Ofisi ya Msajili Hazina sasa kubadilishwa jina

Viongozi na Watendaji wa Taasisi mbalimbali wakisikiliza na kufuatilia kwa makini hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua Kikao Kazi kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Haziana. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Ofisi ya Msajili wa Hazina sasa kubadilishwa jina na kuitwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, ili kuendana na wakati na kuongeza tija.
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema jina la taasisi hiyo litabadilika kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji majukumu yao.
Mchechu amesema hayo jana Jumapili Agosti 20, 2023 jijini Arusha katika mwendelezo wa kikao kazi cha Wenyeviti na Watendaji wa Mashirika ya Umma chenye lengo la kuongeza ufanisi na tija.
Kikao hicho, kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), chenye mada ‘uimarishaji wa utendaji taasisi na mashirika ya umma’ kilifunguliwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyewataka Watanzania kuwa na imani na Serikali katika mageuzi ndani ya mashirika na taasisi za umma.
Akiwasilisha mipango na mikakati ya ofisi hiyo, Mchechu amesema, “kwa kuzingatia majukumu ya sheria ya msajili wa hazina hasa uwekezaji na umma, jina hili halizingatii jukumu hili kubwa la msingi wa uangalizi, sambamba na majukumu mengine ya ushauri, usimamizi na ubinafsishaji.
“Mabadiliko ya jina linalopendekezwa litakidhi matakwa ya sheria ya mamlaka na majukumu ya Msajili wa Hazina na kuiwezesha ofisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Kulikuwa na hoja nyingi mbona mamlaka zipo nyingi, mbona tutajishusha, lakini jambo majukumu tulionayo,” amesema Mchechu.
Mchechu aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) amesema jina la Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, linaendana na wakati uliopo kwa sababu kila kinachofanyika kinaendana na uwekezaji.
“Jina linapoanza kusomeka linawabadilisha fikra watu na kuwakumbusha kitu kinachotakiwa kufanyika,” amesema Mchechu aliyeteuliwa na Rais Samia Februari 24 mwaka huu, kuwa Msajili wa Hazina.
Katika hatua nyingine, Mchechu amesema majukumu yatakayorudishwa kwa taasisi na masharika ya umma hayataangalia sura, bali maandiko ya miundo mkakakati yatakayowezesha taasisi au mamlaka husika kufikia malengo waliojipangia.
Pia, amesema miongoni mwa vigezo vya taasisi kupewa uhuru wa kujiendesha ni pamoja na maslahi na malengo ya kimkakati ya nchi, uchangiaji wa mapato yasiyo ya kikodi katika mfuko mkuu wa Hazina, uwezo wa kujiendesha kwa mapato ya ndani ya taasisi kutegemea Serikali.
“Vigezo vya uhuru viko vingi vipitieni (wakuu wa taasisi na masharika) na kujiridhisha ndio mkataba wetu na nanyi wa kukurudishieni mamlaka yenu...,” amesema.
Juzi akifungua kikao kazi hicho, Rais Samia alizungumzia kuhusu maboresho ya mashirika ya umma, kuna baadhi ya yataunganishwa na mengine kuondolewa. Hata hivyo, aliagiza Ofisi ya Hazina, kuzungumza na mashirika hayo na kupata maoni yao kabla ya kuunganishwa ama kufutwa.