Amsons Group yawashawishi wawekezaji wa Tanzania kupanua biashara Afrika Mashariki
Rais wa Kenya, William Ruto akiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Muktasari:
- Yasema uzoefu wa kampuni hiyo nchini Kenya umekuwa wa mafanikio na wenye mazingira rafiki kwa uwekezaji.
Dar es Salaam. Kampuni ya Amsons Group imewataka wawekezaji wa Kitanzania kutumia fursa zilizopo nchini Kenya na katika ukanda wa Afrika Mashariki kupanua shughuli zao za kiuchumi, ikisisitiza kuwa mazingira ya biashara yanazidi kuboreshwa kutokana na ushirikiano wa kikanda.
Akizungumza Mei 4, 2026 katika maonesho yaliyoandaliwa sambamba na Jukwaa la Uwekezaji Tanzania–Kenya, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Amsons Group, Edha Nahdi amesema uzoefu wa kampuni hiyo nchini Kenya umekuwa wa mafanikio na wenye mazingira rafiki kwa uwekezaji.
“Tumeona Kenya ikiwa soko lenye kiu ya maendeleo ya miundombinu na lenye nguvu kazi yenye ujuzi wa hali ya juu. Uzoefu wetu huko umekuwa wa ukuaji na mapokezi mazuri,” amesema Nahdi.
Jukwaa hilo la uwekezaji lilifanyika sambamba na ziara ya kiserikali ya Rais wa Kenya, William Ruto aliyekuwepo nchini Tanzania kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Nahdi amesema uwekezaji wa Amsons Group nchini Kenya umeingia hatua mpya ya uwajibikaji, baada ya kampuni hiyo kununua asilimia 69 ya hisa za East African Portland Cement Company na pia kuchukua umiliki wa kiwanda cha saruji cha Bamburi, hatua aliyoitaja kuwa inalenga kuunga mkono ajenda ya viwanda na miundombinu ya Kenya.
“Tumeacha kuwa wawekezaji wa kawaida tu; sasa tumebeba jukumu la kuchochea maendeleo ya viwanda na miundombinu,” amesema Nahdi.
Amesema kampuni hiyo pia imewekeza mamilioni ya dola katika miradi mbalimbali ya kikanda, ikiwamo mpango wa Dola 250milioni kwa ajili ya Kiwanda cha Klinka eneo la Kwala nchini Tanzania.
Akihutubia Bunge la Tanzania Mei 5, 2026, Rais William Ruto amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya, akisema kuwa uwekezaji wa pande zote mbili ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Afrika Mashariki.
Ruto amesema kampuni za Kenya zimewekeza zaidi ya Dola 1.7 bilioni nchini Tanzania, zikichangia ajira na uhamishaji wa ujuzi katika sekta mbalimbali zikiwamo viwanda, nishati, usafirishaji na kilimo.
Kwa upande mwingine, amesema uwekezaji wa Tanzania nchini Kenya umefikia zaidi ya Dola 336 milioni na unaendelea kukua kwa kasi.
“Uwekezaji si mtiririko wa mitaji pekee, bali ni kichocheo cha biashara na viwanda. Tunahitaji sera bora zaidi ili kukuza zaidi fursa hizi,” amesema.
Nahdi ameeleza kuwa, kuingia kwa Amsons Group katika soko la Kenya hakukuwa rahisi, akibainisha kuwa kampuni hiyo ilijaribu mara kadhaa kuanzia mwaka 2012, 2017 na 2018 bila mafanikio, hadi ilipofanikiwa mwaka 2024 kupitia mkakati ulioboreshwa.
“Hii si mara ya kwanza kujaribu Kenya. Tulijifunza kutokana na changamoto za awali na mwaka 2024 tukafanikiwa kwa maandalizi bora zaidi,” alisema.
Amesisitiza kuwa Afrika Mashariki ina nafasi kubwa ya kiuchumi ikiwa nchi zitashirikiana badala ya kushindana.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa ongezeko la kampuni za Kitanzania kuwekeza nje ya nchi, ikiwamo Amsons Group, ni ishara ya ukuaji wa sekta binafsi na ushirikiano wa kikanda unaoimarika.
Amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono wawekezaji wake wanaovuka mipaka kwa lengo la kupanua masoko na kuongeza ajira.
Mustakabali wa ushirikiano wa kiuchumi
Nahdi amehitimisha kwa kutoa wito kwa wawekezaji wa Tanzania kutumia fursa za soko la Kenya, akisema nchi hiyo ina nguvu kazi yenye ujuzi na msingi imara wa viwanda.
“Tunapaswa kuiona Afrika Mashariki kama soko moja. Pale mtaji wa Tanzania unapokutana na ubunifu wa Kenya, matokeo yake ni mabadiliko makubwa ya kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) haipaswi kuonekana tu kama taasisi ya kisiasa, bali kama injini moja ya uchumi inayoweza kubadilisha maisha ya wananchi wa ukanda mzima.