Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki ya Coop ilivyojipanga kuteka soko la huduma za kifedha Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah akifanya mahojiano maalumu na Mhariri wa Uchumi wa Biashara wa Mwananchi, Ephrahim Bahemu. Mahojiano hayo yalifanyika katika tawi jipya la benki hiyo jijini Dar es Salaa. Picha na Michael Matemanga

Dar es Salaam. Benki ya Ushirika (Coop Bank) imejipanga kwa kasi kujiweka katika nafasi ya juu kwenye sekta ya huduma za kifedha nchini, ikilenga kuchochea ujumuishi wa kifedha na kukuza uchumi jumuishi kupitia sekta ya ushirika na kilimo biashara.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah, anasema mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa benki hiyo umekuwa wa mafanikio makubwa, huku ukithibitisha kuwa sekta ya ushirika na shughuli za kilimo zinaweza kuwa msingi imara wa biashara ya kibenki.

“Tumethibitisha kuwa kuna fursa kubwa sana katika kuchagiza ujumuishi na ukuaji wa pamoja kupitia mifumo na modeli za ushirika,” anasema Ng’urah, akieleza pia shukrani zake kwa Rais na Serikali kwa ushirikiano wanaoupatia benki hiyo.

Anabainisha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, benki imepiga hatua kubwa katika viashiria vya kifedha. Mizania ya benki imeongezeka kutoka Sh49 bilioni wakati wa kuanzishwa hadi kufikia Sh178 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

“Wakati tunaanza tulikuwa na mikopo ya Sh14 bilioni, lakini sasa kitabu cha mikopo kimefikia Sh101 bilioni. Amana pia zimepanda kutoka chini ya Sh15 bilioni hadi kufikia Sh102 bilioni,” anafafanua.

Kwa upande wa mtaji wa wanahisa, Ng’urah anasema umeongezeka kutoka Sh27 bilioni hadi Sh42 bilioni, huku ubora wa mikopo ukiendelea kuimarika, ambapo mikopo chechefu imeshuka kutoka asilimia 2 hadi asilimia 1.

Anasema mafanikio hayo hayajaishia kwenye takwimu pekee, bali pia yanaonekana katika upanuzi wa huduma. Idadi ya matawi imeongezeka kutoka matatu hadi saba, huku mipango ikiendelea kufungua matawi mapya katika mikoa ya Mwanza, Mbeya na Arusha.

“Tayari tumefungua matawi Kagera, Mtwara Mjini na Tabora, na sasa tuko hatua za mwisho kukamilisha Mwanza kabla ya kuelekea Mbeya na Arusha,” anasema.

Ng’urah anasisitiza kuwa mafanikio ya benki hiyo yanatokana na maamuzi ya kimkakati yaliyofanywa na bodi na wanahisa tangu kuanzishwa kwake, yakilenga sekta yenye uhitaji mkubwa wa mitaji hasa kilimo na ushirika.

“Siri yetu ni kujikita kwa wale wanaohitaji fedha kwa ajili ya shughuli zao. Kwa kufanya hivyo, tulijikuta tunashindana na maono yetu wenyewe. Ukweli ni kwamba kuna ‘bahari’ kubwa ya fursa katika sekta ya ushirika ambayo bado haijaguswa kikamilifu,” anasema.

Anaeleza kuwa Benki ya Coop si taasisi mpya kabisa, bali ni matokeo ya muunganiko wa benki za ushirika zilizokuwapo awali, zikiwamo Benki ya Ushirika Kilimanjaro na Benki ya Ushirika Tandahimba.

“Tumepitia mchakato wa mageuzi (transformation) na kuunganisha uzoefu wetu. Kabla ya muunganiko, baadhi ya benki hizi zilikuwa zikikumbwa na hasara ya zaidi ya Sh600 milioni, mitaji hasi na mikopo chini ya Sh1 bilioni. Leo hii, hali ni tofauti kabisa,” anasema.

Kwa mujibu wa Ng’urah, mafanikio ya sasa si ya muda mfupi, bali ni matokeo ya mikakati ya muda mrefu iliyolenga kuijenga benki kwa msingi imara na endelevu.

Katika kupanua wigo wa wateja, benki hiyo imeamua kutotegemea vyama vya ushirika pekee, bali pia kuwafikia wafanyakazi, wajasiriamali na wadau wote wa mnyororo wa thamani katika kilimo biashara.

“Kila mtu anayehusika katika kilimo biashara ni mteja wetu. Tumeangalia changamoto zinazowazuia watu kutumia huduma za kibenki na kuzitatua, ikiwamo kupunguza gharama za mikopo kwa kutafuta vyanzo mbadala vya fedha,” anasema.

Anaongeza kuwa hatua hiyo imewezesha benki kutoa mikopo kwa riba nafuu ya tarakimu moja (asilimia 9 hadi 10), hasa kwa vyama vya ushirika vinavyopata fedha kwa gharama ya chini.

Katika kuhakikisha huduma zinawafikia Watanzania wengi zaidi, benki hiyo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), hatua inayowezesha utoaji wa huduma bila hitaji la mteja kufika tawi la benki.

“Tumejenga mifumo imara ya Tehama inayotuwezesha kutoa huduma nchi nzima. Pia kupitia vyama vikuu vya ushirika, tuna mawakala wanaowezesha uwekaji na utoaji wa fedha kwa urahisi,” anasema.

Ng’urah anabainisha kuwa benki hiyo inalenga kuwa na wateja milioni 10 ifikapo mwaka 2030, lengo analosema linawezekana kutokana na mkakati waliouweka.

“Ajenda yetu ni kuchochea ustawi jumuishi. Tunataka kila Mtanzania awe na akaunti ya benki, bima, na uwezo wa kupata mikopo na kufanya miamala. Fedha iwe na haki ya uraia,” anasisitiza.

Anaeleza kuwa msingi wa kufikia lengo hilo ni mtandao mkubwa wa vyama vya ushirika nchini, ambapo kuna zaidi ya vyama 10,000 vyenye wanachama zaidi ya milioni nane, pamoja na zaidi ya watu milioni mbili wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

“Tuna orodha na taarifa za wanachama kupitia mifumo yetu ya Tehama, hivyo tuna uwezo wa kuwafikia kwa urahisi na kuwapa huduma stahiki,” anasema.

Kwa sasa, idadi ya wateja wa benki hiyo imeongezeka kutoka 5,000 hadi 36,000 ndani ya muda mfupi, hatua inayotoa taswira ya ukuaji wake wa kasi.

Ng’urah anaamini kuwa iwapo mkakati wao utafanikiwa, Benki ya Coop itakuwa kinara kwa idadi ya wateja nchini ifikapo 2030, huku pia ikipunguza pengo la watu wasio na huduma za kifedha kwa takribani asilimia 50.

Anasema kundi kubwa la watu walioko nje ya mfumo wa kibenki ni wakulima wadogo na wajasiriamali, ambao wengi wao wameunganishwa kupitia vyama vya ushirika eneo ambalo benki hiyo inalipa kipaumbele.

Pamoja na kupanua wigo wa wateja, benki hiyo pia imeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti mikopo chechefu kwa kuimarisha utawala bora, kuwekeza katika rasilimali watu yenye weledi na kutumia mifumo ya kisasa inayopunguza uingiliaji wa kibinadamu.

Ng’urah anasisistiza kuwa kuwekeza katika kilimo ni sawa na kuwekeza katika uchumi wa taifa, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo.

“Ukishughulikia kilimo, unakuwa umeshughulikia uchumi na maisha ya watu wengi. Hilo ndilo eneo tulilochagua kulipa kipaumbele,” anasema.

Kwa wadau na wateja, Ng’urah anasema wanapaswa kutarajia huduma zenye gharama nafuu, kasi, uhakika na ubora. “Sisi ndiyo chaguo sahihi kwa huduma za kifedha gharama nafuu, haraka na zenye uhakika.”