Prime
Magari chakavu, kamari, bidhaa za urembo zaguswa kodi mpya
Dar es Salaam. Serikali imependekeza hatua mpya za kikodi kwa mwaka wa fedha 2026/27 zenye lengo la kuchochea uwekezaji, kuongeza uzalishaji, kulinda viwanda vya ndani na kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akiwasilisha mapendekezo hayo bungeni Alhamisi Juni 11, 2026, wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari amesema maboresho hayo yanalenga kukuza uchumi, kuongeza ajira na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kupitia sera rafiki kwa biashara na uwekezaji.
Amesema maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na sekta za uzalishaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta ya kupikia, pamba, nguo na mavazi pamoja na matumizi ya nishati safi.
Waziri huyo amesema mafuta ya kupikia ni bidhaa muhimu inayotumiwa na wananchi wengi na ina nafasi kubwa ya kuchochea uwekezaji, kuongeza ajira na kukuza mapato kupitia mnyororo wake wa thamani.
Hivyo, Serikali itaendelea kuweka vivutio vya kikodi ili kuhamasisha kilimo cha mazao ya mafuta, kuongeza matumizi ya mbegu zinazozalishwa nchini na kuimarisha viwanda vya ndani vinavyochakata na kuzalisha mafuta ya kupikia.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, msamaha huo ulianza kutekelezwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 na ulitarajiwa kumalizika Juni 30, 2026.
Nguo, mavazi vya ndani kunufaika
Katika sekta ya pamba, Serikali imependekeza hatua za kuendelea kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha vitambaa na bidhaa zinazotokana na pamba inayozalishwa nchini.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nguo na mavazi yanayozalishwa kwa kutumia pamba ya ndani.
Kwa mujibu wa Waziri Omar, hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya malighafi za ndani, kuimarisha ushindani wa viwanda vya ndani na kuongeza thamani ya zao la pamba.
“Hatua hii inatarajiwa kuokoa mapato ya Serikali yanayotokana na marejesho ya VAT kwa walipakodi yenye thamani ya Sh6.3 bilioni,” amesema.
Magari ya umeme kupewa nafuu
Katika jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, Serikali imependekeza kusamehe VAT kwenye vifaa vinavyotumika katika vituo vya kuchaji magari ya umeme vinavyoingizwa nchini.
Pia, imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme.
Waziri Omar amesema hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya nishati mbadala, kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na kulinda mazingira.
Kwa mujibu wa makadirio ya Serikali, utekelezaji wa hatua hizo utapunguza mapato ya Serikali kwa takribani Sh5.97 bilioni.
Amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na viwanda vya kuunganisha magari vilivyopo nchini ili kuweka utaratibu wa kutoa vivutio maalumu vya kikodi kwa wawekezaji watakaojihusisha na uunganishaji wa magari ya umeme hapa nchini.
Mita janja za gesi zaguswa
Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Serikali imependekeza pia kusamehe VAT kwenye mita janja za gesi ya kupikia (LPG Smart Meters) zinazoingizwa nchini.
Msamaha huo utatolewa kwa kampuni na taasisi zinazojihusisha na usambazaji wa gesi ya kupikia.
Kwa mujibu wa Waziri Omar, hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa Sh16.8 milioni, lakini itachangia kuongeza matumizi ya gesi safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa nishati zinazoharibu mazingira.
Kwa upande mwingine, Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwa magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, magari yenye umri wa miaka minane hadi 10 yatatozwa ushuru wa asilimia 20 badala ya asilimia 15 ya sasa.
Magari yenye umri wa zaidi ya miaka 10 lakini yasiyozidi miaka 20, yatatozwa ushuru wa asilimia 40 badala ya asilimia 30, huku yale yenye umri wa zaidi ya miaka 20 yakitozwa ushuru wa asilimia 50.
Waziri Omar amesema hatua hiyo inalenga kuongeza mapato ya Serikali na kudhibiti uingizaji wa magari chakavu ambayo huongeza changamoto za mazingira na gharama za usimamizi wa taka ngumu.
TRA kutumia akili unde kuongeza mapato
Mbali na hatua za kikodi, Serikali imetangaza mikakati mipya ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia teknolojia.
Waziri Omar amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaongeza matumizi ya Akili Unde (AI), mifumo ya kidijitali na teknolojia ya msimbo pau (barcode) katika kufuatilia bidhaa zinazoingizwa na kuuzwa nchini.
Amesema matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza ukwepaji kodi, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa mapato ya Serikali.
Matumizi ya fedha taslimu kuounguzwa
Katika hatua nyingine pia, Serikali imesema inadhamira ya kuendelea kupunguza matumizi ya fedha taslimu kwa kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Waziri Omar, hatua hiyo inalenga kupunguza ubadhirifu wa fedha, kuongeza uwazi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Sambamba na hilo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeelekezwa kuanza kuondoa matumizi ya vocha za simu za kukwangua kwa mkono na kuhamia mfumo wa kidijitali.
Amesema utekelezaji wake utaanza katika maeneo ya mijini kabla ya kusambazwa nchi nzima kulingana na matokeo ya tathmini ya awali.
Bidhaa za urembo, viatu vya plastiki, kamari zaguswa
Katika mapendekezo mengine ya kodi, Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa bidhaa za urembo zinazoingizwa nchini kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15.
Aidha, viatu vya plastiki vitatozwa ushuru wa asilimia 10, huku ushuru wa kamba za nyuzi za plastiki ukiongezwa kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 25.
Pia, imependekeza kutoza ushuru wa asilimia tano kwa magari yenye ujazo wa injini usiozidi CC 1,000 yanayoingizwa nchini.
Katika sekta ya michezo ya kubahatisha, imependekeza kutoza ushuru wa asilimia tano ya thamani ya dau kwa michezo ya kubashiri inayochezwa kwa njia ya mtandao au katika vituo.
Ushuru huo pia utahusisha michezo ya kasino, mashine za sloti na michezo mingine ya kubahatisha.
Waziri Omar amesema asilimia 10 ya mapato yatakayokusanywa kupitia ushuru huo yataelekezwa katika Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) ili kuimarisha udhibiti wa sekta hiyo.