Mikakati mipya ya Zipa kuifungua Pemba kiuchumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohamed
Muktasari:
- Jitihada hizo ni pamoja na kuifanya kuwa mwenyeji wa kongamano kubwa la uwekezaji litakalofanyika visiwani humo.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), imeeleza jitihada inazofanya katika kuvifungua visiwa vya Pemba, ikiwemo kuwa mwenyeji wa kongamano kubwa la uwekezaji litakalofanyika visiwani humo.
Hayo yamesemwa leo, Jumanne, Aprili 15, 2025, na Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohamed, alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), zilizopo Tabata, jijini Dar es Salaam.
Mohamed amesema kongamano hilo la siku tatu, litakalofanyika kuanzia Mei 7 hadi 10, lina lengo la kuwashawishi wawekezaji kwenda kuwekeza Pemba, wakiwemo wa ndani na nje ya nchi, ambapo watu zaidi ya 1,000 wanatarajiwa kushiriki.
“Katika siku zote hizo tatu, wawekezaji hao watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuwavutia kufanya uwekezaji, ikiwemo kwenye misitu, mali kale na shughuli za uvuvi.
“Pia watapata nafasi ya kutembezwa maeneo ambayo Serikali imeyatenga kwa ajili ya uwekezaji na yale ambayo wananchi wangependa kuingia ubia na watu kufanya uwekezaji,” amesema mkurugenzi huyo.
Aidha, katika kongamano hilo amesema kutakuwepo na shughuli mbalimbali, ikiwemo matembezi yatakayofanyika siku ya kwanza, lengo likiwa kuunga mkono juhudi za viongozi kuyafanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha.
Shughuli nyingine itakayofanyika ni kongamano lenyewe litakalofanyika siku ya pili, ambalo litakwenda sambamba na kuzinduliwa kwa jarida linaloelezea uwekezaji visiwani Zanzibar.
“Siku ya tatu kutakuwa na dhifa ya kitaifa. Katika siku zote hizo tatu kutakuwa na maonyesho na majadiliano mbalimbali kutoka kwa washiriki,” amesema Mohamed.
Malengo ya kufanya hayo, amesema, ni katika kuifungua Pemba kibiashara, ambayo ilikuwa imesahaulika kwa muda mrefu kiasi kwamba mtu akifika Unguja hudhani tayari amemaliza Zanzibar yote.
Akielezea hali ya uwekezaji visiwani humo, Mohamed amesema kwa kipindi cha miaka mitano, Zipa imesajili miradi 480 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6 (Sh16.1 trilioni).
Eneo jingine alilotaja Mohamed ni safari za baharini, afya, viwanda, mafuta na gesi.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa Zanzibar ipo tayari kwa ajili ya uwekezaji kwa mtu yeyote, ilimradi awe amefuata sheria na taratibu zote za nchi, huku akizitaja sekta za kipaumbele kuwa ni utalii, uchukuzi baharini, afya, viwanda, mafuta na gesi.