Prime
Hii hapa kauli ya Rais Samia kwa mashirika, taasisi
Muktasari:
- Serikali yapokea gawio la Sh1.32 trilioni kutoka katika mashirika na taasisi inazomiliki hisa. Rais Samia atasema taasisi za umma zipimwe kwa matokeo badala ya takwimu.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema shabaha yake ni kuona suala la kujitegemea linaondoka kuwa dhamira na sasa linaanza kutekelezwa kwa vitendo ndani ya Serikali.
Aidha, amepongeza gawio la Sh1.32 trilioni lililotolewa na taasisi na mashirika ya umma kwa Serikali, akitaka utendaji wa taasisi hizo upimwe kwa matokeo, siyo takwimu za kubumba.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akizungumza kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu jijini Dar es Salaam, Julai 30, 2026.
Msisitizo wa kujitegemea umeshuhudiwa hata katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ya Sh62.3 trilioni. Katika bajeti hiyo, Serikali imeweka mkazo wa kukusanya mapato ya ndani kuliko kutegemea nje.
Rais Samia amesema hayo leo, Jumanne, Juni 30, 2026, alipohutubia Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema gawio ni sehemu ya lengo la kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi katika kugharimia shughuli za maendeleo.
Katika bajeti ya mwaka huu, amesema utegemezi wa nje ni mdogo na kwamba juhudi zikiongezeka katika bajeti za miaka miwili ijayo nchi itategemea zaidi rasilimali zake.
“Kadiri taasisi za umma zinavyoimarika, ndivyo Serikali inavyoimarisha uwezo wa kutekeleza vipaumbele vya maendeleo ya wananchi kwa rasilimali zetu wenyewe, ndani tunaelekea kujitegemea,” amesema.
Taasisi zijitegemee
Rais Samia amesema taasisi haziwezi kuendelea kutazama mtaji wa Serikali kama jibu la kila changamoto, ilhali baadhi zina mali zinazoweza kuvutia mitaji kwa njia halali na zenye tija.
Amesema uwekezaji wenye matokeo ni ule unaovutia mitaji, kupunguza gharama za kufanya biashara, kukuza ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
Ameelekeza kufanyika kwa tathmini ya taasisi zinazoweza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kukuza uwazi, kuimarisha nidhamu ya soko na kuwashirikisha wananchi katika umiliki wa uchumi.
Pia, amesisitiza tathmini zilizofanyika ziendelee na hatua za utekelezaji huku changamoto za kisheria zikibainishwa na kutatuliwa haraka.
Kuhusu utekelezaji wa dira
Katika hotuba hiyo, Rais Samia amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji taasisi zenye uwezo wa kuingia kwenye ushindani wa soko.
Amesema taasisi hizo zinapaswa kuwa imara na zenye uwezo wa kuhimili mazingira ya ushindani yanayobadilika.
“Lengo letu ni kuona jambo hili likitoka kwenye dhamira kwamba tuna dhamira ya kujitegemea na sasa tuingie katika njia ya kulitekeleza, tufikie kwenye kujitegemea,” amesema.
Amesema ni vigumu kujenga uchumi shindani kwa taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea, na kwamba kinachohitajika ni taasisi zinazopimwa kwa matokeo badala ya takwimu.
Amesema ripoti zenye takwimu nyingi hazina maana kama hazioneshi matokeo yanayoonekana katika uchumi na maendeleo ya taasisi.
Rais Samia amesema anachotaka kuona ni taasisi zinatoka kwenye takwimu na kwenda kwenye uhalisia, ambapo zikitoa namba basi matokeo yake yaonekane pia.
‘Mipango mizuri itafsiriwe’
Ameeleza Serikali ina mipango mingi mizuri, ikiwemo mipango ya maendeleo ya miaka mitano, lakini yote haitaleta tija kama haitatafsiriwa na kusimamiwa utekelezaji wake.
Ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuendelea kusimamia na kuratibu kampuni ambazo Serikali ina hisa ili kuhakikisha uwekezaji unaleta manufaa kwa Serikali, sekta binafsi na wananchi.
“Dira ya 2050 haitakamilika kwa mipango na utajiri wa rasilimali, bali itatekelezwa kwa namna rasilimali hizo zitakavyosimamiwa, kulindwa na kugeuzwa kuwa fursa, huduma na maendeleo kwa wananchi,” amesema.
Rais Samia amezitaka wizara na bodi za wakurugenzi zinazosimamia taasisi kuhakikisha zinatafsiri dira kwenye mipango ya kazi zao ili Taifa lisonge mbele.
Amesema kazi hiyo siyo jukumu la Msajili wa Hazina pekee, bali kila wizara ina wajibu wa kuhakikisha taasisi zilizo chini yake zinafanya kazi kwa ufanisi, zinaongozwa kwa weledi na zinapimwa kwa matokeo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango ya Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, Juni 30, 2026.
Amepongeza mafanikio yaliyopatikana, akisisitiza taasisi zisibweteke kwa sababu viwango vya mwakani vinapaswa kuwa vikubwa zaidi ya vya mwaka huu.
Amesema anachotamani kuona ni idadi ya taasisi zinazochangia mfuko mkuu wa Serikali ikiongezeka sambamba na kupungua kwa utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.
Amesema mashirika yameundwa, yamelelewa na kupewa ruzuku hadi kufikia yalipo sasa, hivyo yanapaswa kujitegemea na kurudisha serikalini kwa kuongeza mchango wao katika mapato ya ndani.
“Natamani kuona idadi ya taasisi zinazochangia mfuko mkuu wa Serikali ikiongezeka sambamba na kupungua kwa utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini,” amesema.
Gawio lenyewe
Awali, akitoa taarifa ya gawio, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema Serikali imekusanya Sh1.32 trilioni hadi Juni 29, mwaka huu, ikiwa ni gawio na michango kutoka mashirika na taasisi.
Kiwango hicho cha makusanyo ni ongezeko la Sh300 bilioni (sawa na asilimia 30) kutoka Sh1.02 trilioni kilichokusanywa Juni mwaka jana.
Tathmini ya mashirika
Mchechu amesema mapema Julai mwaka huu ofisi yake itafanya mapitio ya kina kubaini taasisi za umma zinazotakiwa kukatiwa au kupunguziwa utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitano utegemezi wa ruzuku za Serikali kwa taasisi zisizo za kibiashara umepungua kwa wastani wa asilimia 12.8.
Viongozi na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, Juni 30, 2026.
Amesema hatua hiyo itafanyika kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, kuhakikisha Serikali inazikatia au kuzipunguzia baadhi ya taasisi utegemezi, hasa kwenye fedha za mishahara na matumizi ya kawaida.
“Hili tunatarajia kwamba tutafanya mapema Julai kwa sababu tunafikiri pia, katika kipindi hiki cha uchumi na mwelekeo wake, lazima tuingie katika hali ya kujifunga mkanda na kujitegemea zaidi ndani kuliko misaada,” amesema.
Mashirika vinara kwa gawio
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kuwa kinara wa kutoa gawio kati ya taasisi zinazochangia mfuko mkuu wa Serikali, ikichangia Sh205.5 bilioni kutoka Sh181 bilioni za mwaka jana.
Mchechu ametaja mashirika mengine kuwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) iliyochangia Sh61 bilioni, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Sh42.8 bilioni, na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Sh27.9 bilioni.
Mengine ni Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Sh20.4 bilioni, Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha) Sh15 bilioni, na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Sh14.7 bilioni.
Yanayofuata ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) Sh11.4 bilioni, Shirika la Reli Tanzania (TRC) Sh11 bilioni, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Sh10.6 bilioni, na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) Sh10.1 bilioni.
Viongozi na wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, Juni 30, 2026.
Katika taarifa yake, TPA imesema mafanikio hayo yanaakisi kuimarika kwa shughuli za biashara ya bandari, ongezeko la mizigo inayopita katika bandari za Tanzania na juhudi zinazoendelea za kuboresha miundombinu na huduma.
Huu ni mwaka wa nne mfululizo kwa TPA kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa gawio la asilimia 15 ya mapato ghafi, hatua inayoonesha mchango wake katika kuimarisha mapato ya Serikali.