RC Dodoma: Bashe na ushirika ni kama mchawi aliyepewa mtoto amlee

Muktasari:
- Hatimaye ndoto ya wana ushirika imetimia, baada ya Benki ya Ushirika Tanzania kuzinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (RC), Rosemary Senyamule amesema kwa namna Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alivyokuwa mpinzani wa ushirika na baadaye akapewa nafasi ya kuukuza inafanana na msemo wa mchawi mpe mwanao akulelee.
Amesema isingetarajiwa mtu aliyekuwa mpinzani wa ushirika na baadaye akapewa nafasi ya kuhakikisha anaukuza na amefanya hivyo kwa mafanikio hadi kufanikisha upatikanaji wa Benki ya Ushirika Tanzania.
Kauli ya Rosemary, inatokana na historia ya Waziri wa Kilimo, Bashe ambaye kabla ya kushika wadhifa huo, alitumia jukwaa la Bunge kukosoa ushirika na usimamizi wa sekta ya kilimo.

Rosemary ameyasema hayo leo Jumatatu, Aprili 28, 2025 alipotoa salamu za Mkoa wa Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa Benki ya Ushirika inayofanyika jijini Dodoma. Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema amekuwa akimsikia Bashe alipokuwa mbunge, katika hoja zake nyingi kuhusu sekta ya kilimo, ziliupinga ushirika.
"Sikujua kilitokea nini akapewa tena nafasi ya uwaziri wa kilimo na akaambiwa akuze ushirika. Sasa nimeelewa kuwa kumbe mchawi alipopewa mtoto akamkuza hadi akazaa na benki," amesema.
Wakati akitoa kauli hiyo, Bashe aliyekaa pembeni mwa Rais Samia walikuwa wakitabasamu, sawia na washiriki wengine wa shughuli hiyo.
Sambamba na hilo, amesema katika mkoa huo kuna wanachama 21,266 wa ushirika wanaounda jumla ya vyama 21 vya ushirika.
Naye Mkurugenzi wa benki hiyo, Godfrey Ng'urah amesema kuanzishwa kwake kunaakisi utekelezaji wa Ilani ya CCM mwaka 2020/25 inayotaka kukuza sekta za uzalishaji na ushirika.
Amesema mchakato wa uanzishwaji wa benki hiyo unatokana na Benki ya Ushirika Kilimanjaro na Tandahimba ambazo mwaka 2014-2020 zilikumbwa na changamoto ya ukwasi.
Baadaye amesema Serikali iliona haja ya kuwa na benki ya ushirika na ndipo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wa wakati huo, hayati Anna Mghwira kuanzisha benki itakayosimamia ushirika.
Amesema ulifika wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilidhamini benki hizo za Tandahimba na Kilimanjaro ili zikopeshwe kwa ajili ya kuinuka tena.

Ameeleza baadaye benki hizo mbili ziliinuka na kuunganishwa na ndipo baadaye ikazaliwa benki ya ushirika iliyopo sasa.
"Benki ya CRDB imesamehe fedha zote Sh10 milioni ilizotoa kufanikisha kuanzishwa kwa benki hii ya ushirika," amesema.
Amesema benki hiyo inaanza ikiwa na matawi manne na bodi ya wakurugenzi inatarajia kufungua matawi mengine manne mwishoni mwa mwaka huu.
Ng'urah amesema wameshasaini makubaliano na Bodi ya Stakabadhi Ghalani na wameanzisha programu maalumu ya kuhakikisha mkulima anapata fedha za mauzo ya mazao yake mapema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Abdulmajid Nsekela amesema wamefanya kazi kuhakikisha ushirika unaunganishwa katika mfumo wa kidijitali ili taarifa zake zipatikane kwa urahisi.
Amewashukuru wana ushirika wa Tandahimba na Kilimanjaro waliokubali kuunganishwa na sasa kuwa wamoja.
Amesema uendeshaji wa benki hiyo hauna tofauti na nyingine na anatarajia kuona ikiendeshwa kwa weledi na bodi inakuwa yenye maadili ili mtaji wa wana ushirika isipotee.
Amesema vyama vingi vya ushirika vina mali nyingi zisizofanya kazi na watahakikisha zinakwenda kutumika na kuanza kuzalisha.

"Nawashukuru wana ushirika kwa kuridhia kuwekeza na matarajio yao ni kutafsiri huduma za ushirika katika bidhaa zilizoundwa. Hivyo huduma zitaendana na bidhaa stahiki," amesema.
Amesema benki imeanza bila mkopo na wanatarajia kuiona ikiwa haina madeni na kinyume na hapo uongozi utakuwa hausimamii vema.