Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa nini ni hatari kwa nchi kutegemea sekta ya madini

Katika historia ya maendeleo ya kiuchumi, mataifa mengi yenye utajiri wa rasilimali za madini yamejikuta yakikabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na utegemezi mkubwa katika sekta hiyo.

Ingawa madini yanaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa serikali na wawekezaji, utegemezi wake kupita kiasi huleta hatari ya kuyumbisha uchumi wa taifa.

Soko la madini linakabiliwa na mabadiliko makubwa ya bei kutokana na mahitaji na hali ya uchumi wa dunia. Kwa mfano, bei ya mafuta, dhahabu, shaba, au madini mengine inaweza kupanda au kushuka kwa kiasi kikubwa ndani ya muda mfupi.

Hii inamaanisha kuwa nchi inayotegemea madini kama chanzo kikuu cha mapato inaweza kuathirika vibaya pale bei zinapoporomoka.

Mfano halisi ni Venezuela, ambayo ilitegemea mapato ya mafuta kwa zaidi ya 90% ya mauzo yake ya nje. Kushuka kwa bei ya mafuta mwaka 2014 kulisababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi, kushuka kwa thamani ya fedha yake, na uhaba wa bidhaa muhimu.

Madini pia ni rasilimali zinazoweza kuisha. Nchi inapoendelea kuchimba madini kwa kiwango kikubwa bila mikakati ya muda mrefu ya kuwekeza katika sekta nyingine, hatari ya kuishiwa na rasilimali inakuwa kubwa.

Mataifa kama Zambia, ambayo yalitegemea sana shaba katika miaka ya 1970, yalijikuta katika mdororo mkubwa wa kiuchumi baada ya kushuka kwa bei ya shaba na kupungua kwa uzalishaji wake.

Jambo lingine ambalo huathiri uchumi unaotegemea sekta ya madini ni teknolojia mpya ambazo zinaweza kupunguza mahitaji ya madini fulani. Kwa mfano, maendeleo katika nishati mbadala yamepunguza kwa kiasi fulani utegemezi wa mafuta, na mabadiliko katika utengenezaji wa betri yamepunguza mahitaji ya madini fulani.

Hii inamaanisha kuwa nchi inayotegemea madini fulani inaweza kujikuta katika hali ngumu ikiwa maendeleo ya teknolojia yatapunguza thamani ya rasilimali zake.

Mchambuzi wa uchumi, Profesa Abel Kinyondo anasema sekta ya madini inabadilika sana, siyo ya kuiwekea moyo kwani leo inaweza kukuinua kesho ikaweka chini.

“Ni sekta ambayo inaathiriwa sana na mabadiliko ya teknolojia, kadri teknolojia inavyobadilika baadhi ya madini yanakosa soko. Mathalani kama si vita vya Russia na Ukraine, gesi ilishaanza kusemwa kuwa ni nishati chafu,” anasema Profesa Kinyondo.

Mhadhiri huyo wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema ni hatari kuitegemea sekta ambayo inaathiriwa muda wowote na ili kukabiliana na athari zake lazima uwe tayari.

“Nikeli ambayo tulikuwa tunaishangilia kuwa ni madini muhimu na ya kimkakati hivi sasa wazilishaji wote wapo kwenye ‘maintenance’. Hawaendelezi chochote mpaka bei itakapopanda,” anasema Profesa Kinyondo.

Mchumi huyo anasema yeye anaitazama sekta ya madini kama kichocheo cha kukuza sekta nyingine lakini sio kuitegemea kwakuwa kuna hadithi mbaya kwa nchi zilizoweka utegemezi huko.

Anasema miongoni mwa athari hasi za sekta ya madini ni kuharibu mazingira, kuongeza mfumo wa bei katika maeneo ye uchimbaji na kudumaza sekta nyingine muhimu kwa kila mtu kukimbilia neema iliyoko kwenye madini.

Kuhusu utegemezi wa sekta ya madini, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakirasilimali, Adam Antony anasema nchi haipaswi kutegemea sekta ya madini kwa sababu bidhaa zake huwa zinabadilika sana bei hivyo ni vigumu kutabiri kesho yake itakuwaje.

“Hata ukiangalia hapa nchini kwetu mapato tunayoyapata mara nyingi ongezeko lake halitokani na kuongezeka kwa uzalishaji isipokuwa ni bei inakuwa imeongezeka hivyo kama kuna kuongezeka kwa bei kushuka pia kunatakiwa kutarajiwa,” alisema.

Anasema kawaida pesa inayopatikana kwenye madini inapaswa kuwekezwa kwenye maeneo mengine ambayo uzalishaji wake ni endelevu na yanaajiri watu wengi akitolea mfano sekta ya kilimo na viwanda.

Kadhalika Antony anasema sababu nyingine ya kutotegemea madini ni kwa kuwa yanaisha, hivyo hayatapatikana siku zote hivyo ni muhimu kuwekeza kwenye sekta ambazo zina uhakika wa kuwepo kwa muda mrefu.

Anasisitiza kuwa ni vyema fedha inayotokana na madini isitumike kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya nchi kama kulipa mishahara, kwani siku ikikosekana itakuwa vigumu kumweleza mtu kuwa mshahara wake unatakiwa upungue.


Matarajio ya wananchi

Ingawa sekta ya madini inaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, kutegemea sekta hiyo pekee ni hatari. Historia imeonyesha kuwa nchi zinazotegemea madini hupata changamoto kubwa za kiuchumi pindi bei zinaposhuka au rasilimali hizo zinapokaribia kuisha.

Wananchi pia wanapaswa kuwa na matarajio ya wastani juu sekta ya madini, kwa kuelewa kuwa madini peke yake hayawezi kuleta maendeleo endelevu bila mikakati madhubuti ya kiuchumi na uwekezaji katika sekta nyingine muhimu.

Katika nchi nyingi zenye utajiri wa madini, wananchi wana matarajio makubwa kwamba rasilimali hizo zitabadilisha maisha yao kwa haraka. Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa matarajio haya mara nyingi huleta mivutano ya kisiasa na kijamii. Migomo, maandamano, na migogoro ya rasilimali mara nyingi hutokea pale wananchi wanapohisi kuwa wananyimwa haki yao katika utajiri wa madini.

Nchini Nigeria, mapato makubwa kutoka sekta ya mafuta yamesababisha matarajio makubwa kwa wananchi, lakini kutokana na usimamizi mbovu na rushwa, utajiri huo haujawanufaisha watu wengi. Matokeo yake, kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara katika maeneo yanayozalisha mafuta, kama Delta ya Niger.

Uzoefu wa mataifa mbalimbali umeonyesha kuwa utegemezi wa madini unaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiuchumi kama Dutch Disease (Kudorora kwa sekta nyingine) na Resource Curse (Laana ya rasilimali).

Dutch Disease hutokea pale ambapo mapato makubwa kutoka sekta ya madini au bidhaa nyingine za uziduaji husababisha thamani ya fedha ya nchi kupanda, na hivyo kufanya sekta nyingine kama kilimo na viwanda kuwa duni katika ushindani wa kimataifa.

Mataifa kama Uholanzi (baada ya kugundua gesi asilia), Nigeria, na Venezuela yamekumbwa na tatizo hili, likisababisha kuporomoka kwa sekta za uzalishaji nje ya madini.

Resource Curse ni hali ambapo mataifa yenye rasilimali nyingi hushindwa kufanikisha maendeleo kwa sababu ya utegemezi mkubwa kwa sekta hiyo, ufisadi, na ukosefu wa sera madhubuti za kiuchumi. Nchi kama Angola, Sudan Kusini, na DRC zimekumbwa na changamoto hizi, licha ya utajiri mkubwa wa madini.


Tanzania hali ikoje

Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali za asili na sekta ya madini imekuwa ikichangia zaidi ya asilimia 10 katika pato la taifa la miaka ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/2025 iliyosomwa na Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, katika miaka 20 iliyopita Tanzania iliuza zaidi mazao ya kilimo wakati sasa mauzo ya nje yanatawaliwa zaidi na madini.

“Pia katika miaka 20 iliyopita tuliuza zaidi bidhaa zetu katika masoko ya Ulaya, Marekani na Afrika lakini kwa sasa tunauza zaidi katika masoko ya nchi za Asia (China, India), Kenya na Uganda na nchi za Mashariki ya Kati,” alisema Profesa Mkumbo.

Hata hivyo katika miaka ya 2000, bidhaa zilizokuwa zikiuzwa sana ni dhahabu kwa asilimia 11.6, almasi (7.47), Fish fillet (13.9) nazi, Brazil nuts na korosho kwa asilimia 8.18, pamba ghafi (4.48), tumbaku ghafi (7.34) na kahawa kwa asilimia 9.22.

Hilo lilibadilika na miaka ya kuanzia 2020, dhahabu sasa ilikuwa ikibeba asilimia 39.9 ya mauzo yote ya nje huku mazao ya nazi, Brazil nuts na korosho ambayo ndiyo yalifuata kwa kuuzwa nje kwa kiasi kikubwa yakiwa na asilimia 6.52 pekee, huku mazao kama pamba, kahawa yakiwa na mauzo ya chini ya asilimia nne kila moja.