Hisa za upendeleo DCB kuwaletea tija Watanzania

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaut Julius (katikati), akikata utepe, kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la uuzaji wa Hisa za Upendeleo za Benki ya Biashara ya DCB, jijini Dar es Salaam leo. Wa nne kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Zawadia Nanyaro na wa tatu kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi pamoja na wawakilishi wa taasisi nyingine waliohudhuria.
Muktasari:
- Uuzaji wa hisa za upendeleo unatarajia kuwaletea wanahisa na Watanzania kwa jumla tija za kiuchumi.
Dar es Salaam. Katika kuwaletea wanahisa na Watanzania tija za kiuchumi, Benki ya Biashara ya DCB, imezindua uuzaji wa hisa za upendeleo, ikitarajia kupata zaidi ya Sh10.7 bilioni.
Hatua hiyo inakuja ili kuongeza kiasi cha mtaji wake unaofikia Sh15 bilioni kwa sasa, pamoja na mambo mengine kukidhi vigezo vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa uuzaji wa hisa hizo jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Novemba 11, 2024, Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Zawadia Nanyaro amesema uamuzi huo unakwenda sambamba na mikakati yao ya maendeleo ya miaka mitano katika kuongeza mtaji wake kutoka ulipo sasa hadi kufikia Sh61 bilioni.
Amesema uuzaji wa hisa za upendeleo unatarajia kuwaletea wanahisa na Watanzania kwa jumla tija za kiuchumi, baada ya kuongeza mtaji wa benki unaolenga kukuza biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati mitaji ya kukuza biashara zao.
“Bodi ya Wakurugenzi ya DCB iliidhinisha mpango mkakati wa miaka mitano ukijikita kwenye mambo makuu matano; kukuza mtaji wa benki kutoka Sh15 bilioni (2024) hadi kufikia Sh61 bilioni ifikapo mwaka 2028.”
"Pili ukusanyaji wa amana nafuu za benki kupitia wanahisa wakuu na wateja wetu, tatu kuongeza wigo wa mikopo bora itakayotolewa kwa ufanisi na umahiri, nne utaoaji wa mikopo kwa wateja wadogo wadogo na wa kati ili kuendelea kutimiza lengo la kuanzishwa kwa benki yetu,” amesema.
Jambo la tano ni kuboresha njia za utoaji huduma na kuongeza bidhaa zinazotolewa kwa njia za kijiditali.
Amesema bodi ya DCB pamoja na menejimenti ya benki ilipendekeza na kuidhinisha uuzaji wa hisa za upendeleo 97,646,913 zenye thamani ya Sh10.74 bilioni kwa bei ya punguzo ya Sh110 kwa kila hisa moja, kinyume na Sh160 iliyopo sokoni.
Aidha, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaut Julius ameipongeza benki hiyo kwa uamuzi huo uliofanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa na kupata idhini kutoka CMSA.
Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi amesema benki imeweza kutengeneza faida katika robo ya pili na ya tatu huku ikiendelea kutoa huduma za kibenki bila kusahau mkazo mkubwa katika huduma zake za kidigitali ili kuhakikisha Watanzania wengi wanafikiwa na huduma za kibenki.