Kilimo cha chai kufufuliwa kukidhi mahitaji ya kiwanda

Muktasari:
Akizungumza baada ya kukagua kiwanda cha kuchakata majani ya chai juzi, Mlingwa alisema kinafanya kazi chini ya kiwango na historia inaonyesha kinaweza kuajiri vijana wengi na kuondokana na umaskini.
Tarime. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa ameuagiza uongozi wilayani hapa kutoa elimu ya kilimo cha chai ili liwe zao la biashara.
Akizungumza baada ya kukagua kiwanda cha kuchakata majani ya chai juzi, Mlingwa alisema kinafanya kazi chini ya kiwango na historia inaonyesha kinaweza kuajiri vijana wengi na kuondokana na umaskini.
Mlingwa aliwataka wakulima kuacha kilimo cha mazoea badala yake waanze cha tija cha mazao ya biashara na ya chakula.
“Kiwanda hiki kinatakiwa kuanza kuchakata majani ya chai kwa ajili ya biashara ili vijana wajipatie ajira, lakini pia wakulima waache kulima kwa mazoea badala yake wajifunze kulima kisasa ili kuondokana na umaskini,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime, Apoo Tindwa alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika tani nane kwa siku, lakini kutokana na uhaba wa majani ya chai kinalazimika kusindika tani moja.
Tindwa alisema wananchi wengi hawana mwamko wa kilimo cha chai na kwamba, iwapo ekari 500 zitalimwa zinaweza kutosheleza mahitaji ya kiwanda tofauti na ilivyo sasa zinalimwa ekari 77 pekee.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga alisema zaidi ya miche 200,000 itagawanywa bure kwa wananchi ili waweze kulima chai na kujikwamua na umasikini wa kipato.
Luoga alisema wilaya hiyo haiwezi kukumbwa na baa la njaa kwa kuwa inapata mvua kwa mwaka mzima, hivyo wananchi wanaweza kulima na kuvuna chakula kwa kipindi hicho chote.