Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ripoti yaanika hasara ya mabilioni ya Shilingi, upotevu wa maji

Picha na Mtandao.

Tanzania hupoteza mapato ya takribani Sh182.6 bilioni kila mwaka kutokana na upotevu wa maji unaozidi kiwango kinachokubalika, hali inayoongeza mzigo kwa mamlaka za maji na kuchelewesha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha upotevu wa maji kimeongezeka kutoka asilimia 36.8 mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 42.3 mwaka 2024/25, kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Kiwango kinachokubalika kitaifa ni chini ya asilimia 20, jambo linaloonyesha pengo kubwa kati ya uzalishaji na mapato halisi yanayokusanywa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2024/25, upotevu huo unatafsiriwa moja kwa moja kama fedha ambazo hazikusanywi kutokana na maji yanayozalishwa lakini hayafiki kwa wateja au hayalipwi.

Hata hivyo, baadhi ya mamlaka zimeonyesha kuwa inawezekana kudhibiti upotevu huo. Mamlaka za maji za Nzega, Biharamulo, Mwanhuzi, Maganzo, KASHWASA, Busega na Shinyanga zimefanikiwa kushusha upotevu hadi chini ya asilimia 20, hivyo kupunguza hasara ya mapato.

Kwa upande mwingine, mamlaka kama Mugango-Kiabakari, Same-Mwanga, Rombo, Namanyere, Mbulu, HTM, Dawasa na Mkwajuni zimeripoti upotevu wa zaidi ya asilimia 50, hali inayochochea hasara kubwa zaidi ya kifedha.

Ripoti hiyo pia inaonyesha maboresho katika baadhi ya maeneo, ambapo mamlaka za Ifakara, Kasulu, Liwale, Mpanda na Bariadi zimepunguza upotevu wa maji kwa zaidi ya asilimia 10 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Nzega, Mhandisi Humphrey Mwiyombela, amesema mafanikio yao yanatokana na mbinu ya kugawanya mtandao wa maji katika kanda ndogondogo (District Metered Areas).

Amesema mbinu hiyo inarahisisha ufuatiliaji wa mtiririko wa maji na kubaini kwa haraka maeneo yenye uvujaji au matumizi yasiyo halali.

“Hizo kanda ndogondogo zinaturahisishia kudhibiti upotevu kwa sababu mtandao unakuwa mdogo na wateja wachache, hivyo usimamizi wake ni wa karibu zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa ushirikishwaji wa wananchi kupitia mabalozi wa maji umechangia mafanikio hayo, ambapo kila balozi husimamia kaya kati ya 80 hadi 100 na kutoa taarifa za haraka pale changamoto zinapotokea.

“Hao mabalozi wameunganishwa na mafundi wa kanda. Wakibaini tatizo wanawasiliana nao na matengenezo hufanyika kwa haraka,” amesema, akibainisha pia kuwa mamlaka hiyo imewekeza katika kuboresha miundombinu chakavu na kudhibiti ubora wa vifaa vinavyotumika.

Kwa upande wa Mamlaka ya Maji Shinyanga, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Reuben Mwandumbya, amesema mafanikio yao yametokana na kushughulikia uvujaji kwa wakati na kudhibiti wizi wa maji.

“Tunadhibiti pia mgandamizo wa maji ili mabomba yasipasuke na kusababisha upotevu mkubwa,” amesema.

Hata hivyo, kwa mamlaka zenye upotevu mkubwa, jitihada bado zinaendelea. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Godwin Chacha, amesema tayari wamewasilisha mikakati yao kwa EWURA kwa ajili ya tathmini na ufuatiliaji.

Kwa upande wa wadau, Meneja wa Kiwanda cha Tanzania Breweries Limited, Patel Kilaveli, amesema sekta binafsi ina wajibu wa kushiriki katika kupunguza matumizi na upotevu wa maji. Amesema kampuni hiyo inalenga kupunguza kiwango cha maji kinachotumika kuzalisha bia moja ifikapo mwaka 2030, huku tayari ikiwekeza zaidi ya Sh2 bilioni katika mifumo ya kuchakata maji taka ili kulinda mazingira.

Mbali na hilo, amesema kampuni hiyo imekuwa ikiwezesha jamii zinazozunguka vyanzo vya maji, ikiwemo wakazi wa Ruvu, Kibaha, kujihusisha na ufugaji nyuki kama njia mbadala ya kipato inayosaidia uhifadhi wa mazingira.

Katika kudhibiti upotevu huo, EWURA ilitoa mwongozo wa mwaka 2021 unaotaka mamlaka zote kuhakikisha kiwango cha upotevu hakizidi asilimia 20 ya maji yanayozalishwa. Pia ilitoa mwongozo wa usimamizi wa dira za maji ili kuhakikisha usahihi wa vipimo na ukusanyaji wa mapato.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2024/25, mamlaka za maji 28 kati ya 83 zilikuwa na mikakati iliyoidhinishwa ya kupunguza upotevu wa maji, kutoka mamlaka 25 mwaka uliotangulia. Aidha, mamlaka zote 83 zimeanza kuandaa mizania ya maji (water balance) kupima viwango vya upotevu.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Maji, Waziri wa Maji, Juma Aweso, amesema serikali itaanza kupima utendaji wa wakurugenzi wa mamlaka za maji kwa kuzingatia uwezo wao wa kudhibiti upotevu.

“Wizi wa maji upo. Baadhi ya watendaji wanaruhusu maji yaibiwe na kuandikwa kuwa yamepotea. Pia baadhi ya hoteli na viwanda haviunganishwi kihalali,” amesema.

Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni miundombinu chakavu inayosababisha uvujaji mkubwa pamoja na kutokuchukuliwa hatua kwa taarifa zinazotolewa na wananchi.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Aweso amependekeza kuundwa kwa vikosi kazi maalumu ndani ya mamlaka za maji pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kubaini na kudhibiti upotevu wa maji.

“Tunahitaji mifumo itakayomwezesha mwananchi kutoa taarifa kwa haraka, hata kwa kupiga picha na kuituma. Teknolojia ipo, ni wakati wa kuitumia,” amesema.


Alichokibaini CAG

Kwenye sekta ya maji, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere juzi alipokuwa akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya mwaka 2024/25, alisema upotevu wa maji umeendelea kuisababishia Serikali hasara.

Amesema kwa mwaka 2024/25 upotevu wa maji umeongezeka kufikia asilimia 35 kutoka asilimia 32.

Kiwango hicho kipo juu ya lengo la kitaifa la kutozidi asilimia 20 hali iliyosababisha hasara ya Sh248.78 bilioni huku baadhi ya mamlaka zikiwa na kiwango kikubwa cha upotevu wa maji.

"Same-Mwanga kama anazalisha asilimia 100 ya maji asilimia 70 yanapotea, Dar es Salaam asilimia 53 ya maji yanayozalisha yanapotea, Morogoro asilimia 50 yanapotea kwa maana hiyo asilimia kubwa hayafikii wananchi au yanayowafikia hayatozwi," alisema CAG Kichere.

Alisema chanzo kikubwa cha tatizo ni miundombinu chakavu na wizi wa maji, hali inayoathiri uendelevu wa mapato mamlaka za maji na kupunguza upatikanaji wa huduma na kutegemea ruzuku Serikalini.

“Napendekeza Serikali iimarishe uwekezaji katika ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya maji, mifumo ya upotevu wa maji na kuchukua hatua ya miunganisho haramu kupunguza hasara na kuongeza ufanisi wa sekta.”