zaidi. Kiwanda hicho cha kusafisha mafuta, kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata mapipa 650,000 kwa siku, kinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 15 hadi 17 bilioni za Marekani (Sh38.9 trilioni hadi Sh44.1 trilioni).
“Wakenya wanatumia zaidi, na wana uchumi mkubwa zaidi,” amesema, huku akifafanua kuwa mafuta ghafi yanaweza kusafirishwa kwa meli, hivyo si lazima kiwanda hicho kijengwe karibu na bomba la mafuta litakalobeba mafuta kwa karibu kilomita 1,500 kutoka maeneo ya mafuta ya Uganda hadi Tanga.
“Mpira uko mikononi mwa Rais Ruto. Atakachosema Rais Ruto ndicho nitakachofanya,” amesema.
Ili mradi wa Afrika Mashariki uanze, Dangote amesema atahitaji Rais Ruto kutoa ardhi, kupata fedha kutoka nchi za Afrika Mashariki, sambamba na ulinzi dhidi ya kile alichokiita uingizaji wa mafuta ya bei rahisi kutoka mataifa kama Russia au India.
“Hakuna kiwanda chochote cha kusafisha mafuta duniani kinachoweza kuishi bila ulinzi huo. Tukikubaliana, tunaweza kuanza mwaka huu,” amesema.
Alichosema Ruto
Kabla ya Dangote kutoa msimamo huo, siku chache zilizopita akiwa ziarani nchini Tanzania, Rais wa Kenya, William Ruto, alisema angejua uamuzi wa kujenga kiwanda hicho Tanga ungeleta maneno, basi angependekeza kijengwe Mombasa, Kenya.
“Nimeambiwa kuwa tangazo langu la kusema tujenge refinery Tanga limewakera kiasi, ningejua ningetangaza hiyo refinery ijengwe Mombasa kwa sababu hii ni fursa kubwa,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mei 4, 2026, Ikulu jijini hapa, Ruto alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni fursa kubwa ya biashara, viwanda, ajira, sekta ya petrochemical, viwanda vya plastiki na viwanda vya mbolea.
Alisema alipozungumza na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, walijadili namna ya kufanya ukanda huo uwe wa viwanda kwa kutumia rasilimali za madini, nishati na kilimo, kwani ndiyo sehemu utakapopatikana utajiri, ajira na fursa kwa wananchi.
“Watanzania mna bahati kwa sababu tunajadili kujenga refinery Tanga, ni uwekezaji ambao Serikali ya Kenya iko tayari kuwekeza, Serikali ya Uganda iko tayari kuwekeza, na nilimsikia kaka yangu Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuwa yuko tayari kuwekeza, na nchi nyingine nyingi ziko tayari kuwekeza. Ninaamini na Tanzania iko tayari kuwekeza.
“Hii ni fursa kwa wote kujenga mfumo mkubwa wa biashara na viwanda hapa Afrika Mashariki. Tunatambua kutoka Tanga hadi Mombasa ni kilomita 190 tu. Tayari kuna bomba la mafuta. Tunaweza kutumia miundombinu iliyopo kusafirisha bidhaa na kufanya biashara kubwa pamoja kama nchi na kama sekta binafsi,” alisema.
Mbali na mafuta, alisema nchi hizo pia zinatazama fursa ya kusindika madini yao wenyewe, kwani haiwezekani kuendelea kuuza malighafi bali bidhaa iliyoongezewa thamani.
“Haiwezekani kuendelea kuuza kazi na fursa halafu tunarudishiwa bidhaa zilizoongezewa thamani kwa bei kubwa. Hilo si sahihi. Nimejadili na dada yangu kwamba Tanzania itaongoza njia ya kuhakikisha rasilimali zilizopo Tanzania, Uganda na Kenya zinatumika kwa manufaa ya watu wetu,” alisema.
Awali, Rais Samia Suluhu Hassan alisema alipozungumza na Ruto ndani, alimbana kuwa ametangaza kuwa kiwanda cha kuchakata mafuta kitajengwa Tanga wakati yeye hajashirikishwa.
“Atasema mwenyewe pale kwanini katangaza,” alisema Samia wakati akimkaribisha Ruto kuzungumza.
Wasemavyo wachambuzi
Mchambuzi wa uchumi na biashara, Profesa Abel Kinyondo, amesema ni wakati wa kumuita Dangote na kumuelezea faida zinazoweza kupatikana Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine ili asikilizwe.
“Ile sentensi ya Dangote inatakiwa kuchukuliwa kama call (wito) ya kuangalia baadhi ya vitu vinavyopaswa kufanyika kabla mwekezaji hajaweka hela yake,” amesema.
Amesema Dangote kama mfanyabiashara anaangalia sehemu yenye urahisi kwake, hivyo Serikali ya Tanzania ni vyema iangalie namna ya kumshawishi kuja kufanya uwekezaji huo Tanzania.
“Dangote huyu tayari ana kiwanda cha saruji Mtwara na amekuwa akilalamika katika baadhi ya vitu, ikiwemo vile alivyoahidiwa baadhi yake havifanyiki. Kama mwekezaji anajaribu kutuma ujumbe kwa Tanzania kuwa kuna vitu vinatakiwa kukaa sawa ambavyo kwa Kenya vinaweza kuwa sawa,” amesema.
Amesema hoja ya kusema kina cha bandari ni mambo yanayoweza kubadilishwa, au mazingira ya biashara yanaweza kuimarishwa.
“Tanga na Mombasa ni karibu, hakuna umbali mkubwa. Tunaweza kumuonesha baadhi ya miradi ambayo imefanyika, ikiwemo ule wa bomba la mafuta na vitu vilivyotubeba ili kuongeza ushawishi huo,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Lutengano Mwinuka, amesema mara nyingi wawekezaji kabla ya kufanya uamuzi huangalia vivutio, urahisi katika mazingira ya ufanyaji biashara na mambo yanayotabirika.
“Pia wanaangalia urahisi. Kwetu kumekuwa na utitiri wa mamlaka nyingi zinazotoza kodi. Inaweza kuwa si shida kwa wawekezaji kulipa, lakini kuangalia namna wanavyoweza kulipa vyote katika dirisha moja ndiyo muhimu,” amesema.
Amesema jambo lingine linalopaswa kuangaliwa ni kasi ya utekelezaji, akitolea mfano uongezwaji wa kina cha bandari ya Tanga unaofanyika si kwa haraka kiasi cha kuwezesha kufungua ghati nyingine za bandari hiyo ambazo zingeleta ushawishi.
Katika upande wa kujenga ushawishi, Dk Mwinuka amesema ni vyema kuwaandaa watu watakaokuwa wakizungumza na wawekezaji kwa kuwapa vivutio vya kwanini wawekeze Tanzania, watapata nini na nchi itanufaikaje.
“Na kama kuna changamoto zishughulikiwe. Changamoto nyingine zimekuwa zikishughulikiwa lakini kasi yake si kubwa, na sasa tunaelekea Dira 2050. Sekta binafsi inapaswa kuchangia asilimia 70 ya uchumi.
“Hivyo ni lazima kuweka mazingira mazuri kwa ajili yao. Kuwe na kasi katika utekelezaji, kuwa na kodi zinazolipika ili kuwa na wafanyabiashara wengi, kujenga uchumi mkubwa na miradi ya ubia iangaliwe vizuri,” amesema.