Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango maalumu kupunguza matumizi chupa za plastiki

Muktasari:

  • Mpango huu unakuja wakati ambao ripoti ya tathmini ya hali ya uchumi ya Aprili mwaka huu iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la uingizaji wa bidhaa za plastiki kutoka nje ya nchi.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kupiga vita matumizi ya chupa za plastiki kutokana na athari zake katika mazingira, Kampuni ya AGL Tanzania imezindua kampeni maalumu ya kupunguza matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja.

Hatua hiyo inayolenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuchangia mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kupitia mpango unaojulikana kama ‘Plastic-Less’, kampuni hiyo imeanza kutekeleza mabadiliko mbalimbali ndani ya maeneo yake ya kazi huku ikipanua juhudi hizo kwa jamii kupitia shughuli za uwajibikaji kwa jamii (CSR).

Mpango huu unakuja wakati ambao ripoti ya tathimini ya hali ya uchumi ya Aprili mwaka huu inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la uingizaji wa bidhaa za plastiki kutoka nje ya nchi kutoka zenye thamani ya Sh2.09 trilioni mwaka ulioishia Machi 2025 hadi kufikia Sh2.147 trilioni.

Akizungumza kuhusu mpango huo jana Jumatano, Juni 10, 2026, Meneja wa Masuala ya Sheria wa AGL Tanzania, Angeline Mtulia amesema uendelevu umeendelea kuwa sehemu ya msingi wa shughuli za kampuni hiyo ukibebwa na ahadi ya ushirikishaji wafanyakazi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Kupitia mpango wa ‘Plastic-Less’, tumeonesha kwamba mabadiliko madogo ya tabia, yanapoungwa mkono na miundombinu sahihi pamoja na ushirikiano wa kijamii, yanaweza kuleta matokeo yenye manufaa makubwa kwa mazingira na jamii,” amesema.

Akielezea utekelezaji wa kampeni hiyo amesema wamegawa chupa za maji zinazoweza kutumika tena kwa wafanyakazi wake wote ili kupunguza matumizi ya chupa za plastiki zinazotupwa baada ya matumizi.

Hilo limeenda sambamba na kuweka visambaza maji katika vyumba vya mikutano na maeneo mbalimbali ya kazi ili kurahisisha upatikanaji wa maji na kuwahamasisha wafanyakazi kujaza tena chupa zao badala ya kutumia plastiki za matumizi ya mara moja.

“Kwa wageni wanaotembelea kampuni hiyo, AGL imeanzisha matumizi ya glasi zinazoweza kuoshwa na kutumika tena, hatua inayolenga kupunguza zaidi taka za plastiki zinazozalishwa kila siku,” amesema.

Uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo ulifanyika Juni 5 mwaka huu sambamba na maadhimisho ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi chini ya kaulimbiu ya ‘Act Now for the Climate’.

Katika hafla hiyo, timu ya Ubora, Afya, Usalama na Mazingira (QHSE) ya kampuni ilitoa elimu kuhusu umuhimu wa kupunguza matumizi ya plastiki na namna kila mfanyakazi anavyoweza kuchangia kulinda mazingira kupitia mabadiliko ya tabianchi.

Sehemu ya maadhimisho hayo ilihusisha mafunzo ya usimamizi wa taka na uhifadhi wa mazingira yaliyotolewa kwa ushirikiano na kundi la urejelezaji taka la The Recyclers.

Kupitia mafunzo hayo, wafanyakazi walipata elimu kuhusu athari za matumizi ya plastiki kwa mazingira na umuhimu wa kutenganisha taka pamoja na kuhimiza matumizi ya bidhaa zinazoweza kutumika kwa muda mrefu.

Mbali na juhudi za ndani ya kampuni, AGL kupitia kampuni dada ya Eastern Africa Logistics Services (EALS) ilipeleka kampeni hiyo katika Shule ya Sekondari Mabibo jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, kampuni hizo zilitoa mapipa 12 ya kuhifadhia taka, vizima moto 27 pamoja na king’ora cha tahadhari ya moto kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa mazingira na usalama wa wanafunzi.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya kampuni hizo na shule hiyo, ambao ulianza mwaka 2025 kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyoo na maktaba.

Wanafunzi wa shule hiyo walipata mafunzo kuhusu madhara ya matumizi ya plastiki kwa mazingira na umuhimu wa kubadili tabia ili kupunguza uchafuzi wa mazingira, sambamba na kufundishwa namna sahihi ya kutenganisha taka kwa kutumia mapipa yaliyowekwa alama maalumu kwa ajili ya taka za chakula, plastiki na nyinginezo.