Nanauka ataka Coop Bank ivutie vijana
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa tawi la benki hiyo lililopo Morocco jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa tawi jipya la Coop Bank Tanzania katika eneo la Morocco, Dar es Salaam. Ushirikiano huo unalenga kuhamasisha ujumuishi wa kifedha, kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia elimu na teknolojia.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka ameitaka Benki ya Coop Tanzania na washirika wengine wa kifedha kuhakikisha mfumo wa ushirika hauonekani kuwa wa wanyonge, bali wa watu wenye nguvu ya kujitegemea na kukuza uchumi wao, hivyo kuwavutia vijana.
Nanauka ameyasema hayo leo, Ijumaa Juni 5, 2026 wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo lililopo Morocco jijini Dar es Salaam.
Amesema: "Tukizungumza vijana kwenda kwenye kilimo hatuzungumzii kilimo peke yake, mnyororo wa kilimo ni mkubwa. Kule kwetu Mtwara tunaagiza viuatilifu kwa mabilioni ya fedha, kwenye huo mnyororo tunashindwaje kuwa na vijana tukawapa tenda za kufanya hizo kazi?
"Leo korosho wanawekeza vitalu, wanawagawia vijana mbegu, hiyo kazi kwa nini isifanywe na vijana waliokopeshwa kupitia Coop Bank na kuwa na vitalu na kusambaza kwa sababu soko lipo tayari," amesema.
Nanauka amesema katika mazao ya korosho na kahawa hakuna vijana wanaolima, wakati ndiyo yanayoiingizia nchi fedha nyingi za kigeni.
Amesema vijana wengi wanajitenga na ushirika kwa sababu unaonekana kama mfumo wa wazee pekee. Kutokana na hilo, kazi kubwa ya sasa ni kubadili fikra na mitazamo ya vijana ili wajiunge na ushirika.
Katika hatua nyingine, kwenye hafla hiyo, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imesaini mkataba wa ushirikiano wa uhamasishaji wa ujumuishaji wa kifedha na Benki ya Coop.
Makubaliano hayo yanalenga kuhamasisha ujumuishaji wa kifedha, kuongeza uelewa wa huduma za kifedha na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na majukwaa ya kidigitali.
Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Mkurugenzi wa Biashara MCL, Kadambara Maita amesema ushirikiano huo ni zaidi ya mahusiano ya kibiashara, kwani unalenga kutumia nguvu ya habari na mawasiliano kufikisha kwa wananchi fursa mbalimbali za kifedha na maendeleo.
“Huu sio ushirikiano wa kawaida kibiashara. Ni ushirikiano wa simulizi zenye mguso, ushawishi chanya na maendeleo endelevu ya taifa,” amesema.
Kupitia ushirikiano huo, amesema taasisi hizo mbili zitafanya kazi kwa pamoja kuelimisha wananchi kuhusu huduma za kifedha, matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha, uwezeshaji wa wajasiriamali na fursa zinazopatikana kupitia mfumo wa ushirika.
Kadambara amesisitiza juhudi hizo zinakusudia kuyafikia makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wadogo, vijana, wanawake na wakulima wanaohitaji huduma za kifedha ili kukuza shughuli zao za uzalishaji na biashara.
Amesema MCL itaunga mkono utekelezaji wa ushirikiano huo kupitia magazeti yake ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti pamoja na majukwaa yake ya kidigitali yanayofikiwa na mamilioni ya watumiaji kila mwezi.
Amesema malengo ya Coop Bank ya kuleta “Ustawi kwa Wote” yanaendana na dira ya MCL ya “Tunaliwezesha Taifa”, hali inayoweka msingi wa ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi na uchumi wa nchi.
Aidha, Kadambara amesema ushirikiano huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi unaochochewa na matumizi ya teknolojia, upatikanaji wa huduma za kifedha na ushiriki wa makundi yote katika maendeleo.
Sambamba na utiaji saini wa makubaliano hayo, Coop Bank Tanzania ilizindua tawi jipya la Morocco, hatua inayolenga kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha katika Jiji la Dar es Salaam.
MCL imeipongeza Coop Bank kwa kuendelea kupanua mtandao wa huduma zake nchini na kuwekeza katika mikakati inayochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi wa Taifa.