Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Riba inavyotafuna mabilioni miradi ya maendeleo

Muktasari:

  • Riba inayotokana na ucheleweshaji wa malipo katika miradi mbalimbali ya maendeleo imeendelea kutafuna mabilioni ya fedha za umma.

Dar es Salaam. Ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na taasisi za umma umeendelea kuwagharimu walipakodi, kutokana na riba inayotozwa Serikali na wakandarasi wa miradi hiyo.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, katika ripoti yake ya mwaka unaoishia Machi 2023 iliyowasilishwa bungeni jana Jumatano, Aprili 16, 2025.

Katika Ripoti ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyowasilishwa bungeni, Kichere ameeleza kuwa ucheleweshaji huo umeisababishia Serikali kulipa ziada ya Sh90 bilioni.

Kiasi hicho cha fedha, kwa mujibu wa CAG, kinahusisha miradi ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda, Daraja la Kigongo–Busisi, ujenzi wa minara ya mawasiliano, ukarabati na ujenzi wa masoko na vituo vya mabasi, pamoja na miradi ya maji vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa).

Pia ametaja ujenzi na matengenezo ya mifumo ya maji taka na Daraja la Pangani pamoja na barabara zake unganishi.

Katika uchambuzi wa stakabadhi za malipo, CAG amebaini wakandarasi wa mradi wa Bwawa la Kidunda walicheleweshewa malipo kwa siku kati ya 16 hadi 299 kuanzia Januari hadi Oktoba 2024, hali iliyosababisha Serikali kutozwa riba ya Sh90.67 bilioni.

Kati ya kiasi hicho, ni Sh8.3 bilioni pekee ndizo zililipwa hadi kufikia Juni 6, 2024, hivyo kuacha Sh82.37 bilioni kama deni la riba linalosubiri kulipwa.

“Ucheleweshaji huu ulitokana na kutofikishwa kwa wakati kwa fedha kutoka Hazina. Licha ya Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuikumbusha mara kadhaa Wizara ya Maji, kucheleweshwa kwa malipo ya vyeti vya muda (IPCs) kuliendelea, na hivyo kusababisha riba kubwa na gharama za ziada,” amesema CAG Kichere.

Amependekeza kuwepo kwa uratibu bora baina ya Dawasa, Wizara ya Maji na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati.

Pia ameshauri kuwepo kwa mipango bora ya kifedha na ufuatiliaji madhubuti ili kuzuia ucheleweshaji wa malipo na gharama za riba kwa siku zijazo.


Kwa upande wa mradi wa Daraja la Kigongo–Busisi, CAG amesema Serikali ililipa Sh4.5 bilioni kama adhabu ya kuchelewesha malipo ya IPCs, kinyume na makubaliano ya mkataba yaliyomtaka mwajiri kulipa ndani ya siku 28 baada ya vyeti kuthibitishwa.

“Ukaguzi wangu umebaini kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) alichelewesha malipo kwa mkandarasi hadi siku 137. Kwa wastani, kila cheti kilicheleweshwa kwa siku 60, ambapo muda mfupi zaidi ulikuwa siku 13 na mrefu zaidi siku 137,” amesema CAG.

Ucheleweshaji huo, amesema ulitokana na Wizara ya Ujenzi kuchelewa kupeleka fedha kwa Tanroads kwa siku kati ya 41 hadi 193. Hata walipopokea fedha, Tanroads walihitaji hadi siku saba kuwalipa wakandarasi.

CAG amependekeza kuwepo kwa mfumo wa pamoja wa ushirikiano kati ya Tanroads, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha IPCs na ankara zinalipwa kwa wakati.

Katika miradi ya minara ya mawasiliano chini ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), CAG ameeleza Sh3.8 bilioni za fidia hazikudaiwa kwa awamu za 5, 5A, 6 na BSZ6 licha ya kuwepo ucheleweshaji wa siku mbili hadi 767.

“UCSAF waliepuka kudai fidia hizo ili kudumisha uhusiano na watoa huduma ambao tayari walikuwa na ugumu wa kufika maeneo ya pembezoni kutokana na kutopata faida. Hii ilidhoofisha nafasi ya UCSAF kudai fidia na kuchochea ucheleweshaji zaidi,” amesema.

Ameishauri UCSAF kutekeleza masharti ya mikataba ya fidia ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kuwajibisha watoa huduma.

Kuhusu miradi ya masoko ya Kariakoo na Mwanza Central, ripoti imebainisha ucheleweshaji wa miezi 13 na 44 mtawalia, uliosababisha miradi hiyo kutokamilika kama ilivyopangwa kufikia Oktoba 2024, badala ya Oktoba 2023 na Februari 2021.

CAG ametaja sababu kuwa ni kuchelewa kuidhinishwa kwa michoro ya kiufundi na mabadiliko ya kazi, ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi na upanuzi wa mradi.

Kwa soko la Kariakoo, ucheleweshaji wa idhini ulitofautiana kati ya siku 17 hadi 78.

Ucheleweshaji huo umesababisha madai ya ushauri wa Sh209.98 milioni kwa Kariakoo na Sh1.14 bilioni kwa soko la Mwanza kama fidia ya muda wa usimamizi ulioongezeka. Wakati wa ukaguzi, madai hayo yalikuwa bado hayajaidhinishwa.

CAG ameshauri Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam na Mwanza kuhakikisha idhini na malipo yanatolewa kwa wakati ili kuharakisha kukamilika kwa miradi na kudhibiti gharama.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa mradi wa Ruwasa wa Morong’anya uliigharimu Serikali Sh711.79 milioni kama riba kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Kadhalika, miradi mitano ya maji taka na usafi wa mazingira ilisababisha riba ya Sh273 milioni.

Kwa upande wa mradi wa Daraja la Pangani na barabara zake, Tanroads ilidaiwa na wakandarasi Sh54.75 milioni kutokana na kuchelewa kulipa IPCs.

Ucheleweshaji huo, amesema ulitokana na bajeti ya Serikali kubanwa na kushindwa kutimiza wajibu katika miradi mingi kwa wakati mmoja.

“Matokeo yake, malipo ya miradi kama Daraja la Pangani yalicheleweshwa mara kwa mara. Hali hii si tu inatishia uwezo wa kifedha wa wakandarasi, bali pia inaongeza gharama zisizo za lazima kwa Serikali kwa njia ya adhabu,” inasomeka ripoti hiyo.

CAG Kichere ameitaka Tanroads kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha na Ujenzi kuhakikisha malipo ya IPCs yanafanyika kwa wakati ili kuepuka adhabu.

Wakati akiwasilisha ripoti ya mwaka 2020/21, CAG Kichere ameonya kuwa Tanzania ilikuwa ikipoteza mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi, uvunjaji wa mikataba ya uwekezaji kinyume cha sheria na uratibu duni baina ya taasisi za Serikali.

Amesema kaguzi maalumu 56 zilifanyika mwaka huo; 37 kwa mamlaka za Serikali za mitaa, 12 kwa Serikali Kuu, sita kwa taasisi za umma, na mmoja kwa mifumo ya Tehama.

CAG ametolea mfano wa mkataba wa Symbion uliogharimu Dola milioni 153.43 baada ya kuvunjwa kinyume na taratibu, kama mojawapo ya hasara kubwa zinazoweza kuepukika.