Reli ya SGR kuundiwa mkoa wa Kitanesco kumaliza kero

Muktasari:
- Reli hiyo imewekewa laini yake, hivyo atakuwepo meneja wa mkoa wa SGR pamoja na timu nzima inayotakiwa kuisimamia.
Dodoma. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limetaja dawa ya kumaliza matatizo katika uendeshaji wa treni ya umeme (SGR), kuwa ni kuanzisha mkoa wa Kitanesco kwenye laini hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 26, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gisima Nyamuhanga huku akikiri kuwepo kwa changamoto ya umeme, inayosababisha usumbufu kwa watumiaji wa reli hiyo.
Nyamuhanga alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kazi zilizofanywa na Tanesco kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akijibu swali la mwandishi aliyehoji jinsi shirika hilo linavyosababisha usumbufu kwa treni ya SGR kutokana na kukatika kwa umeme, amesema:
“Ni kweli kulikuwa na matatizo hayo, lakini katika kipindi hiki, sisi Tanesco na wenzetu upande wa reli tulikuwa tunajifunza, maana mambo haya ni mapya kwetu, lakini tumeshabaini namna ya kumaliza matatizo hayo,” amesema kiongozi huyo.
Mkurugenzi huyo amesema reli hiyo imewekewa laini yake, hivyo atakuwepo Meneja wa Mkoa wa SGR pamoja na timu nzima inayotakiwa kwa lengo la kuisimamia.
Kuhusu ununuzi wa umeme kutoka nchi jirani wakati Tanzania inatajwa kuwa na uzalishaji mkubwa, Nyamuhanga amesema hilo halina shida, kwa kuwa kama nchi haiwezi kujifungia sehemu moja kama kisiwa, badala yake ubadilishanaji wa bidhaa kati ya nchi na nchi utaendelea ilimradi kama unasaidia wananchi.
“Kubadilishana bidhaa katika mipaka ya nchi jirani hilo haliepukiki, ndiyo maana tutaendelea kubadilisha huduma na wenzetu na hili si jambo baya kutokana na mazingira na jiografia yetu, kwa sasa umeme wa Kagera na Sumbawanga tunanunua kutoka kwa majirani zetu hadi tutakapofikisha miundombinu yetu,” amesema Nyamuhanga.

Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Gisima Nyamuhanga
Mtaalamu huyo amekiri kuwa hivi sasa uzalishaji wa umeme umekua kwa kiwango kikubwa na maeneo mengi yameunganishwa kwenye gridi ya Taifa, licha ya kuwepo baadhi ya mikoa ambayo mikakati yake ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2027, kila mmoja unakuwa na umeme wa gridi.
Ameitaja mikoa hiyo ambayo haijaungwa na gridi ya Taifa ni Rukwa, Lindi, Mtwara, Katavi Sumbawanga na baadhi ya wilaya katika Mkoa wa Kagera, licha ya kuwepo ongezeko la wateja waliounganishiwa kutoka milioni 3.17 hadi kufikia milioni 5.39.
Katika kipindi cha miaka minne, Tanesco imetaja kuongeza vituo vya kupoza umeme kutoka 128 vilivyokuwepo hadi 139 na kufanikiwa kudhibiti upotevu wa umeme kutoka asilimia 15.1 hadi kuwa na upotevu kwa asilimia 14.54.
Bwawa la Nyerere
Akizungumzia ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme wa maji la Mwalimu Julius Nyerere, Nyamuhanga amesema umefikia asilimia 99.82.
Hata hivyo, amesema shirika linatupia macho pia katika baadhi ya maeneo ya kuendeleza miradi ya uzalishaji umeme kwa njia ya jua ikiwamo wilayani Kishapu ambako mpaka sasa wamefikia asilimia 50 ya utekelezaji.