Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa nini TTCL haiachi biashara ya simu licha ya nguvu ndogo sokoni?



Katika soko la mawasiliano linalotawaliwa na ushindani mkali kutoka kwa kampuni binafsi zenye uwekezaji mkubwa, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea kubaki kwenye biashara ya simu za mkononi licha ya kuwa na sehemu ndogo ya soko hilo.

Kwa muda sasa kumekuwapo na mjadala wa umma unaosema kuwa TTCL ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 inapaswa kujiweka kando na biashara ya simu na badala yake wajikite zaidi katika mkongo wa Taifa ambao ndiyo biashara yake kubwa kwa sasa.

Hata hivyo pamoja na maoni hayo Shirika hilo linaamini lina mchango mkubwa katika mawasiliano ya simu hususani usioonekana moja kwa moja na ndiyo maana limechagua kuendelea kushikilia pande zote sawa na watoa huduma wengine sokoni.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, anaeleza kwa kina sababu za kimkakati, kijamii na kiuchumi zinazolifanya shirika hilo kuendelea na biashara ya simu, hata kama haliko kileleni kwa idadi ya wateja.

Katika mahojiano hayo Mwananchi ilitaka kujua ni wapi mzani wa shirika umeegemea katika kutoa huduma kwa wananchi na kufanya biashara na Marwa anaeleza umuhimu wa kufanya yote.

“Kwetu yote yanaenda sawasawa kwa kweli,” anasema. “Kwa sababu tukiwa kama shirika ambalo linamilikiwa na serikali na ambalo limeanzishwa kwa sheria yake ya TTCL ya mwaka 2017 tumepewa majukumu ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma za mawasiliano kwa wananchi.”

Anasisitiza kuwa utoaji wa huduma (service part) hauwezi kutenganishwa na uendeshaji wa kibiashara. “Lakini vilevile kwenye hiyo sheria ambayo imetuanzisha imetuelekeza kwamba tuyaendeshe haya mambo katika hali ya biashara,” anaongeza.

Kwa tafsiri rahisi, TTCL inalazimika kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja: kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano bila ubaguzi, huku pia ikiendesha shughuli zake kwa ufanisi wa kibiashara bila kutegemea ruzuku ya Serikali kwa matumizi ya kila siku kama mishahara, maji au umeme.

Licha ya dhamira hiyo, takwimu zinaonyesha wazi kuwa TTCL ipo nyuma katika soko la simu za mkononi. Hii si siri, na Marwa anakiri hilo bila kificho lakini anaeleza sababu.

“Ni kama ulivyosema ni kweli, katika biashara ya simu za mkononi ukubwa wetu sokoni sio mkubwa,” anasema na kusema kuwa sababu kuu, kwa mujibu wake, ni uwekezaji mdogo ukilinganisha na washindani wao.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchi (TCRA) hadi Desemba 2025, kulikuwa na jumla ya laini hai za simu milioni 106.9 lakini TTCL ilikuwa inamiliki asilimia 1.6 ya soko hilo sawa na laini milioni 1.7.

Kwa upande wa mgawanyo wa dakika za huduma ya sauti ndani ya mtandao kwa kila mtoa huduma kati ya dakika bilioni 24.7 zilizopigwa mwezi Desemba TTCL ilikuwa na asilimia 0.3 kwa dakika bilioni 22.5 nje ya mtandao TTCL ilimiliki asilimia 0.9.

Hali hiyo haiishii katika dakika tu, kwa mujibu TCRA hata katika huduma za SMS, Intaneti ya simu na hata miamala ya simu shirikia hilo lina watumiaji wachache ikilinganishwa na wengine sokoni.

“Uwekezaji ambao wenzetu wanaufanya ukilinganisha na sisi ni mkubwa ambao unawasababisha waendelee kuwa bora zaidi katika kupata na kuhudumia wateja,” anafafanua Mara akije hoja kwa nini wao hawana utawala mkubwa wa soko.

Anasema kampuni binafsi za mawasiliano huwekeza zaidi ya Sh100 bilioni kila mwaka katika kuimarisha na kupanua mitandao yao ya simu. Kwa upande wa TTCL, kiwango hicho hakifikiwi hali inayopunguza uwezo wake wa kushindana kwa nguvu sawa.

Hata hivyo, alisema TTCL inaongoza katika eneo lingine muhimu ambalo ni huduma za fixed line (Simu za mezani) na faiba. Hapa ndipo shirika hilo limewekeza zaidi na kuona matokeo chanya, likiwa mhimili wa miundombinu ya mawasiliano ya intaneti nchini.

Aidha Marwa anasema moja ya changamoto kubwa zinazoikabili TTCL ni upatikanaji wa mtaji. Tofauti na washindani wake binafsi, TTCL inalazimika kupata ruhusa ya Serikali kabla ya kukopa au kufanya uwekezaji mkubwa.

Marwa anaeleza wazi hali hiyo: “Huku Serikali kuna mahitaji mengi hivyo eneo hilo linaweza lisipewe kiwango cha fedha ambacho kinatakiwa.”

Hii ina maana kuwa hata kama TTCL ina mipango ya kupanua mtandao wake wa simu, utekelezaji wake unaweza kuchelewa kutokana na vikwazo vya kifedha tofauti na washindani wake ambao mchakato wao unaweza kukamilika ndani ya mwezi mmoja.

Marwa anasema shirika hilo linafanyia kazi mbinu mpya za kuongeza uwezo wake wa kupata fedha, ikiwa ni pamoja na kukopa kama wanavyofanya washindani wao lakini kwa kufuata taratibu za Serikali.


Je, TTCL inapaswa kuacha biashara ya simu?

Kwa mantiki ya kawaida ya biashara, kampuni ambayo haifanyi vizuri kwenye eneo fulani inaweza kuchagua kujiondoa au kuacha biashara hiyo na kuelekeza nguvu zake kwenye maeneo yenye faida zaidi. Lakini kwa TTCL haijafanya uamuzi huo.

“Kuna wakati ambapo kunakuwa hakuna mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma wengine kwenda kutoa hizo huduma kwa wananchi,” anasema Marwa.

Hapa ndipo dhana ya “huduma kwa wote” inaingia. Serikali ina jukumu la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za mawasiliano, bila kujali kama eneo analoishi lina faida kibiashara au la.

“Katika huduma ni muhimu kwamba hizi huduma ziwafikie watu wote mawasiliano yanawezesha huduma za kijamii na kiuchumi,” anasisitiza.

Kwa maneno mengine, TTCL ni kama mkono wa Serikali unaofika mahali ambapo soko halivutii wawekezaji binafsi hasa maeneo ya vijijini au yenye idadi ndogo ya watu.

“Ukiachia tu hizi kampuni ambazo zinajiendesha kibiashara… kuna baadhi ya maeneo ambayo biashara haiwezi kutengenezeka lakini huduma lazima ziwafikie wananchi,” anaongeza.

Hivyo, hata kama biashara ya simu haina faida kubwa kwa TTCL kwa sasa, ina thamani kubwa kijamii na kiuchumi.


Hofu ya uingiliaji wa Serikali

Katika jamii, kumekuwa na hofu miongoni mwa baadhi ya wananchi kwamba kutumia huduma za TTCL kunaweza kufungua mlango wa Serikali kuingilia mawasiliano yao binafsi lakini Marwa anapinga mtazamo huo.

“Uoga huo hauna uhalisia ni mtazamo tu hasi,” anasema na kuongeza kuwa “Kama kuna mwingilio wa Serikali kinachoweza kutupata sisi kinaweza kumpata yeyote hapa nchini.”

Anasisitiza kuwa taratibu na viwango vinavyotumika vinasimamiwa na mdhibiti wa sekta ya mawasiliano (TCRA) na vinawahusu watoa huduma wote bila ubaguzi. “Hakuna utenganisho wa kwamba TTCL inatazamwa kwa karibu zaidi kuliko wengine,” anaeleza.

Hasara na ufanisi wa Shirika

Kwa miaka mingi, TTCL imekuwa ikitajwa katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama shirika linalopata hasara. Hata hivyo, hali hiyo imeanza kubadilika.

Marwa anasema tangu alipochukua uongozi, shirika hilo limeanza kuonesha dalili za mafanikio ya kifedha. “Tumetoka kwenye hasara ya bilioni 18 na kutengeneza faida ya bilioni 22.9 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025,” anasema.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/2026, TTCL tayari imepata faida ya zaidi ya Sh15 bilioni na inatarajia kuvuka kiwango cha mwaka uliopita ifikapo Juni.

Mabadiliko haya, kwa mujibu wa Marwa, yanatokana na mageuzi ya ndani na msisitizo wa kujiendesha kibiashara.

“kwa miaka ya nyuma ripoti ya CAG ikitoka moja ya habari kubwa ilikuwa ni hasara ya TTCL lakini hilo jambo sasa limebaki kuwa historia. Siri ya mafanikio ni mabadiliko katika shirika na hata matarajio ya Rais ni sisi kujiendesha kibiashara,” anabainisha.