Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mageuzi mapya kwa ushirika

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa kipindi cha miaka zaidi ya 20 nyuma, sekta ya ushirika haikuwa ikifanya vizuri na akiwa miongoni mwa waliokosa imani nayo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuimarishwa kwa ushirika na matumizi ya Tehama katika uendeshaji wake, ndizo nyenzo zitakazowezesha ukuaji wa sekta hiyo iliyopitia milima na mabonde.

Amesema kwa kipindi cha miaka zaidi ya 20 nyuma, sekta hiyo haikuwa ikifanya vizuri, naye akiwa miongoni mwa waliokuwa wanaichukia.

Katika kufanikisha uimarishwaji wa ushirika, mkuu huyo wa nchi ameitaka Wizara ya Kilimo iwe na jicho la karibu, kulea na kuhamasisha wakulima kujiunge katika sekta hiyo ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa masoko.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu, Aprili 28, 2025 alipohutubia hafla ya uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania jijini Dodoma.

Amesema kihistoria sekta ya ushirika haikuwa ikifanya vizuri na ilionekana kama kichaka cha upigaji, hivyo kuwapo haja ya kuimarishwa ili iwe na manufaa kwa wakulima na Serikali kwa ujumla.

"Kwa uelewa wangu miaka labda 20 au 15 nyuma, ushirika haukuwa unafanya vizuri kabisa na wale waliokuwa hawana imani na ushirika nilikuwa mmoja wao sio Bashe (Waziri wa Kilimo) peke yake," amesema.

Lakini, amesema kwa namna inavyokwenda na viongozi wapya na mabadiliko ya mifumo, ushirika umeanza kusimama vizuri na unamwongezea hamu ya kuongeza uwekezaji ili ukue zaidi.

"Mwaka 2018 nilifanya ziara Shinyanga, kuzungumza na wananchi kuna bwana alikuwa akiitwa Emmanuel Cherehani (sasa hivi ni mbunge wa ushetu), alikuja kuniona akaniambia sisi wana ushirika tunacheleweshewa kupata mbegu, mbolea akaniambia tupeni ruhusa sisi tuna fedha zetu tuagize wenyewe," amesema.

Alipomuuliza shida iko wapi, amesema akaambiwa tume ya ushirika ndio inayosababisha washindwe kuagiza kwa kuwa imeweka masharti mengi.

Hata hivyo, amesema hilo limekomeshwa kwa sasa kwani tayari wana ushirika wana haki ya kwenda kukopa fedha na kuagiza mahitaji yao.

Ametaka kuwepo ubunifu utakaowezesha wakulima wajiunge na mifumo na waweke akiba, ikiwemo bima za afya.

"Tunavyokwenda kutumia Tehama na mifumo mbalimbali ile ujanjaujanja itaenda kupungua," amesema.

Amesema wanatamani sasa kuona vyama vya ushirika vinakuwa na viwanda vyao kwa ajili ya kuongeza thamani bidhaa za kilimo kwa viwango vinavyokubalika.

Amesema vyama hivyo vimeanza kukopa kwa ajili ya kujenga maghala jambo litakalofanya mazao yawe katika hali nzuri hata sokoni.

"Upande mwingine tunafungua masoko uzalishaji unakuwa mdogo," amesema.

Ametaka vyama vya ushirika vijiendeshe kibiashara, uwazi na fedha za mahesabu zisomwe kwa wakati ili kujenga imani kwa wana ushirika.

"Vyama vyote vya ushirika vitumie mifumo ya Tehama, ili vyote viwasiliane," amesema.

Katika hotuba yake hiyo, Raia Samia ameitaka Wizara ya Fedha ya  kilimo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zikae kuzungumza ili kuja na sera itakayoitoa nchi katika ombwe la mikopo kwenye sekta ya kilimo.

"Kuwe na sura inayoeleweka ambayo Tanzania tunajua sera yetu ya mikopo kwa sekta ya kilimo inatuongoza hivi. Wote mpo serikalini kaeni mzungumze," amesema.

Ametaka fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ziende kwenye mfuko wa pembejeo na benki hiyo kufungua madirisha maalumu kwa ajili ya wakulima.

"Ili kuona wakulima wanakopesheka mazao yanaongezeka na tuweze kuongeza thamani," amesema.

Amesema ni muda mrefu kulikuwa kukihitajika benki imara itakayowahudumia wana ushirika na sasa ndoto hiyo imetimia.

Amempongeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Katibu Mkuu wake, Gerald Mweli kwa kushirikiana na watendaji wengine kufanikisha hilo.

"Nilipomteua Gerald (Mweli-Katibu Mkuu) akitoka somewhere (eneo fulani) kuja kilimo, nikamwambia Bashe una uhakika mbona kama boss sana, wakati ule Mweli akiongea mabega yanapanda hivi... nikamwambia Bashe una hakika? akaniambia niamini mimi niletee huyu mtu," amesema.

Amesema Serikali inaimiliki benki hiyo kwa asilimia 10, tisa wadau wengine, wana ushirika asilimia 50 na hicho ni kielelezo cha nguvu cha ushirika wa sasa.

Amesema ni furaha yake kuona benki hiyo inazinduliwa ikiwa na mtaji wa Sh58 bilioni na itachangia kuongeza usalama wa mitaji.

Amesema anatarajia kila fedha inayowekezwa kwenye ushirika na kilimo itachochea taasisi nyingine za fedha kutoa mchango wao ili kuikuza sekta hiyo.

"Inatia moyo kuona mmejipanga kuhakikisha huduma zenu zinafika kwa uaminifu uadilifu kwa wakulima," amesema.

Amevitaka vyama vya ushirika na benki hiyo kupanua mtandao wake ili ifikike na kupatikana kwa urahisi.

Pamoja na nia ya kuendeleza ushirika, amesema benki hiyo itaendelea kuwa kama zilivyo nyingine na iwapo misingi yake itazingatiwa itatoa hakikisho la uimara na uwezo wa kujiendesha.

Kwa kuwa benki ya ushirika itakuwa sehemu ya mpango huo, amesema anatarajia itakuwa kipaumbele kutoa huduma za kisasa.

"Benki tunayoizindua leo ni ya ushirika sio kuja kupindua benki nyingine. Kuja kwa benki hii ni kuongeza nguvu ya kuwafikia Watanzania hasa wale wa vijijini kwa hiyo tushirikiane nayo. Najua biashara ya benki ni ushindani lakini tushirikiane nayo," amesema.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuona ushirika unachukua nafasi yake ili kuongeza tija kwenye kilimo na hatimaye pato la Taifa.

Alichokisema Bashe

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Dk Bashiru Ally na Rais Samia Suluhu Hassan wote ni wanahisa wa benki hiyo.

Ameeleza kuanzishwa kwa benki hiyo kutaifanya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), iendelee na jukumu lake la kutoa mikopo ya kugharamia miundombinu ya kilimo kwa muda mrefu.

Amesema TADB kisera ni benki ya maendeleo na kwamba haiwezi kuwa kibiashara, yenyewe inapaswa kuwekeza kwa muda mrefu na ilikuwa inatekeleza majukumu ya kibiashara kwa sababu hakukuwa na benki ya ushirika.

Bashe amemwomba Rais Samia katika fedha za pembejeo na ruzuku kama BoT haitakubali kufanya mageuzi ya mtindo wa uwezeshaji utakaosababisha kuwepo mifumo ya ukopeshaji kwenye mifugo na uvuvi, kutakuwa na safari ndefu ya kuzikuza sekta hizo.

"Mkulima akopeshwe kwa mtindo tofauti na anavyokopeshwa mwingine yeyote," amesema.

Amesema Dola 129 milioni zimepatikana na wameomba kuwe na dirisha la uwezeshaji na zitapelekwa na kutoa dhamana kwenye miradi ya kilimo ili iwe na riba nafuu tofauti na kwingineko.

Amesema fedha hizo hazitatoka serikalini bila kuwa na riba ya chini ya asilimia mbili hadi tatu.

Amesema benki hiyo ipo kwa ajili ya ushindani na benki nyingine za biashara na wanachokitaka ni kuhakikisha taasisi zote za fedha zinakuwa na jicho jepesi kwa wakulima.

Bashe amesema wakulima wote walioko katika vyama vya ushirika watafikiwa na huduma za kibenki kupitia ofisi za vyama vyao.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amesema ushirika ni sera ya msingi ya chama hicho iliyoirithi kutoka kwenye vyama vya ukombozi.

Amesema inafanyika hivyo, ikijulikana kwamba, shabaha ya kumkomboa mkulima ndiyo msingi wa ukombozi wa kiuchumi utakaowafanya watu wote waishi vizuri.

"Kazi hii inatimiza azimio la kuhakikisha kila mwananchi anaishi vizuri na wananchi waishi maisha ya leo mazuri kuliko ya jana," amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Uvuvi na Biashara, Deodatus Mwanyika amesema kilichofanyika ni kufungua pazia jipya katika sekta ya kilimo.

Ameambatanisha hilo na ombi kuwa, iwapo Bashe ataendelea kuwa waziri katika awamu ijayo ya Serikali aendelee kupewa wizara ya kilimo kwa kuwa ameiongoza vema.

"Viongozi wenye umahiri sio wengi sana, sisi tunakuachia wewe (Rais Samia). Kama Bashe anapandishwa kwenye nafasi za juu sisi ni nani kuzuia, lakini kama ataendelea kuwa waziri basi aendelee kuiongoza Wizara ya Kilimo, kwa sababu amesimamia vema," amesema.

"Wabunge tunaridhika mno kwa namna ambavyo Serikali yako inafanya kazi kwenye sekta ya kilimo," amesema Mwanyika.