Msajili wa Hazina aonya taasisi za umma zenye utendaji duni
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, akizungumza katika mahojiano maalumu kuelekea Siku ya Gawio itakayofanyika Juni 30, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Miongoni mwa matendo yanayotafsiriwa kuwa utendaji usioridhisha kwa taasisi za umma ni kushindwa kutimiza malengo ya faida na kuchangia ipasavyo katika mapato ya Serikali.
Dar es Salaam. Serikali imezitaka taasisi za umma zenye mwenendo wa utendaji usioridhisha kujitathmini na kuchukua hatua za haraka za kujiboresha, ikisisitiza haitazivumilia muda mrefu.
Miongoni mwa matendo yanayotafsiriwa kuwa utendaji usioridhisha kwa taasisi hizo ni kushindwa kutimiza malengo ya faida na kuchangia ipasavyo katika mapato ya Serikali.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alipozungumza katika mahojiano maalumu kuelekea Siku ya Gawio itakayofanyika Juni 30, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam.
Amesema taasisi zote zinazostahili kuwasilisha gawio na michango mingine serikalini zinapaswa kutekeleza wajibu huo kwa wakati.
Amesisitiza kuwa mashirika ya umma si mali ya bodi za wakurugenzi au menejimenti, bali ni mali ya wananchi kupitia Serikali, hivyo kurejesha mapato yanayostahili si hiari, bali ni wajibu.
“Lazima taasisi zetu ziyaishi malengo ya faida ambayo huwa tunazipa. Kiongozi ambaye ataendelea kushindwa kuleta gawio kwa kipindi kirefu, huyo hatufai,” amesema.
Mchechu ameongeza kuwa gawio na michango mingine kwa Serikali vinapaswa kutokana na faida au ziada halisi ya taasisi husika, badala ya fedha za mikopo.
Amesema taasisi zinazokopa fedha ili kutoa gawio zinatoa taswira isiyo sahihi kuhusu hali halisi ya utendaji wake.
“Ukikopa ili utoe gawio au mchango mwingine kwa Serikali, unakuwa unamdanganya Rais na hata nafsi yako mwenyewe,” amesema.
Kuhusu hatima ya taasisi zitakazoshindwa kufanya vizuri, Mchechu amesema kufutwa au kuunganishwa kwa taasisi za umma ni mchakato unaofuata taratibu maalumu na hauamuliwi na matokeo ya Siku ya Gawio pekee.
Amesema Serikali huzipa taasisi hizo muda wa kufanya maboresho, na pale zinaposhindwa kuonesha mabadiliko ndipo hatua zaidi huchukuliwa.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) ilikusanya Sh1.028 trilioni kupitia gawio na michango mingine kutoka kwa mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, kiwango kilichoweka rekodi mpya tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo mwaka 1959.
Licha ya mafanikio hayo, Mchechu amesema bado kuna fursa kubwa ya kuongeza makusanyo kupitia uboreshaji wa utendaji wa taasisi za umma na usimamizi wa uwekezaji wa Serikali.
“Tunategemea tutaanza na nguvu mpya, mwaka huu tutavunja rekodi ya mwaka jana na mwakani tutavunja rekodi ya mwaka huu,” amesema.
Kauli hizo zinaendana na msimamo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye amewahi kuonya taasisi na mashirika ya umma yanayoendelea kuonesha utendaji usioridhisha kwamba yako hatarini kufutwa au kuunganishwa endapo hayataboresha utendaji wake.
Profesa Mkumbo amesema haiingii akilini kuona baadhi ya mashirika yakishindwa kutoa gawio stahiki licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.
“Ni afadhali kuwa na mashirika machache ya biashara, lakini yanayotoa gawio stahiki kwa Serikali,” amesema.
Kwa mujibu wa OTR, Serikali inamiliki hisa katika taasisi na kampuni 308, ambapo 91 ni za kibiashara na 217 ni za kutoa huduma za umma. Serikali imewekeza takribani Sh92.3 trilioni katika taasisi hizo.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara wa OTR, Lightness Mauki, amesema ofisi hiyo itaendelea kuimarisha usimamizi wa utendaji ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na usimamizi wa uwekezaji wa Serikali.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kibiashara wa OTR, David Shambwe, amesema mashirika hayo yanapaswa kuonesha matumizi bora ya rasilimali za umma na utoaji wa huduma wenye tija licha ya kutokuwa na lengo la kuzalisha faida.
Amesema kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kutasaidia kuhakikisha mashirika hayo yanatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, uwajibikaji na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma.